The Chant of Savant

Saturday 16 January 2016

Magufuli atafakari sana vita dhidi ya mihadarati


            Akihutubia bunge la kwanza akiwa rais, Dk John Magufuli aliwaahidi watanzania kupambana na biashara haramu ya mihadarati ambayo imekuwa aibu, kero na tishio kwa taifa. Alisema kuwa hatakuwa na simile na wauza unga na atawasaka vinara wote wa jinai hii. Kwa kazi ambazo ameishafanya na mifano yake, Magufuli anamaanisha asemacho na kusema amaanishacho. Kwani ana mapenzi na mipango ya dhati na kweli kwa watanzania ambao kadhalika wanamuamini na kuwa tayari kushiriki; na kushirikiana naye katika vita hii ya kulikomboa taifa.
            Pamoja na dhamira safi na juhudi kubwa za kupambana na jinai ya mihadarati, rais Magufuli anapaswa kufahamu baadhi ya mambo –kama hajayafahamu na kama anafahamu abadili mkakati kutoka ukalipiaji hadi ukamataji wahusika na kuwafikisha kunakostahili. Rais Magufuli ni msemakweli anayeamini katika uwazi. Sentensi “Msemakweli ni mpenzi wa Mungu” huwa haikauki kinywani mwake. Hata hivyo, mambo mengine –hasa yanayohusiana na usalama –hayahitaji ukweli kuwekwa wazi. Kwani kufanya hivyo kunaweza kumgharimu mhusika. Na huu ni ukweli tu.  Kwa mfano, wauza unga wameonyesha kuwa na uwezo mkubwa kifedha na kimkakati kiasi cha kuyumbisha utawala uliopita kiasi cha kujenga hisia kuwa wakubwa zake walikuwa na namna walivyokuwa wakinufaika na kadhia hii. Kwa kutumia fedha, ushawishi, mitandao na mikakati yao, wauza mihadarati waliweza kuuhujumu na kuuweka mfukoni utawala uliopita ukiachia mbali kuwaua baadhi ya watu walioshupaa kupambana na kadhia hii.
            Jambo la kwanza analopaswa kufanya rais na timu yake ni kupunguza maneno na kuongeza matendo. Achukue mfano wa rais wa Marekani, Barack Obama anavyopambana na ugaidi duniani. Obama huwa hasemi atafanya nini na vipi. Badala yake hutenda na kutangaza baada ya kutenda kama alivyofanya alipofanikiwa kumuua kiongozi wa mtandao wa al-Qaeda Osama bin Laden na vinara wengine waliouawa kwa kutumia ndege za drone kwenye maeneo sugu na mazalia ya ugaidi.obama husema machache na kufanya mengi na hii ndiyo siri ya ufanisi wake katika kupambana na ufisadi.  Hivyo basi, badala ya rais kuapa na kuahidi atapambana na wauza unga, anapaswa kuanza kuwasaka na kuwakamta ndipo atangaze. Anaweza kufanya hivyo hata kwa mafisadi, vidokozi, wala rushwa, wakwepa kodi na wahalifu wengine wanaokwamisha maendeleo ya taifa letu.
            Katika makundi yote ya kihalifu, hakuna kundi hatari na linalotishia usalama wa taifa letu kama magenge ya wafanyabiashara haramu ya mihadarati. Wana fedha, ushawishi, mitandao hata ndani ya serikali kiasi cha kuweza kutumia uwezo huu haramu na hatari kuhatarisha maisha ya yeyote anayetaka kuyaangamiza. Historia ni shahidi. Wako wapi akina Amina Chifupa waliojitolea kufichua uovu huu? Rejea jinsi rais mstaafu Jakaya Kikwete alivyopewa orodha ya wauza unga na wahalifu wengine akashindwa kuzifanyia kazi. Je aliogopa au kuzuiwa na nini? Je kulikuwa na namna alivyokuwa akinufaika na jinai hii au aliogopa hatari iliyoko nyuma ya magenge haya? Hivyo, rais –japo ni taasisi –anapaswa kuzingatia na kuchukua tahadhari dhidi ya kitisho hiki hasa ikizingatiwa kuwa wakubwa wa magenge haya wengine wamo serikalini na kwenye taasisi mbali mbali za binafsi na umma. Hakuna tahadhari na mkakati bora wa kuwazidi kete wahalifu kama kuwakamata kwanza na kutangaza baadaye. Maana unawastukiza na kuwanyima nafasi ya kujihami kwa kuhujumu mikakati yako.  Magenge ya wauza mihadarati ni tishio hili si kwa Tanzania tu bali kwa dunia nzima.  Rejea kugundulika kwa wakubwa wa megenge ya wauza mihadarati wenye nchi ya Guinea Bissau ambapo mkuu wa majeshi aligundulika kuwa kingpin wa jinai hii. Rejea mauaji ya mameya, magavana na viongozi wengi wa juu nchini Brazil pale serikali ilipoamua kupambana na mihadarati. Rais bado anahitaji watendaji waaminifu na walio tayari kumsaidia katika mapambano haya.  Pia awatumie wala na wavuta unga ili kuelekeza vyombo vya upelelezi kwa wale wanaowauzia unga.
            Pamoja na ukweli kuwa rais Magufuli amekuwa serikalini kwa muda mrefu, hivyo, anajua aina ya magenge anayopambana nayo, anapaswa kuchukua tahadhari zaidi. Watanzania wanamkubali na kumpenda na wako tayari kushirikiana naye kukomboa taifa lao toka kwenye kashfa na aibu ya mihadarati, ufisadi, ujambazi, rushwa na uchafu mwingine. Pamoja na kujihami yeye binafsi, anapaswa kuwalinda watoa taarifa, wakamataji na magereza kwa ujumla kwa kuhakikisha wahusika wanapokamatwa hawataroshwi. Muhimu, rais angeaanza kukamata na kutangaza baadaye.
            Tumalizie kwa kumsisitiza rais umuhimu wa ukimya katika kuwasaka vinara wa biashara haramu ya mihadarati. Kamata kwanza, tangaza baadaye. Pia chukua hatua za haraka kuhakikisha vinara wa mihadarati wako magerezani na si uraiani wakipanga kuhujumu juhudi zako hata kukuangamiza. Kwa leo tunaishia hapa.
Chanzo: Tanzania Daima Januari 17, 2016.

2 comments:

Anonymous said...

Mwalimu Mhango,salaamu.
Nakubaliana na wewe kwa kila ulichokiandika katika makala hii na pia nakupongeza kwa mchango wako mkubwa wa mara kwa mara tangu Rais wetu wa awamu ya tano kuja madarakani.
Ni kweli kabisa hii biashara ya mihadarati ni moja ya janga kubwa la kitaifa katika nchi changa kama yetu,na kwa kuwa ni biashara iliyopevuka sana tangu Rais wa awamu ya nne kuja madarakani,Kwa maana kwamba nchi yetu ni biashara ambayo imechelewa sana kuja na bado changa,lakini kwa matandao wa biashara ya mihadarati inapofikia kuingia ngazi za juu kazi yake inakuwa ni NGUMU MNO kutokana na ushirikiano wa wafanya biashara wa nyumbani na wa kimataifa wa biashara hiyo.Kwa hiyo tangu Rais Magufuli kutangaza vita dhidi ya biashara hiyo ya Mihadarati bungeni ni wazi kwamba na kama inavyokuwa kawaida ya vigogo vya biashara hiyo hawatasalimu amri kirahisihisi kama tunavyotarajia.Balaa la biashara hii ni kwamba kuna soko la nyumbani na kuna soko la kimataifa naam Rais wetu anaweza kulimaliza soko la nyumbani ambalo kwa nchi yetu halina uzito wowote kulidhibiti kwa vile ni rahisi kuwadhibiti na kuwasimimisha wauzaji wadogo wadogo lakini kadhia ni sokol la kimataifa wakati nchi yetu imekuwa ni sehemu ya kuegeshea biadhaa hiyo na kama ujuwavyo watu hawa wa mihadarati walivyokuwa na mbinu mbalimbali za usafirishaji wa hali ya juu na kama ulivyomshauri Rais aende kimya kimya na wao kimya kimya hicho ndicho kitachowasaidia kufanya uovu wao kwa kimya kimya pia.

Nami kwa kuongezea sehemu ya ufumbuzi wa vita hivi endapo Rais amepania kweli kwa vita hivi inabidi atafute msaada wa kimataifa aidha kutoka nchi za ulaya au Marekani kwa kupambana na vigogo vya biashara hii ya mihadarati,isipokuwa kwa kutafuta msaada huo serikali ni lazima ijiandae kwani italigharimu taifa pesa nyingi sana,je Rais wetu yupo tayari kwa gharama hizo?Vita vya biashara ya Mihadarati sio vita lele mama kwani pesa yake inamtia kiwewe kwa kila ambaye anashiriki katika biashara hiyo kwa hatua ya juu.Na ikiwezekana iwekwe sheria ya muhusika wowote yule wa ngazi za juu kiserikali au mfanya biashara mkubwa akipatika na hatia ya biashara hiyo ni kutaifishwa mali zake ambazo zinadhaniwa kwamba amezipata kupitia biashara hiyo.

Naam Rais wetu anatakiwa awe makini na achukue hadhari kubwa endapo ameamua kweli kupambana na wafanya biashara hii ya mihadarati kwani isije nchi yetu katika hali hii ya kuijenga baada ya kubomolewa na kufisidiwa kwa miaka 30 iliyopita yakaja matatizo ya mauwaji ya kusafishana kwa sababu ya biashara hii kama inavyotokea katika nchi zingine ambazo biashara hii imejizatiti.

Mwalimu Mhango,inasemekana na kudaiwa kwamba Rais wa awamu ya nne aliifumbia biashara hiyo macho kwa ajili ya kuwapa vijana ajira na kuboresha maisha yao ya kijamii.Hata kama hilo ni dhana lakini kwa ukweli wa ardhini dhana hiyo inawezekana ikawa na ukweli mkubwa na moja ya sifa aliyojijengea JK ni hii ya kufumbia macho biashara hii ambayo kila sehemu ya jamii ilishiriki kikamilifu kuanzia vijana wa matabaka mbali mbali hadi waliokuwemo serikalini.

Nilikuwa na maoni tofauti katika hili au kama ni ombi kwa Rais wetu kwamba swala la Bangi asilitie katika vita ya biashara hii hususa baada ya kuthibitka kwamba Bangi ina faida kwa wavutaji wake na hakuna rekodi yoyote ile ambayo inayosema kwamba Bangi inawauwa watumiaji wake kwa namba kadhaa kama ilivyokuwa rikodi ya wavutaji wa sigara kama ni vita na aweke mibiginyo ya kutosha kwa wavutaji sigara hususa vijana wetu ambao wana rekodi nzuri tu ya uvutaji wa sigara,kwa kuongezea tu mababu zetu wameivuta sana Bangi na bado wanaivuta lakini tangu waje wababshiri wa dini za kigeni walipokuja na wameingilia kuipiga vita Bangi na kusema ni haramum na sisi tumekinaika kwamba Bangi ni HARAMU!

Na tuzidi kumuombea na kushirikiana na Rais Magufuli kwa yote anayoyapigania kwa ajili ya nchi na wananchi,Nawe uzidi kutoa ushauri wako na nasaha zako kila panapohitajika na kulazimika.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon, nakubaliana nawe kuwa bangi imegundulika kuwa na faida kitabibu na hakuna takwimu zinazoonyesha vifo vitokanavyo na uvutaji bangi. Nadhani bangi si mbaya kama sigara. Kinachotuponza ni imani za kizamani. Huku Ulaya imeanza kuhalalishwa kwa kasi kiasi cha kupunguza masharti dhidi yake wakati Afrika tukibana.
Hili la Kikwete kuwaacha wauza unga eti vijana wapate ajira sikuwa nalifahamu. Nitalifanyia kazi nijionee mwenyewe ila kama ni hivyo basi hawa vijana lazima awe na faida nao au wawe vijana wake. Maana kama ameruhusu wawekezaji kugeuka wachukuaji jambo ambalo linawanyima ajira vijana, kwanini awe na uchungu na vijana kwenye uhalifu.
Karibu tena.