The Chant of Savant

Friday 15 January 2016

Mlevi akataa tuzo kanyabwoya ya mlevi bora


            Kuna kijigazeti cha kitapeli kiitwacho Afro Jua Times kilitaka kuniingiza mjini na kunitumia kikidhani mimi ni njinga na mpenda kusifiwa ujinga kama wale wanaopenda kila upuuzi ilmradi wamesifiwa hata kwa ujinga.
            Kijigazeti hiki –ambacho bila shaka kinamilkiwa na matapeli wa kibongo na kinigeria eti kilinitangaza kama mlevi wa mwaka wakati hakuna nilichowafanyia walevi zaidi ya kushirikiana na wezi kuiba kanywaji kao. Eti kilitaka niende kupokea tuzo hii kichaa utadhani mimi kichaa au Njaa! Hata hivyo –hata ingekuwa kweli nimefanya mambo makubwa kwa walevi –nani anapaswa kujua ubora wa mlevi kati ya walevi na hawa matapeli wa ulaya? Nimewastukia hawa matapeli uchwara wanaotaka kunitumia niwapigie ndogo ndogo kwa Dk Kanywaji baada ya kugundua kuwa tulisoma wote na ni swahiba yangu mkubwa. Nasema wazi mmenoa na mkome na kukomaa. Bongo siyo shamba la bibi tena tangu rafiki yangu Dk Kanywaji akamate ukanda.
            Historia hii ya matapeli kutaka kunigeuza mumu au mpumbavu kwa lugha ya matapeli wa kinegeria inaanzia mbali. Kuna kipindi nilipewa shahada feki ya Udaktari na chuo kimoja cha mtaani kule majuu baada ya kugundua mimi ni kihiyo na mpenda sifa. Punde si punde nikapewa tuzo na wachunaji uchwara na baadhi ya NGOs. Kwa vile walinipata kabla sijawabamba kuwa ni matapeli, waliona mimi ni mumu ambaye wanaweza kumtumia watakavyo. Kama ni kuwa mumu basi wao ndiyo mumu ila siyo mlevi kama mimi bonge la mjanja ambaye nimepiga vitabu kuliko hata ninavopiga ulabu. Guess what. Nimepiga shule hadi nikafikia kibao kisemacho, il n’y a pas plus de classe pour vous. Yaani kwa kisambaa hakuna darasa hapa ndiyo mwisho.
            Kwa wanaotujua wasomi kama sisi na Dk Kanywaji, huwa hatupendi sifa za dezo hasa za kisomi au utendaji. Unakwenda shule haki la mlevi anaona. Unachapa mzigo hadi kila mvivu na mwizi anaona na kupigwa na butwaa. Kwanza, hawa matapeli wamepoteza muda wao. Mimi –sawa na Dk Kanywaji –si watu wa kutumia njuluku za walevi kwenda kuzurura ughaibuni. Si washamba wala malimbukeni wala watu wenye roho mbaya wanaojifanya kutoona jinsi walevi walivyopigika. Hata kama tuzo yenyewe ingekuwa ya ukweli nisingeunguza dola kwenda kupokea upuuzi. Kwa vile mimi ni fyatu, nilipopigiwa simu kuwa nimepata tuzo hii mavi niliamua kuwaambia –kama tuzo ni dili –wawape mama zao waliozaa na kulea matapeli wasiopenda kufanya kazi bali kutapeli wenzao. Walidhani mimi ni bongolala au Vasco da Gama mpenda kuzurura hata kwa vitu vya hovyo? Thubutu yao. Hawampati mtu hata kwa chembe.
            Kama ninastahiki tuzo, basi, tuzo hiyo nitapewa na walevi ambao napanga kuacha kuwabia na kuwatumikia kama Dk Kanywaji anavyotumikia wachovu wa kaya hii iliyokuwa imenajisiwa na vihiyo, mafisi, mafisadi, malimbuke, wavivu, wazururaji, wasanii na wajinga waliokuwa wakitumia masaburi kufikiri badala ya vichwa. Haya ya matapeli na matapeli watapeliwa wenzao tuyaache.
            By the way, ngoja niwape ishu bab kubwa ambayo itanitoa kiasi cha kugeuka bilionea na kuandikwa kwenye gazeti la Forbes. Guess what. Ninataka kuanza bishara ya kuingiza kayani mafuta machafu na kuwalangua wachovu. Maana siku zote sikujua kuwa kumbe wese feki lilikuwa dili na washenzi walikuwa wakiukata wakati sisi tunakatwa na umaskini, ukwete na ukapa! Kwa vile nimeinyaka. Lazima nianze kupiga dili ili nami niwe tajiri ati. Pia nataka kuanza biashara ya kulima miraa. Wasioinyaka misamiati yangu ni kwamba miraa ni mirungi ambayo kule kaya ya jirani ambako binadamu waliamua kujigeuza mbuzi wakibugia majani kama hawana akili nzuri miraa ni dili bab kubwa. Nimeishapata eneo kule upareni ambako nitalima hii kitu na kuula kama wengine.
            Wakati nikingoja wafanyakazi wamalize kulima hii kitu na kuvuna –kwa vile nimesoma ma-commerce, business na madude mengine ya kitapeli lazima nibadili jina na kujiita Mpayukaji Kanywaji ili niweze kuomba kazi pale Banki kuu sawa na vitegemezi vingine vya wanene vilivyojazana pale ambavyo Dk Kanywaji naona hajavistukia na kuvitumbua hata kama ni vijipu vilivyozaliwa na mabusha ambayo nayo hajayatumbua. Hii ikibuma basi nitaamua kufanya kitu kingine ambacho kitaishangaza dunia. Guess what.  Hebu soma taratibu, nitaanza kukusanya habari za Dk Kanywaji nijue kama ana kabinti ambako hakajaolewa nikaoe ili nami niwe mkwe wa dingi ili anikumbuke. Jamaa anavyopenda wachovu na wanyonge, najua atafurahi kusikia kuwa Ayatollah Mlevi ameamua kuwa mkwewe ili nibadili jina vizuri.
            Wakati nikisukuti jinsi ya kutoka, ngoja niende kwa mama Ndiza nikapate kanywaji halafu niende mitaa ya Lumumba kununua kete mbili hivi za bwimbwi nibembee kwenye maraha yangu nikiota kuwa bahari tena wa nchi kavu.
Chanzo: Nipashe Januari 16, 2016.

4 comments:

Anonymous said...

Salaamu Mwalimu Mhango,
katika dunia hii ya leo ya kuvishana vilemba vya ukoka,kukwezwa kwa uliyoyafanya,,usiyoyafanya na usiyoyajua.Dunia ya kufeki shahada za taaluma za juu,dunia ya kujikweza hata sehemu ambayo uwezi kufika ukadai umefika.Dunia ambayo kuna wengine wanatamani watukuzwe,wakwezwe kwa aina mbali mbali,dunia ya leo sifa za shahada ya juu ndio kana kwamba zinamwakilisha mwenye kubeba shada hiyo(zaidi ya taalamu yake ya kuajiriwa) kana kwamba amebobea katika kuishi vyema kitabia na kimaadili ndani ya familia yake,ofisini kwake au katka jamii yake imekuwa ndio piganio la kila msomi.Leo hii kumwita mtu kwa shahada yake ya udakitari,uhandisi,uhasibu na uwakili ndio fahari na ujiko kwa mtu huyo hata kama hana maadili bora ya kijamii.Mbona nchi za wenzetu zilizoendelea imekuwa sio ishu wala big deal kuitana majina kwa utamaduni huu wa utangulizi wa vyeti vya kusomea kupata kazi???!!!!!

Nakupongeza Mwalimu Mhango kwa kuikataa tunzo hiyo au utapeli huo.Na kama livyo kijamii kuzuka kwa waganga wengi wa kienyeji na matapeli wa kidini ni kutokana na kuzidi kwa wimbi la Sunami la itikadi ya dini,uchawi na kutokuwa na kukosekana kwa uwezo wa kufikiri kwa kutafuta sababu na visababisha kisayansi,na ndivyo hivyo hivyo kukuthiri kutafuta heshima na haiba ya kijamii kwa shahada za kielimu ndio kumezuka mtindo huu wa kuzuka kwa matapeli wa kila aina wa kuwakweza watu kuwapa tunzo,shahada na majina makubwa makubwa ya kielimu.Leo tunawasikia akina Dk JK na wa mfano wake kuwa wengi tu katika jamii zetu.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon, kwanza heri ya mwaka mpya na karibu tena ulingoni. Nashukuru kwa kunitembelea na kuacha unyayo. Nilikuwa bize kidogo kiasi cha kuchelewa kujibu. Shukrani kwa pongezi zako ambazo siku zote ni za dhati kweli kweli. Kuna haja ya kuwaeleza wapenda sifa na ibada za kipuuzi toka kwa binadamu wenzo kuwa kuna kipindi wanapatikana hasa na matapeli yanayotaka kuwatumia kama ilivyo kwa Njaa Kaya ambaye amejaziwa tuzo nyingi feki na matapeli ili angalau aguse mfukoni na kuwamegea toka kile alichowaibia watanzania.

Anonymous said...

Salaamu Mwalimu Mhango,

Nawe pia nakutakia heri hizo za mwaka mpya uwe mwaka wa heri,baraka na mafanikio katika mapambano yako na mchango wako wa kulitumikia taifa lako,wananchi wenzako na bara la Afrika.

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Anon, nashukuru sana kwa dua zako na unazidi kunipa motisha na moyo.