Wednesday, 16 November 2016

Kama Magufuli hataki kuchimbua makaburi anyamaze


 Image result for photos of mafisadi tanzania
          Hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli alikutana na waandishi wa habari katika siku ya kuadhimisha mwaka mmoja wa kuwepo kwake madarakani. Baada ya kuongea na waandishi wa habari, rais aliulizwa swali kuhusiana na mategemeo yake alipoingia madarakani. Akijibu swali aliloulizwa na mwandishi wa habari aitwaye Anna Kwambaza kuhusu mambo aliyoyakuta ikulu kama yalikuwa sawa na mategemeo yake, rais Magufuli, pamoja na majibu marefu, alikaririwa na akisema “nimeshughulikia changamoto mbalimbali lakini siwezi kuyafukuwa makaburi yote; kwa sababu kuna mengine nitashindwa kuyafunika, sikuja kufukua makaburi nataka kuanza na yale niliyoyakuta ili tujenge Tanzania yetu.” Hapa alimaanisha madudu aliyoyakuta Ikulu kama yalivyotendwa ima na watangulizi wake au yalivyovumiliwa kama kashfa mbali mbali ambazo zimelitikisa taifa kwa muda mrefu. Aliendelea mbele kutoa mfano kuwa ilifikia mahali ambapo meli zipatazo 60 zilitia nanga bandarini na kutoweka bila kulipa ushuru wala kuingizwa kwenye kumbukumbu yoyote. Hii ina maana kuwa nchi ilikuwa ikichezewa hakuna mfano. Je kama anachukizwa na uhujumu huu wa taifa, anashindwa nini kuunda tume ya kuchunguza kashfa hii na kuwabaini walioutenda na kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria hata kukamata mali zao? Je waliotenda uovu huu hawajulikani? Je hili nalo ni kaburi analoweza kulifukua akashindwa kulifukia?
            Kwa wanaojua namna Magufuli anavyojitahidi kuelezea uovu alioukuta kwenye serikali,  wapo wanaosema kuwa makaburi anayomaanisha Magufuli, ima unaweza kuwa uchafu wa watangulizi wake au hata wao wenyewe hasa ikizingatiwa kuwa ikulu kunaishi watu . Pia wapo wanaodhani kuwa rais anamaanisha kuwa mtangulizi wake alifuja madaraka kiasi cha nchi kufikia kujiendea kama vile hapakuwa na serikali wala kiongozi wa serikali. Hii inaweza kuwa kweli au vinginevyo. Yote inategemea namna unavyoliangalia suala hili na namna unavyotafsiri na kutathmini utendaji wa tawala zilizotangulia.  Maana, kama utaangalia ukweli wa mambo kwa kuzingatia ukweli na hali halisi vitokanavyo na utawala uliopita, utapata jibu kuwa hapa kuna tatizo tena kubwa. Kinachogomba hapa ni ukweli kuwa ni kwanini Magufuli alikuwa wa kwanza kumtetea mtangulizi wake na wenzake hata wale wanaojulikana kubariki uhujumu wa taifa kwa muda mrefu ukiachia mbali ufujaji wa fedha na mali za umma kama kweli anaamisha kuweka nchi kwenye mstari kama ambavyo amekaririwa mara nyingi akisema? Je kama rais mwenye vyombo vyote vya dola analalamika na kuishia kukiri kushindwa, amechaguliwa kufanya nini? Je hao wananchi wa kawaida ambao ndiyo waathirika wakubwa wasemeje au kufanya nini? wapo wanaodhani kuwa ima rais ayafukue makaburi na wananchi watamsaidia kuyafukia au ajinyamazie na kuchapa kazi pale anapoweza badala ya kutumikia mabwana wawili; yaani wananchi na hao wakubwa wa hovyo anaowalinda kwa kugopa kufukua makaburi wakati yanajulikana yamejaa uoza unaonuka?
            Bila kupambana na ufisadi bila kuwa na simile, Magufuli atajipiga mtama mwenyewe. Kwa vile amekiri kuwa amekuwa serikalini kwa zaidi ya miaka 20, anajua kila kitu na vipi kila kitu kiliharibika. Mfano, kuna kashfa zinazojulikana kama Escrow, UDA, TICTS, na nyingine nyingi tu zinazojulikana.
            Japo hataki kuchimbua makaburi kwa kushindwa kuyafukia, inakuwaje anaruhusu makaburi yaendelee kuwatesa wasio na hatia? Tuna makaburi ambayo yanachimbuka na kufikika hasa kama atawashirikisha wananchi na taasisi zake. Kwanini, kwa mfano, tusichimbue makaburi kama NBC, Richmond, SUKITA, Meremeta, Kagoda, UDA, DART, EPA, Escrow na mengine mengi ili kuepusha vifo vya watanzania wasio na hatia ukiachia mbali waliokwishafishwa na hayo makaburi? Je kama rais mwenye kila taasisi anaogopa makaburi, ataweza kuwakabili mafisadi wenyewe wachimba makaburi ya kufichia mali zetu? Kama Magufuli ameshindwa kuchimbua makaburi, basi ajitoe na kuwaachia wenye ujasiri wa kuweza kuyachimbua makaburi na kuyafunika. Je kwanini anaogopa makaburi? Atawezaje walio hai kama vile wauza unga, majangili, mafisadi kila aina wenye kuendelea kushikilia mitandao yao ya kihalifu?
            Alipoulizwa kuhusiana na kurejea mchakato wa Katiba Mpya, Magufuli aliogopa tena kugusa kaburi kwa kusema “tutengeneze nchi kwanza, nimezunguka nchi nzima wakati wa kampeni sikuzungumzia Katiba Mpya; kwa hiyo katiba zinaweza kuwa nyingi tu lakini kwa sasa mniachwe ninyooshe nchi kwanza.” Hapa nilishindwa kumwelewa Magufuli hasa ikizingatiwa kuwa Katiba Mpya iliyofishwa na mafisadi ililenga kupambana na ufisadi na kujenga taifa la uwajibikaji. Magufuli anapaswa kufahamu kuwa nchi si mali yake binafsi. Hawezi kuinyoosha kwa mapenzi yake bila kuwa na sheria inayomsaidia kufanya hivyo. Kama kweli anamaanisha anayosema, hana budi kurejesha mchakato wa Katiba Mpya kama watanzania walio wengi wanavyotaka badala ya kutoa visingizio. Lazima tujenge nchi kikatiba na si kwa kutegemea usongo wa mtu mmoja yaani rais badala ya Katiba Mpya ambayo ililenga kujenga taasisi zenye nguvu badala ya watu wenye nguvu katika kuendesha nchi. rais wa Marekani Barack Obama aliwahi kusema kuwa Afrika ahitaji mabwana au strong men bali taasisi imara yaani strong institutions. Na Tanzania kadhalika, inahitaji Katiba Mpya yenye nguvu badala ya rais mwenye nguvu na utashi wa kufanya atakavyo. Kama rais anaogopa kuchimbua makaburi kwa vile hawezi kuyafunika, awaachie wananchi wamasaidi kayafunika au ajinyamazie tu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: