Saturday, 5 November 2016

Kwa Hili, Naingia Bongolalaland Kuwekeza Ardhini

Baada ya kugundua kuwa kuna magabacholi wanaweza kuja Bongolalaland na kughushi vyeti vya kuzaliwa na kujizolea ardhi kila kona watakavyo kama alivyofanya Hamnazo Pateli, mlevi sitaki niachwe nyuma wakati naweza kuukata bila kutoa jasho. Nani hataki ulaji wa dezo hasa kwenye shamba la bibi tena bibi mwenye kipofu? Pamoja na ulevi na mibangi yangu, sikujua kuwa bado kuna walevi duniani wanaoweza kuchezea ardhi na mali zao asilia kwa kuruhusu majambazi na matapeli wa kigeni kuja kujineemesha wakati walevi tukiendelea kunyotolewa roho na ukapa, umaskini na ujinga wa kujitakia.
            Baada ya kuinyaka hii inshu, pamoja na kupanga namna ya kujilimbikizia ardhi na kwenda kuchukua mikopo na midebe benki na kuukata, nilitamani niwe dingi mwenyewe ili ninyonge wahalifu hawa. Kwani wanadhani mzee Mchonga wa Burito aliyelinda ardhi alikuwa juha kama wao siyo? Hapa lazima nife na mlevi kabla ya kuingia kwenye mishemishe ya kuukata kirahisi huku walevi wakiendelea kukodoa mimacho kama hamnazo. Pamoja na uroho na roho mbaya yao, hata manyang’au wa kwa nonihino hawajawahi kuruhusu ardhi yao ichezewe na matapeli wawe wa kitasha, kichainizi hata kigabacholi kama ilivyo kwa Bongolalaland bin Danganyika ya walevi uchwara. Mnauza na kugawa ardhi ili baadaye muishie kuwa wakimbizi kwenye kaya jirani siyo? Nani aliyewaroga nyie wanahizaya kiasi cha kuanza sasa kutuguza pabaya kwa uroho na uchoyo wenu ukiachia mbali upogo na upofu na tamaa vya kipumbavu?
            Hebu niulize swali la kichokonozi: Hivi kufuta hati za gabacholi aliyenyakua ardhi ndiyo jibu? Kwanini hamkumngoja akatia guu Bongo na kumtia lupango ili akajibu makosa ya kughushi hati na kujipatia mali kinyume cha sheria? Ningekuwa na lisirikali langu bila shaka hawa ningenyongelea mbali bila kusikia kelele za haki za walevi au kufunga maisha kama siyo kuramba shaba. Hapa lazima tujiulize maswali kibao. Je huyu gabacholi alisaidiwa na nani kupata na kughushi hizo nyaraka halafu akapewa ardhi kama hajatembeze kitu kidogo na kitu kikubwa? Je kuna genge la uuzaje ardhi ya walevi linalolenga kujineemesha kwa kuhujumu vizazi vijavyo? Hapa lazima dokta Kanywaji afe na mtu. Hapa hapahitaji kutumbua bali kuteketeza mwili wote uliooza.
            Baada ya kueleza mawazo na namna ambavyo ningeshughulikia kadhia hii, ngoja nizame kwenye dili lenyewe.
            Kwanza, nitaomba kazi kwenye ofisi ya vizazi na vifo  ili kuweza kuwa jikoni ambako vyetu feki na halali hutoka. Bila shaka hapa ndipo gabacholi alikochezea karata zake kwanza, kabla ya kwenda benki kuchukua mamilioni ya njuluku na kwenda zake majuu kutimia kwa raha zake.
            Pili, nitahakikisha napata mlevi wangu kwenye wizara ya ardhi ili nitakapotuma wateja wangu ambao nitawaghushia vyeti vya kuzaliwa wapete niendelee kupiga njuluku.
            Tatu, lazima niwe na washikajio kwenye wizara ya mambo ya kaya hasa kwenye idara ya uhamiaji ambayo nitaitumia kama ya uhamishaji kama hawa wanaogawa ardhi kama hawana akili nzuri. Hapa, hata washikaji zangu wa kineigeria wanaosifika kwa kusafirisha bwimbwi lazima niwatoe njuluku ili wapate pasi za Bongolalaland na kusafirishia kago zao bila kustukiwa sana.
            Nne, nitahakikisha napenya hata kwenya mabenki ili kuwawezesha wateja wangu nitakaowaghushia vyeti vya kuzaliwa wakapata ardhi ili waende huko kukopa kwa kuweka ardhi poni na kupata minjuluku kama alivyofanya gabacholi huyu ambaye bila shaka ana uhusiana na yule habithi Chavda aliyechukua mashamba yetu ya mkonge na kukopa njuluku na kutokomea zake ugabacholi kutumia na wachovu wa huko huku wachovu wa hapa wakiendelea kupika wakati mali wanayo lakini wanaikalia na kuifuja.
            Mwisho, tuache utani na ujuha. Unapochezea ardhi, licha ya kuchezea amani, unaua mstakabali wa kaya hasa vizazi vijavyo. Achene ujuha na ufisi mthamini na kutunza mali za umma. Napendekeza wahusika wote wanyongwe. Na kwa taarifa yenu, hii biashara nimebadili mawazo. Sifanyi. Badala yake nitawawinda wale wote wanaouza vyeti vyetu vya kuzaliwa ili niwafanyie ugaidi kinomi. Thatha naona niishie hapa.
Chanzo: Nipashe Jumamosi, leo.

No comments: