The Chant of Savant

Sunday 27 November 2016

Nchi ya viwanda Escrow, UDA, NSSF nk wapi na wapi?

          Baada ya rais John Pombe Magufuli kuingia madarakani na kukuta madudu na mdororor wa uchumi, alikuja na mipango ya kuifanya Tanzania nchi ya viwanda. Magufuli, pamoja na mengini, alilenga kutengeneza ajira, kufufua uchumi, kuwezesha watanzania kupata huduma safi na kufaidi raslimali za nchi yao na kuboroesha maisha ya watanzania.
            Pamoja na mipango na nia nzuri vya rais, kuna mambo yanapaswa kuwekwa wazi kabla ya kuendelea kujiaminisha kuwa tunaweza kujenga Tanzania ya Viwanda bila kuyakabili bila simile. Yafuatayo ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika safari yetu ya kwenda nchi ya viwanda:
            Mosi, kwanza tuunde sera ya kitaifa ya viwanda bila kutegemea sera ya chama kinachotawala. Hapa lazima tubadili katiba na kutamka wapi Tanzania inapokwenda na itafanya hivyo vipi. Kwani, kwa sasa, sera ya viwanda ni ya kisiasa na si ya kiuchumi. Mpaka sasa si rahisi kuelezea Tanzania inatumia mfumo na sera zipi zaidi ya ujamaa unaoendelea kubakia kwenye katiba wakati haupo tena.
            Pili, lazima tuliandae taifa kwenda kwenye nchi ya viwanda. Mfano, tueleze tutakavyovuna nguvu kazi iliyopo na kutengeneza wataalamu wa kutufikisha kule. Hata nchi ya Ulaya zilipoamua kufanya mapinduzi ya viwanda (industrial revolution), pamoja na kutumia nguvu kazi ya bure ya watumwa, zilijiandaa kupata na kuvuna nguvu kazi hiyo. Kwa sasa utumwa haupo tena. Tuna watu wetu; tuwaandae na kuwatumia vilivyo. Kwani mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe. Je tumewaandaa wananchi wetu kwa kuijenga nchi ya viwanda au tutategemea wawekezaji wasioaminika na ambao wanaweza kuondoka wakati wowote maslahi yao yanapoguswa?
 Tatu, lazima tupambane na ufisadi kwa maana ya kupambana bila kubagua, kubangaiza, kuonea wala kupendelea.
            Nne, tuangalie kama sheria zetu zinapambana na ufisadi na wizi wa mali za umma na makosa yatokanayo na hayo. Kama hazifai tuzibadili au kutunga mpya na kufuta nyingine.
            Tano, tumifunze toka kwa nchi zilizotoka kwenye mazingira kama yetu. Kwani, nchi ya viwanda kama China haijengwi kwa woga na matamanio bali mipango madhubuti na ya makusudi.  Huwezi kujenga nchi ya viwanda wakati huandai maisha ya kuzalisha na kukusanya kodi vilivyo. Tunapaswa kuwashughulikia wote wanaotukwamisha na waliotukwamisha bila huruma. Hapa lazima wahusika wafilisiwe na watanzania wawe na mfumo wa kila mmoja kutoa taarifa za kodi na mapato kila mwaka ili kubaini wanaotuibia na kutukwamisha. Huwezi ukajenga nchi ya viwanda katikati ya kashfa kama EPA, Escrow, NSSF, UDA na nyingine nyingi ambazo karibu tawala zote zimeonyesha kuzigwaya au kuzivumilia kwa sababu wajuazo wahusika.    
            Sita, nchi ya viwanda inahitaji mtaji ambao nao unaibiwa na tunaangalia au kusuasua kushughulikia majizi yanayojulikana kwa sura na majina. Hivi kashfa tajwa hapo juu zilisababisha taifa hsara ya mabilioni mangapi? Je fedha hiyo ingejenga viwanda vingapi au kusaidia kuweka msingi wa viwanda nchini kama ingesimamiwa vizuri au kuwakamata wahusika wakairejesha?
             Saba, je tunahofia nini na tunamdanganya nani kwa kutaka kujenga nchi ya viwanda bila sera ya kitaifa iliyowekwa kwenye katiba ya nchi? Haiwezekani tukashughulikia kashfa ya NSSF kwa kuchagua. Inakuwaje, kwa mfano, aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa NSSF ateuliwe balozi badala ya kuchunguzwa kusikia ana ushahidi na utetezi upi kuhusiana na kashfa iliyotendeka chini ya uangalizi wake?
            Nane, kama ilivyodokezwa hapo juu, China imepiga hatua kwa kasi ya ajabu kiuchumi kutokana na kasi ya ajabu katika kushughulikia ufisadi na wizi wa mali ya umma. Imeishafunga vigogo zaidi ya milioni moja tangu idhamirie kubadili mwelekeo wa maendeleo yake. Zamani nchini China ukiwa kwenye chama tawala basi umeula na huguswi sawa na ambavyo ilivyo nchini ambapo baadhi ya wazito wanatuhumiwa hata kusafirisha nyara za taifa ughaibuni na bado wako ofisini ukiachia wale waliotuhumiwa wazi wazi kujihusisha na mihadarati.
             Kwa mujibu  wa Kamati kuu ya Ukaguzi wa Nidhani ya China (CCDI), serikali ya China  imeanzisha kampeni tangu rais Xi Jinping  achukue usukani wa  Chama  Kikomunisti cha China (CCP) mwishoni mwa mwaka 2012, maafisa wa ngazi za juu 414,000 wameishawajibishwa na chama kwa ufisadi; na maafisa wapatao 201,600 walishashitakiwa. Mfano kwenye mkoa wa Shanxi, mmoja wa mikoa fisadimaaafisa wapatao 15,450 walipatikana na hatia mwaka jana ambalo ni ongezeko la aslimia 30 ikilinganishwa na mwaka 2013.  Kauli mbiu ya inaelezea hatua hii kama kuua chui na kupunga inzi.
            Tisa, ukiangalia maendeleo ya kupiga vita ufisadi iliyofikia China, kwetu ni kinyume. Tunaua inzi na kupunga mapapa. Vinginevyo walioko nyuma ya kashfa tajwa hapo juu wangekuwa wameishauwa na si kupungwa.
            Kumi, na mwisho, tunasisitiza kuwa lazima tubadili katiba na kuja na katiba mpya ya uwajibikaji na uchapa kazi badala ya kutegemea nguvu ya kisiasa chama au mtu mmoja. Nchi ya viwanja inajengwa na wananchi wote wanapotambua na kujua wanachotaka na wanachotaka kufanya.
Nashauri tuanzie kwa haya machache, pamoja na mengine, kuiandaa Tanzania kwenda kwenye nchi ya viwanda.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: