Wednesday, 23 November 2016

Kijiwe chashangaa wanaoshupalia njuluku ya tetemeko


         
            Wiki jana baada ya vyombo vya umbea kusheheni malalamiko ya wahanga wa tetemeko kule kwa akina Nshomile, Kijiwe kimeamua kuingilia kati lau kutoa elimu na ushauri vya bure.
            Leo anayeanzisha mada ni Mipawa tokana na baadhi ya marafiki zake aliokwenda nao shule kukumbwa na tetemeko ikiwemo shule alikosomea kidato cha tano na sita kabla ya kwenda Ng’ambo kunyaka shahada zake nyingine. Anaonyesha gazeti la Rongorongo lenye kichwa cha habari “Wahanga wa Tetemeko waijia juu Lisirikali.”
            Anatongoa “mmeona hii kasheshe kati ya wahanga na akina Nshomile baada ya lisirikali kusema kuwa njuluku iliyokusanywa itaelekezwa kwenye ujenzi wa miundombinu badala ya mbavu za mbwa binafsi? Jamaa wanapokoma kama hawana akili nzuri.”
            “Kwa lisirikali la sasa watalia sana na wamechemsha. Si rahis keshasema kuwa si kazi ya lisirikali kunjengea mchovu; sasa wanadhani malalamiko yatasaidia,” anachomekea Mbwamwitu.
            Msomi Mkatatamaa anakula mic “hapa nakubaliana na lisirikali. Kwani miundombinu ni muhimu kuliko wachovu binafsi. Nadhani wanaolalamika–pamoja na kuwa ni haki yao kufanya hivyo–wanapaswa kujiuliza baadhi ya maswali hata kama si ya kufurahisha. Mfano, mbona mbavu zao za mbwa zilipopukutishwa na tetemeko, wengi licha ya kulilalamikia na kupata misaada toka kwa lisirikali hilo hilo wanaloliaani sasa walitegemea miundombinu hiyo hiyo hiyo kama vile mashule, barabara, kliniki na mahospitali kupata huduma za kwanza, kujihifadhi na hata baada ya hapo? Mnyonge mnyongeni; lakini haki yake mpeni jamani.”
             Kabla ya kuendelea Mgoshi Machungi anamchomekea na kusema “Kwei Mgoshi, shue ni bora kuiko ubavu wa mbwa wa mchovu binafsi.  Nadhani badaa ya kulaamika, waathiika wanapaswa kukaa na seikai na kuangalia namna ya kusaidiana akini siyo kuazimishana na kutoa laana bue.”
            Kapende aliyekuwa ndiyo anamaliza kusoma gazeti la Rongorongo anakatua mic, “nasikia lisirikali lilikusanya madafu kama bilioni 15 na ushei. Kwa wachovu maskini wanadhani hii njuluku ni kubwa na lukuki wasijue gharama ya miundombinu usipite. Hebu fikiria mfano kujenga barabara moja yenye urefu wa kilometa kumi toka njini Bukoba kwenda huko kwa waathirika ni bei gani?”
            Kabla ya kuendelea, Da Sofia Lion aka Kanungaembe anadakia “hapa hujaongelea shule, hospitali, zahanati, na miundombinu mingine. Hapa wajanja hawajapiga chao hasa ikizingatiwa kuwa kaya yetu ina ugonjwa wa kuwa na vitu hewa.”
            Leo inaonekana ni kuchomekea mtindo mmoja. Kwani kabla ya da Sofi kumaliza si Mchunguliaji anamchomekea akisema “sitashangaa kusikia kuna wahanga hewa, na madai hewa bila kusahau, misaada hewa. Mara hii wahanga wamesahau wapigaji waliokuwa wameishafungua akaunti kujipatia njuluku za dezo! Ama kweli kufa kufaana. Lazima na serikali iboreshe miundombiu yake hata kama ilikuwa imeishabomoka hata kabla ya tetemeko kuimalizia au vipi?”
            Kanji anaamua kula mic “Sahili iko penda sana lalamika sana. Sasa dugu yangu tetemeko naangusa jumbani yako veve lau sirkali diyo naangusa? Je kama sirkali haikotangaza tetemeko, hiyo saada veve iko weza pata bila sirkali tangaza na kusimamia ili janja chache isiibe saada?”
            Mpemba aliyekuwa kimya akisikiliza anaamua kula mic “mie ndhani watu wafanye tathmini kwanza. Pia waangalie kipi cha kupata kipaumbele kwanza yakhe. Huwezi jenga nyumba ya Shaame au Makame kabla ya kujenga shule wala hospitali ati. Hivi kama tetemeko likirejea, hawa wanaolalamika watanlalamikia nani kutaka nsaada kama siyo hiyo hiyo sirikali waniyoilaumu sasa? Hapa zahitajika busara na subra vinginevyo twaweza shikana uchawi na hilo siyo jibu ati.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kula mic “mie silaumu wahanga wala lisirikali. Naweza kusema tu kwa ufupi kuwa usawa huu wa kuadimika njuluku, kila mmoja analalamika hata wale waliozoea za kupiga na wavivu. Je kama hawa wanaolalamika hawajakumbwa na janga lolote zaidi ya kukatwa mirija yao, hawa wahanga wa tetemeko usawa huu unategemea wafanye nini? Nadhani lisirikali lingeacha ung’ang’anizi. Kama wahanga wataona kuwa mbavu zao za mbwa kwao ni muhimu kuliko miundombinu, basi ikae nao na kuwaelimisha juu ya nini kinahitajika kwanza badala ya kuwaacha Solemba wakilalamika. Nadhani hapa hakuna kilichoharibika zaidi ya mawasiliano haba. Kama wakubwa wa lisirikali watakutana na wahanga na kuwapa sababu za kutoa kipaumbele kwa miundombinu wataelewa na kukubali yaishe huku wakijipa matumaini na kungoja zamu yao au vipi?”
            Mgoshi Machungi anarejea na kukatua mic “hapa azima isiikai iseme ukwei vinginevyo wahanga watazani imekula ushwa kama yue bwana mdogo Makondakonda aiyewahifadhi wahaifu akijidai kakataa ushwa bila kueeza namda aivotaka kuhongwa njuuku iii aluhushu shisha.”
            Msomi aliyekuwa akibofya kisimu chake anamchomekea Mgoshi “sasa Mgoshi hili la dogo Makondakonda kuchemsha na kuramba mlungula linaingiaje au umechanganya madawa au vipi?”
            Mgosi anagundua alivyochemsha na kuamua kujitetea “kwei kaka nimechemsha. Unajua wakati mkizoza niikuwa namtumia meseji bi mkubwa Nesaa ujumbe kuwa aniandaie ie mboga ya kishambaa iitwayo kinyeto. Shamahani ndugu zangu kwa kuchemsha. Hizi simu nazo!”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si ikapiga radi! Acha tutoke mkuku tukidhani ni tetemeko jingine!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: