Saturday, 19 November 2016

Magufuli unangoja nini kumtumbua Makonda?

         Mheshimiwa rais John Pombe Magufuli,
                 Najua unajua kuwa hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makond alitoa mpya ya kufungia mwaka. Makonda alikaririwa na vyombo vya habari akidai kuna wafanyabiashara wa shisha (kumradhi sijui maana yake) wapatao 10 waliomwendea na kutaka kumhonga shilingi 5,000,000 kila mwezi kila mmoja akakataa.  Madai haya, licha ya kushangaza, yamezua maswali mengi kuliko majibu. Je ni kweli kuwa Makonda alikataa rushwa hii au inaweza kujenga dhana kuwa alisema haya ili aonekane safi na kupata sifa kirahisi?  Mosi, tokana na uzito wa shutuma hizi, basi wengi wangetaka Makonda awataje hadharani wahusika ili sheria ichukue mkondo wake. Pia ingekuwa vyema Makonda aeleze ni kwanini hakuwawekea mtego wakakamatwa?
Pili, Makonda, awaombe radhi aliowatuhumu bila ushahidi wala sababu za msingi zaidi ya kile kinachoweza kutafsiriwa kama kutaka kujijengea umaarufu kwa kuwachafua wengine. Maana kufanya hivyo kunawaonyesha kama wala rushwa na mawakala wa shisha bila sababu na ushahidi vya kutosha. Nitashangaa kama wahanga hawatamchukulia hatua za kisheria Makonda. Wasipofanya hivyo, watakuwa wanathibitisha ukweli wa madai ya Makonda.
Tatu, je kwanini Makonda, kama hakuwa na maslahi na biashara hiyo aliamua kuwaficha wahusika wakati akijua kuwa ni wajibu wa kila mtanzania kulipoti kosa la jinai anaposhuhudia ima likitendeka au likiwa katika harakati za kutendeka?
Nne, je kama mkuu wa mkoa kama Makonda analalamika lalamika, hao wa chini–ambao wengi wao ni waathirika wa jinai hii–wafanye nini?
Tano, je Makonda huwa anajitahidi kuruhusu kinywa na ubongo viwasiliane kabla ya kunena; au ndiyo hayo hayo ya kujisemea kila kinachotoka ima kujijenga, kujifurahisha na kuifurahisha hadhira yake?
Sita, kama Makonda atashindwa kuwataja wahusika, basi awajibishwe mara moja ima kwa kuwaficha wahalifu au kutaka kuuongopea umma kwa faida binafsi. Hatuwezi kuendelea na kuuzoea mchezo huu ambao madhara yake yanaweza kuwa makubwa huko tuendako. Kwa kauli kama hizi, umma unaweza kuishiwa imani na serikali, jambo ambalo si jema kwa nchi.
Saba, hata hivyo, Makonda ana bahati kuwa aliyemweleza, yaani waziri mkuu Kassim Majaliwa alichukulia tuhuma zake kimzahamzaha kama si kumuonea huruma na kumuepusha na aibu. Vinginevyo, Waziri Mkuu–kama naye angeamua kuwajibika kwa wadhifa wake–bila shaka alipaswa kumtaka awataje wahusika au kutoa kueleza ni kwanini hakuvitaarifu vyombo husika ili viwashughulikie.  Hapa napo Waziri Mkuu alionyesha udhaifu mkubwa kiutendaji.  Nadhani aliyosema Makonda, kama angeyasema mbele yako, ungemtaka awataje pale pale vinginevyo atumbuliwe; vinginevyo angetumbuliwa yeye. Rejea ulivyokataa taarifa, tena kwenye msiba, kuwa meya wa zamani wa jiji la Dar es Salaam, Didas Masaburi alikuwa na mke mmoja wakati alikuwa nao wengi tu.
Nane, je fungate ya Makonda inaanza kuisha kiasi cha kuanza kufichua kilichoko nyuma ya pazia ya Makonda waliyezoea kumuona watanzania? Maana madai ya Makonda; na namna alivyoshughulikia hii rushwa ni ya ajabu na ushahidi kuwa kuna tatizo tena kubwa tu.
Tisa, ikumbukwe. Hii si mara ya kwanza Makonda kulalamika bila kufuata hata utaratibu. Nani amesahau namna alivyomchomea utambi Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam wa zamani marehemu Wilson Kabwe badala ya kufuata utaratibu? Nani amesahau Makonda alivyowahi kuwaweka ndani watumishi wa Manispaa ya Kinondoni?
Kumi, mchezo wa kujisemea na kutoa madai ya ajabu si jambo jipya kwa baadhi ya watendaji wa juu wa serikali ya awamu ya tano. Rejea hapo mnamo mwezi Machi mwaka huu waziri wa Ardhi, William Lukuvi, kama Makonda, alikuja na madai kuwa kuna wafanyabiashara wawili walanguzi wa ardhi walitaka kumhonga shilingi bilioni tano akazikataa bila kuwawekea mtego wakamatwe wala kuwa tayari kuwataja majina.
Hivi kweli Makonda hajui kuwa kumshawishi mtu tena kiongozi wa juu kama yeye kupokea rushwa ni kosa la jinai?  Je hapa Makonda haoni kuwa alitenda kosa la jinai kwa njia ya kutochukua hatua (omission) kama raia na kiongozi? Usomi wake sasa ni wa nini kama hajui vitu rahisi kama hivi? Tokana na ukali na kutenda haki vilivyoonyeshwa na serikali ya awamu ya tano, nakushauari umtumbue Makonda mara moja ili liwe somo kwa wengine wanaodhani vyeo ni sehemu ya kuchezea na kujifanyia mambo watakavyo hata kwa kukiuka wazi sheria. 
Nimalizie kwa kumtaka Makonda auambie umma ukweli na kwanini hakuchukua hatua kama si mnufaika wa jinai aliyoieleza. Hakuna haja ya kuwang’ang’ania viongozi wa aina hii hasa ikizingatiwa kuwa kuna watanzania wengi wenye sifa tosha. Huu hakika ni mtihani kwako hasa ikizingatiwa kuwa ulimtumbua Mkuu wa zamani wa Mkoa wa Shinyanga Anna Kilango Malecela kwa kueleza umma uongo. Itashangaza kama utamvumilia Makonda. Maana, hii itaonyesha kuwa kuna wasioguswa katika serikali ya awamu ya tano jambo ambalo si zuri na linaloweza kuchafua sifa nzuri ya seriakali husika katika kuwatumikia na kuwakomboa watanzania toka kwenye uovu na uoza uliokuwa umeanza kuzoeleka.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: