Sunday, 6 November 2016

Mihadarati: Kwanini Kikwete hamsaidii Magufuli?

            Japo balaa la uuzaji na utumiaji wa madawa ya kulevya nchini linazidi kugeuka janga la taifa, si viongozi wengi wanapenda kuliongelea. Hata hivyo, hivi karibuni, akiongea kwenye wilayani Same, Kilimanjaro alipokuwa akizungumza wakati wa mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika shule ya sekondari ya Mtakatifu St.Joachim, spika mstaafu Anna Makinda aliamua kulitolea uvivu balaa hili. Makinda alikaririwa akisema “matumizi ya dawa za kulevya katika shule za sekondari yamekuwa ya kawaida ingawa madhara yake ni makubwa katika jamii. Madawa hayo yanachangia maadili kumomonyoka kwani kuna baadhi ya vijana wa kiume wanalawitiana wenyewe kwa wenyewe.”   Hapa unaweza kuona kuibuka balaa jingine la ulawiti na umalaya miongoni mwa vijana wanaotegemewa kuwa viongozi na wazazi wa baadaye. Hii maana yake ni kwamba taifa litajikuta likiwa na kizazi kijacho cha hovyo ambapo watoto wengi wanaweza kuzaliwa wakiwa na athari za mihadarati ukiachia mbali kusambaa kwa kasi kwa maambukizi ya Ukimwi na magonjwa mengine yatokanayo na ulawiti na umalaya.
            Makinda alikwenda mbali na kusema “hali kwa sasa si nzuri, yaani matumizi ya dawa hizo yameongezeka, ndiyo maana ninasema kuna haja ya kuongeza nguvu za kupambana na matumizi ya dawa hizo.” Kwa wanaojali mstakabali wa taifa na wanaojua historia ya mapambano dhidi ya balaa hili, watakumbuka namna rais mstaafu Jakaya Kikwete alivyowahi kuiambia dunia kuwa vyombo vyake vya usalama vilikuwa vimempatia orodha ya vigogo wa madawa ya kulevya; lakini–kwa sababu anazojua mwenyewe–wala hakuwahi kuwashughulikia japo mmoja. Sana sana kilichotokea na kupoteza maisha ya mbunge Amina Chifupa aliyekuwa ameapa kuweka mambo hadharani akisema hata kama mhusika angekuwa mumewe ambaye pia ni marehemu. Na wote wawili wamekufa kwenye mazingira ya kutatanisha kiasi cha kuonyesha namna kadhia hivi ilivyo nchini.
            Kwa vile rais John Pombe Magufuli ameonyesha uzalendo wa hali ya juu wa kutaka kukomesha maovu nchini, tunamshauri Kikwete ampe hiyo orodha aliyoshindwa kuifanyia kazi ili Magufuli aifanyie kazi. Ukiachia hili, kama tutakuwa serious, wanaouza na kutumia madawa ya kulevya wanajulikana; hasa ikizingatiwa kuwa utumiaji wa madawa haya unafanyika wazi wazi. Mbali na watumiaji, wauza unga nao ni rahisi kuwabaini. Kamata watu wote waliotajirika ghafla bila kujulikana wanafanya shughuli gani za kuwatajirisha haraka kiasi hiki.
            Katika kupambana na watu wa namna hii, serikali inapaswa kwenda mbali na kuchunguza watuhumiwa wote bila kujali wamejificha nyuma ya shughuli gani. Kwani, uzoefu unaonyesha wahalifu wanajificha nyuma ya vitu kama uongozi wa kiroho, sanaa, hata biashara nyingine. Tuna mifano ambapo baadhi ya wahalifu walijificha nyuma ya vyeo safi kama vya kiroho japo si viongozi wote wa kiroho. Mchungaji Joh Arinze (52) mwenye makazi yake nchini Afrika Kusini alikamatwa akiwa na kilo 174 za madawa haya mwezi Julai mwaka huu nchini Afrika Kusini na kumueleza kama Mhalifu Mtakatifu (holy criminal), kwa mjibu wa gazeti la Pulse (2 July, 2016).
            Mwingine aliyekamatwa akiwa amevaa ngozi ya kondoo ni Mtume wa Kanisa la milele la Maserafi na Makerubi, Michael Raji (60) akiwa na madawa yenye uzito wa kilo 174 kwa mujibu wa gazeti la Vanguard (17 February, 2015).
            Kesi iliyostua ulimwengu ni ile ya mkuu wa majeshi ya majini wa zamani wa Guinea Bissau, Rear Admiral Jose Americo Bubo Na Tchuto (70) aliyekamatwa mwaka  2013 na kuhukumiwa kifungo cha miaka mine nchini Marekani, kwa mjibu wa shirika la habari la Reuters (4 Oktoba, 2016) alipokiri kutaka kuingiza madawa nchini humo mwaka 2014.
            Ukiangalia uzito wa cheo cha mhusika, unapata picha kuwa biashara hii inawahusisha watu wakubwa sana hata usiowadhania. Ndiyo maana tunamtaka rais mstaafu Kikwete atoe hiyo orodha ya watuhumiwa aliokiri bila kulazimishwa kuwa alikuwa amepewa kama hana maslahi binafsi nayo.
            Kiashiria kingine kinachoonyesha kuwa mtandao wa wauza madawa ya kulevya ni mkubwa unaohusisha vigogo wengi nchini ni ile hali iliyofichuliwa na rais Magufuli uwanja wa ndege na bandarini ambako alikuwa scanners hazifanyi kazi. Kwa maana hiyo, wahalifu wamekuwa wakipitisha kago zao bila taabu huku wakiishia kutajirika na kuwakoga wenzao wakati ni uhalifu mtupu. Kuna haja ya kuwa serious kuhusiana na kadhia hii na kuepuka kuangalia sura ya mtu. Kikwete anapaswa aeleze ni kwanini hakushughulikia orodha ya watu aliyopewa na ni akina nani na ana maslahi gani nao. Japo ana kinga, sidhani kama kinga hiyo inahusiana na makosa ya jinai kama haya. Mbali na hili, Tanzania inapaswa kupitisha sheria ya ima kuwanyonga au kuwagunga maisha wote watakaopatikana na hatia ya kuuza au kula unga ili kutoa taarifa kwa wale ambao hawajakamatwa au wanapanga kufanya hivyo.  Maana, kwa hali ilivyo, sawa na ufisadi, ni kama biashara ya mihadarati ilikuwa imehalalishwa kwa mlango wa nyuma hasa baada ya Kikwete kugoma kuwashughulikia wahusika anaowajua kwa majina.
            Tumalizie kwa kumtaka Kikwete ampe hiyo orodha Kikwete. Kama ataendelea kuifanya mali binafsi, basi tunamtaka Magufuli atumie rungu lake la urais kumtaka atoe orodha hiyo. Kwani si mali binafsi.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: