Tuesday, 1 November 2016

Magufuli aache kulalamikia maovu atumbue


            Akihutubia wafanyakazi wa bandari hivi karibuni, rais John Pombe Magufuli alikaririwa akisema “ukiajiliwa bandarini umeukata, unaambiwa hongera na umeukata.” Magufuli alisema hayo akiwa bandarini ikiwa ametembelea sehemu hii kwa mara ya pili na kukuta madudu yale yale  yaliyokuwa yemegunduliwa awali asichukue hatua. Ikumbuke; mara ya kwanza Magufuli alipotembelea bandari alibaini madudu kibao kiasi cha kuwawajibisha baadhi ya wahusika.
            Hata hivyo, wengi walidhani kuwa kuwajibishwa kwa wahusika kungekomesha uhujumu wa taifa ambapo mashine nyingi za kuchunguza mizigo scanners zilikuwa hazifanyi kazi, huku mita za kupima mafuta, flow meters yanayoingia nchini zikiwa hasifanyi kazi wa miaka mitano. Madudu mengine yaliyogunduliwa na waziri wake mkuu kabla ya hapo ni utoroshaji wa makontena wa kutisha ambapo maelfu ya makontena yalikuwa yamepitishwa bandarini bila kulipiwa ushuru.
            Magufuli aliongelea nchi kukaa miaka mitano bila flow meters na namna wahusika walivyomdanganya waziri mkuu. Je hawa hawajulikani? Je Magufuli anangoja nini bila kuwashughulika? Je kulalamika kunaleta suluhu? Kamata wahusika; weka ndani na kamata mali zao na wale wote wanaoshirikiana na katika jinai hii; simple. Na hii ahitaji uwe na CIA, FBI au Scotland Yard. Kama serikali itaandaa utaratibu mzuri wa kulinda, kumotisha na kuzawadia watoa taarifa, wapo watu wengine bandarini ambao wanaweza kutoa taarifa nyeti tokana na vipengele vitatu hapo juu ukiachia mbali wengine kuchukia uhujumu wa taifa kama anavyouchukia Magufuli. Hawa watuhumiwa hawakufanya kazi na makompyuta. Walifanya kazi na watu na watu wanawajua vizuri nani alipata nini na kiko wapi na alitumia mbinu gani kufanikisha hujuma hii. Hapa kinachotakiwa ni utashi wa kisiasa lakini si malalamiko. Kama rais analalamika, watu wa kawaida mitaani wafanye nini?
             Tokana na namna sakata hili linavyoshughukiwa, inaweza hata kujengeka dhana kuwa uhujumu huu wa kutisha ulikuwa mradi wa serikali iliyopita; hasa ikizingatiwa kuwa uamuzi wa kufunga mita za mafuta kwa miaka mitano hauwezi kuwa wa kitengo au mamlaka ya bandari pekee. Rejea madudu yaliyogundulika kuwa watu walikuwa wakiajiri ndugu zao na serikali ikaangalia isichukue hatua. Kutokana na uhujumu huu Magufuli aliwaambia wafanyakazi wa bandari kuwa wahusika wanajulikana.  Kwa wanaojua mamlaka aliyo nayo, wanashangaa anaongoja nini kama kweli anawajua wahusika asiwashughulikie wakati kila kitu kinajulikana ukiachia kuwa na vyombo vya usalama vyenu utaalamu wa kutosha wa kuchunguza kadhia kama hizi au kuna namna anaogopa kuwagusa alioahidi kuwakingia kifua waliosimamia jinai hii?
            Tokana na kuonekana kuwapo usugu na kushindana baina ya serikali na watumishi wahujumu na mafisadi, tungempa Magufuli na serikali yake maangalizo yafuatayo:
            Mosi, pamoja na kuwajua walioko nyuma ya hujuma hii ambayo kama ingetendekea China wahusika wangeishia kitanzini, chunguza wote waliopitia au waliopo kwenye sehemu zinazohusiana na mita za mafuta, makontena na kwingineko kwenye ulaji wa namna hii ili kujua ni hasara kiasi gani wamesababishia taifa.
            Pili wachungeze wahusika hapo juu ili kujua kiwango cha utajiri walio nao au washirika zao na wameupataje.
            Tatu, Magufuli anasema wapigaji dili wanajulikana. Kama ni kweli kwanini hawashughulikii au ni yale yale ya mtangulizi wake aliyewahi kusema kuwa alikuwa na orodha ya wauza unga, wahalifu kila aina lakini mpaka anaondoka hakumkamata wala kumhoji hata mmoja.
            Nne, Magufuli aliongeza kusema kuwa watu wenye bandari kavu walikuwa hawalipi kodi kwa vile walikuwa wakishirikiana na watu wa TRA kujipatia fedha. Anangoja nini kuwakamata hawa wahusika katika kadhia hii na kuhakikisha wanarejesha fedha waliyoibia taifa na faini na faida juu au ni watu wasiogushwa wakati alisema hatakuwa na simile na watu kama hawa wala kuogopa ukubwa wa mtu?
            Tano, Magufuli aliitaja kampuni ya TICTS na namna ilivyoongezewa mkataba kinyume cha sheria. Je ameichukulia hatua gani hiyo kampuni ya TICTS? Anataka ushahidi upi wakati kila kitu anakijua kama jinai ya kuiongozea kampuni ya TICTS mkataba wa miaka mitano kinyume cha sheria? Badala  ya kuisimamisha kampuni husika hadi ichunguzwe na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, Magufuli alijipinga na kuangiza eti warekebishe mkataba. Unarekebisha nini wakati kila kitu ni haramu ab initio kisheria?
            Sita, Magufuli aliwalaumu wasomi wa bandarini kuwa ndicho chanzo cha uzembe, wizi na uovu bandarini. Je kwanini asiwashughulikie hawa wasomi au ameamua kuwaonya au kuwatisha kwa vile hana namna ya kuwashughulikia?
            Saba, bila kubadili mfumo wa sasa na kurejesha maadili kitaifa ambapo kila mtanzania atajaza taarifa za kodi na kueleza mali yoyote itakayotiliwa shaka.  Alisema kuwa wafanyakazi wa kwenye mafuta ni mabilionea. Je kwanini hakuwataja na kuwchukulia hatua wakati akijua kila kitu; kuna nini kinaendelea?

            Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli atumbue badala ya kulalamika au amechoka kutumbua? Turudie swali kuu muhimu. Kama rais mwenye mamlaka kisheria, vyombo vya upelelezi na taarifa tayari analalamika, hawa wananchi wa kawaida wanaoibiwa mali yao watafanya nini?
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili juzi.

No comments: