Saturday, 19 November 2016

Mlevi afuta safari kwenda kutibiwa Ughaibuni


 
            Baada ya rais Joni Kanywaji Makufuli kuonekana kwenye hospitali ya kaya ya Muhimbiza akimjulia hali mshirika wake wa bedroom, Bi mkubwa Jane, mlevi ambaye bi mkubwa wangu alikuwa akitarajiwa kuondoka kayani kwenda kutibiwa ughaibuni nilijihisi kushushuka na kuona aibu. Nilipiga moyo kondo na kujisuta; ndipo nilipoamua kumkabili Bi Mkubwa wangu Mama Domokubwa kumpasha kuwa hatakwenda kutibiwa ughaibuni.  Kama kawaida yake, aliamka na kunikaba shati kuuliza kulikoni naongea kama hamnazo. Alidhani wazo hili lilisababishwa na mma na yale majani ninayovuta. Baada ya kuninusa na kukuta sina harufu ya zali lolote ilibidi aniachie. Alijifunga kibwebwe na kushika kiuno. Aliuliza tena “we baba Shikaadabu, unayosema ni kweli au umeanza kunitania siku hizi?” nilimjibu kwa kumpa gazeti la Sema Nao la siku ile lililobeba picha ya Bi Nkubwa Jane akiwa kwenye lango la kutokea la  wodi ya Sewa al Haji. Stori ni ndefu  na ina mivutano na misutano kibao.
            Kwa ufupi, tokana na somo nililopata tokana na kitendo cha Bi Nkubwa Jane kupiga mbonji kwenye Hospitali uchwara, rasmi na wazi wazi, natangaza rasmi kwa walevi wote. Mshirika wangu wa bedroom hatakwenda ughaibuni kutibiwa wala kuchekiwa afya yake baadaye. Badala yake atakwenda kutibiwa Muhimbiza; na siku zote zijazo, atakuwa akichekiwa afya yake pale. Nadhani hii licha ya kuwa kuunga mkono spirit ya rahis, ni kutaka kuwaaminisha walevi ninaowaongoza kuwa ninasema ninayotenda na kutenda ninayosema kuhusiana na uzalendo na kuacha ulimbukeni na kujitukuza kana kwamba hakuna atakayenyotoka roho. Wangapi tumeshuhudia wakienda kutibiwa ughaibuni na kurejea kwenye jeneza? Hakuna kusiko na kifo.
            Kitendo hiki ninachopanga kufanya kitashangaza wengi wapenzi na wabaya wangu. Ukiachia bi mkubwa kwenda kutibiwa Muhimbiza, kuanzia sasa nitaagiza walevi wote wawe wakubwa au wadogo kuchekiwa afya zao kayani na si ughaibuni. Nadhani hii itawasaidia wanaohujumu huduma za jamii kuacha kufanya hivyo; kwa vile watakuwa wakijiumiza wenyewe baada ya kuziba uchochoro wa kuzihujumu na kukimbilia ughaibuni kuunguza kodi za walevi. Mbali na hilo, nitaamuru walevi wote kuacha kupwakia vitu vya nje; na badala yake nitawaamuru watumie vya kayani ili kukuza uchumi wetu.
            Pili, msishangae kusikia nikitoa amri kuwa hata vitegemezi vya walevi wote visomee kayani badala ya kupelekwa ughaibuni na kurejea na kufanya kazi kayani. Kama kuna wazazi wanaoogopa vigegemezi vyao kusomea kayani, kwanini waviamini kufanya kazi kayani? Nadhani na hii itasaidia kuwapa somo wale wanaohujumu elimu kwa kutegemea kutumia njuluku wanazopiga kupeleka vitegemezi vyao ughaibuni. Mbona biggie wetu wote waliosomea hapa kayani na wameweza kuukata wakati wengi wa waliosomea ughaibuni wengine tunawaona wakisuasua kisiasa?
            Tatu, tokana na mfano wa rahis ambao bila shaka alidesa toka kwa walevi kama sisi ambao hujinywea mataputapu ya hapa kaya badala ya kunywa wine, whisk na vinywaji vya kigeni, nina imani kuwa hata mahoteli yetu yanayoitwa ya kitalii yatajifunza hili toka kwetu. Kwa walevi ulevi ni ulevi. Unywe mimaa ya kigeni au ya kienyeji mwisho wa siku wote mtalewa na kuangusha magari, simple and clear au vipi?
            Nne, lazima tukubaliane hata kama hatutaki. Wakati wa wanene kwenda kuchekiwa mafua ughaibuni lazima ugeuke historia. Kuna mlevi mmoja alituacha hoi; alipodai kuwa kuna wakubwa walifikia makufuru hata ya kupeleka mbwa na paka wao ughaibuni kuchekiwa afya kwa kufuja kodi za walevi waliopigika ile mbaya. Hawa wangekuwa chini ya utawala wangu wangekula shaba kama siyo kutimuliwa kibarua ili wakarejee huko madongo poromoka walikotokea.
            Tano, naona hata wakati wa kupunguza mashangingi ya wanene umefika. Kwani, haiigii akilini kwa kaya ya wachovu kuendelea kununua mishangingi hata ya kupelekea mbwa kliniki na vitegemezi vya wanene shuleni. Tunamkomoa nani zaidi ya sisi wenyewe?
            Naona mhariri anaanza kusonya na kupiga kipenga cha kuniondoa dimbani. Acha niwaageni kwa kuwaomba mzingatie aya hizi nilizotoa mimi mtume wa walevi wa kaya hii. Achene ulimbukeni, ubinafsi na roho mbaya ya kufuja mali na njuluku za walevi kwenda kuchekiwa ughaibuni. 
Chanzo: Nipahe Jumamosi leo.

No comments: