Wednesday, 16 November 2016

Kijiwe champongeza Dk Kanywaji na mkewe         
Taarifa zilizozagaa kama moto wa nyika za kuugua na kulazwa kwa mke wa rahis Joni Kanywaji Makufuli kwenye Hospitali chakavu ya Muhimbii, kama apendavyo kuiita Mgoshi Machungi, zilimekikuna kijiwe. Hivyo, katika kikao cha leo kinawatumia salamu wawili hawa kuwamotisha waendelee na uzalendo wao usio kifani.
            Kapende leo ndiye anayeanzisha mada. Anaamkua na kuronga “jamani mmesoma hii stori iliyofurika kwenye magazeti yote ya wiki hii?” kabla ya kuendelea, Mgoshi Machungi anamchomekea “habai gani wakati magazeti yamejaa habai mbai mbai; hemu fafanua tieewe na kumwaga pwenti Mgoshi.”
            Kapende anajibu “Mgoshi umenionea. Sijamaliza kueleza wewe unanchomekea! Habari nimaanishayo ni ya kuugua ghafla na kulazwa kwa mke wa rahis mama Jane pale kwenye mkangafu wa Muhimbii. Nadhani kama nimekupata hili ndilo jibu unalotaka kusikia toka kwenye kichaka cha habari au vipi?”
            Mipawa anakwanyua mic “kusemaga ukweli, hili nami limenistua licha ya kunifurahisha. Nimefurahi kwa sababu rahis na mkewe wamejitahidi kuonyesha wanavyojali kaya yetu kwa vitendo na si kwa tambo na upuuzi wa majukwaani ambao wanasiasa wengi wanafiki hupenda kutumia. Ni faraja nadhani kwa wachovu wote kuona rahis na bi mkubwa wake wanavyoshirika huduma wanazohimiza wachovu kuwa wanajenga kwa ajili yetu sote.”
            Msomi Mkatatamaa hangoji Mipawa amalize utamu was tori. Anaamua kula mic “hata mimi licha ya kunistua, rahis na bi mkubwa wake wameniacha kinywa wazi hasa kwenye kaya hii ya wabinafsi, waroho, wachoyo, wajivuni na malimbukeni wanaopenda kukimbilia Ulaya kwenda kupima mafua ukiachia mbali wengine kupeleka hata wanyama wao kama paka na mbwa kutibiwa kule kwa kodi ya wachovu wa kaya hii.” Anakohoa kidogo na kuendelea “hakika big ameweka historia ya aina yake ya kubana matumizi na kuwa mzalendo wa maneno na matendo. Lazima kijiwe tutafute namna ya kukutana naye na kumpa ushauri kuhusu kuwapiga marufuku wa chini yake waliozoea kutumbua njuluku zetu kwenda kujiangalia afya zao.”
            Mheshimiwa Bwege naye anaweka guu “nakubaliana na wasemaji mliotangulia. Lazima rahis apige marufuku wakubwa uchwara kwenda ughaibuni kuunguza njuluku zetu. Hata hivyo, kwa kitendo cha mkewe kulazwa kwenye hospitali uchwara kama hii, ni katazo la nguvu kwa wenye akili. Najua; wapo watakaojifanya kutoelewa somo na kutaka waendelee na mazoea yao ya kishenzi na kilafi na kibinafsi. Nadhani hili ni suto kwa wote walioshindwa uzalendo wakaishia kuuhubiri majukwaani wakati wakiupiga mtama kwa vitendo nyuma ya pazia.”
            Mpemba naye anaamua kula mic “yupo jamaa yangu alonitonya kuwa huyu jamaa hata wale aniowaongoza bado hawajamwelewa. Huyu rafiki yangu alonitonya asema alisoma na dokta Kanywaji. Asema kuwa jamaa ni mtu wa vitendo zaidi ya maneno na wala si nnafiki wala mpenda sifa. Hamkuona alivoita daraja la Kigamboni mzee Nchoga badala ya kupendekezewa liitwe jinale? Je walo chiniye wanfahamu haya aniyotenda au wangoja watumbuliwe?”
            “Nyie mnaongelea hili tendo la nkewe kulazwa Muhimbii. Mbona kuna jamaa alinitonya hivi karibuni kuwa hata watoto wake wanasoma hapa kayani na si ughaibuni ukiachia mbali kuwatolea nje jamaa zake wanaotaka kutumia nafasi yake kujitajirisha? Angalia hata bi mkubwa aliyelazwa Muhimbii. Hana NGO kama wezi waliopita walivyozoea kutumia afisi ya rahis kujiingizia utajiri wa haraka. Huyu jamaa, kama wabongo watamwelewa, watanufaika,” anazoza mzee Maneno.
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakwanyua mic  “nakuunga mkono kaka Maneno. Huyu dada yetu si mpenda utajiri kama wenzake waliomtangulia. Nawajua wakina mama. Angeweza kumlazimisha mumewe aunde NGO; hata kwenda kutibiwa nje ikizingatiwa kuwa kisheria ana haki ya kufanya hivyo. Nadhani dada yangu anaelewa anachofanya mumewe na kukiunga mkono kwa moyo wote na kwa vitendo kama alivyoonyesha kwa kukubali kulazwa Muhimbi. Si mchezo; ni somo la kutosha kwa wenye akili kusema ule ukweli.”
            Kanji hangoji Sofia amalize. Anamchomekea “Mimi iko sangaa san asana. Iko ona vatu kuba mingi nakwenda Bombei. Hii mama Kufuli natoa somo kuba sana kama ile iko chini ya zee najua nini anawofanya witu yake. Hii mana iko nakuna mimi kweli kweli; na nahesimu na kupenda yeye sana. Kesho takwenda jamatini na kuambia venzangu tuombee yeye afya jema sana.”
            Mchunguliaji ambaye huwa hana tabia ya kuchangia anakula mic “Kanji umenikumbusha. Sasa utasikia matapeli wa majoho wa ndani na nje ya kaya wakiandaa mikesha ya kumuombea wakati ukweli watataka kumtumia kujipatia ujiko na kujenga ukaribu naye ili wafanikishe utapeli wao. Mimi nawapongeza madaktari wa Muhimbii ambao hawakumwangusha kiongozi wetu. Pia nitumie fursa hii kutaka kijiwe kipange mkutano na dk Kanywaji ili kumtaka apige marufuku utumiaji wa mashangingi kayani. ”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si ukapita msafara wa magari wa Mama Kanywaji akitokea hospitali. Acha tuukimbize lau tumpe mkono wa pole. Kama si mataa kutukatili, huenda tungempa salamu zetu kwenda kwa mumewe kuhusu kupiga marufuku kwa malimbukeni kwenda kutibiwa ughaibuni utadhani walizaliwa na kulelewa kule wakati wengi wao walibebwa kwenye ngozi na mbuzi na kunywa kukuzwa na maji ya madimbwi waliyozoea kushea na ngiri na nguruwe huko madongo poromoka walikozaliwa.
Chanzo:  Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: