Saturday, 7 January 2017

Barua ya Faru Toto kwa faru John (Baba)

       

Baba Faru John,
            Naandika waraka huu ili ukufikie huko kuzimu japo ambao bado wanaamini kuwa uko hai. Wanasema eti ulibadilishwa jina na kuitwa Ole Sokoine. Vyovyote iwavyo, nitakuhabarisha. Hii ni kutokana na kutaka kukujulisha kinachoendelea baada ya kifo chako chenye kuzua kila aina ya utata kwa wanyama na wanadamu. Pamoja na kwamba hauko nasi kimwili, wanao tunaamini uko nasi kiroho. Pia, nichukua fursa hii kukufahamisha kuwa kwa sasa wakubwa wa taifa letu wameamua kulinda legacy yako kwa kuwawajibisha wote walioshiriki mauaji yako ya kibinadamu kwa namna moja au nyingine. Ninapoandika, wazito wapo wanahangaishana huku watu wazima wakitoa maelezo ya kitoto kiasi cha kumfanya bosi agomee utetezi wao.
            Vyombo vyote makini vya habari, si vya uchafu aka udaku, vimesheheni habari zako.  Picha yako sasa inajulikana sawa na ya wajina wako John mwenye jina jingine lenye maana ya maji yanayochanganya wanayokunywa binadamu. Kwa vile John si jina la kutania, tunapanga kubadili majina yetu watoto wako wote tuitwe Toto John na Toto Joanna, Janet au Mary kama shukrani ya wakubwa hawa wanaotupigania.
            Baba, baada ya kifo chako nasi tumekuwa maarufu ghafla bin vu. Kama mambo hayatabadilika, baba umejitoa kafala kwa ajili yetu. Maana, hakuna mkubwa anayelala bila kwenda kwa bosi kutoa maelezo ya kufa kwako hata kama hayaingii akilini. Ilmradi kila mkubwa na vimbwanga na vibwengo vyake.
            Waziri mkubwa, kwa alivyokupenda na kukuthamini, ameitisha uchunguzi ambapo vinasaba vyako (DNA) vitachukuliwa toka kwetu watoto wako, pembe zako (kama kweli zile alizopelekewa kwake ni zako), kaburi lako (kama kweli lipo na ni lako) na popote vinapoweza kupatikana ili kuhakikisha kweli ni wewe uliyekufa bila kuugua tena ghafla.
            Baba, tumefarijika kusikia bosi akiuliza maswali ambayo nasi tuliuliza ila kwa vile tu wanyama, hakuna aliyetuelewa. Kati ya mengi, bosi aliuliza maswali, tena yanaoingia akili, mia kidogo. Baadhi yake ni:
            Mosi, ilikuwaje ulikufa bila kuugua?  Sisi wanao tunajua ulivyokuwa mzima wa afya huku ukifyatua wadogo zetu wengine ili kuondoa hali ya sisi kuwa viumbe walioko kwenye hatari ya kutoweka.
            Pili, je daktari wetu alikuwa wapi; ni nani na ana taarifa gani kuhusiana na mauti yako?  Tunamshauri mkubwa na mkubwa wake wajina wako wahakikishe daktari huyu anatoa maelezo yanayoingia akilini.
            Tatu, je baba zima na jabari kama wewe ulitokaje Ngorongoro crater hadi huko Grumetti, sijui guruneti, ulikofia ghafla au ulikanyaga guruneti likakulipua? Je hicho kitufe walichokuwa wamekufunga kikiwasiliana na setalite kilikuwa kinafanya kazi gani na kina taarifa zipi? Nne, je kuna mchezo mchafu hasa baada ya pembe zetu kupata soko kuliko hata dhahabu huko kwenye bara la washirikina wanaopenda kututumia kwa upuuzi wao?  Tano, je ukweli ni upi na nani anao na kama hajautoa anadhani atafanikiwa kuua au utamuua yeye?
            Baba Faru John, watoto wako tunakukumbuka kila siku kiasi cha kushindwa hata kula majani na kuchezacheza kama tulivyozoea. Tunahofia kuwa nasi tukikua tunaweza kupotea kama ulivyopotezwa, kuswagwa au kupakiwa kwenye malori na kwenda kuuawa kwingine ili ushahidi upotee. Kama si bosi kusukuti, ulikuwa ndiyo hivyo, umemalizwa wakati sisi tukingoja kwenye mstari.
            Baba yetu faru John, kwa heshima yako na upendo wetu kwako, sisi watoto wako tunapanga kuandamana hadi ikulu kuomba kuonana na rais ili tuulize maswali yetu kuhusiana na kifo chako na mustakabali wetu kama wanyama wa nchi hii. Umefika wanyama kutendewa haki. Pia tukifika kule, tutamuomba rais awape kipaumbele wenye ulemavu wa ngozi ambao, sawa nasi, viungo vyao vinatumika kishirikina kiasi cha kuhatarisha mustakabali wetu kama viumbe wa muumba.
            Baba, sijui kwanini wanadamu wanakuwa hamnazo kiasi hiki. Wanatuua wasijue wanaua kesho yao na vizazi vijavyo. Au wao hawajali juu ya vizazi vyao kama sisi wanyama ambao kwa sasa tunaonekana kuwa na akili kuliko baadhi yao. Tutashindwaje wakati sisi hutuuani sisi kwa sisi wala kuwaua wao ili kuuza viungo vyao kama wanavyotufanyia?
Wako faru Toto.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: