Saturday, 21 January 2017

Utabiri wa mwaka huu wa mlevi


            Baada ya matapeli wengi kurithi na kuibuka na utapeli uitwao utabiri, nami kwa nguvu ya kanywaji naamua kutabiri hasa ikizingatiwa kuwa hakuna chuo hata kimoja kinachofundisha kitu hii. Atakayedhani navamia ulaji wa wajanja anionyeshe cheti cha utabiri au uchungaji hata ushehe. Siku hizi kila kitu ni akili kichwani. Hamjaona mitume, wachunaji sorry wachungaji, hata manabii wa kujipachika wakiukata wakati nyinyi mnakatwa na ukata siyo? Acha nijitabirie huenda nikapata ujiko na kuwa karibu na wenye ulaji.  Hivyo ufuatao ni utabiri wa mwaka 2017 wa  Dokta, Profesa, Shehe, Alhaj, Mchunaji, Mchungaji, Maulana, Ustaadhi, Gwiji, Nguli Mlevi mwana wa Mchomajani, expert in astrology and astronomy, vitimbwology and blahblahlology.
            Kwanza, natabiri kuwa watabiri wengi wanaowatabiria wenzao mabaya watakufa au kuumbuka hasa ikizingatiwa kuwa waliyotabiri hatatokea au kutokea tofauti.
            Pili, natabiri kuwa rais John Kanywaji Makufuli hatapewa nishani yoyote kutoka nje zaidi ya walevi waliomchagua. Natabiri kuwa rais Kanywaji atazidi kupeta huku wengi wakizidi kumpa tafu kutokana na kuwaridhisha huku wachache wakimchukia kutokana kuwavurugia ulaji. Hata wale wanaojiona kuwa karibu naye, wengine watajikuta wakitupwa nje kama si kutumbuliwa baada ya madhambi yao kuanikwa hadharani.
            Tatu natabiri kuwa maisha yatazidi kuwa magumu huku mianya ya rushwa ikizidi kupunguzwa katika kujenga mazingira ya uimarikaji wa uchumi unaotegemea kazi na si ubabaishaji; pia walevi wengi wataokoka si kwa sababu ya kumcha God bali kukwepa makali ya ukapa na ukata. Pia vitendo vya ufuska, kujiuza na dhuluma vitaongezeka usawa huu na kusababisha mifarakano na kesi nyingi miongoni mwa walevi huku mji mmoja wa katikati ya kaya ukizidi kuchangamka na kupata wakazi wengi wenye njuluku.
            Nne, natabiri kuwa ubabe na undavaundava kwenye siasa za Bongo utaongezeka huku walioko nyuma yake wakizidi kufukuzana, kutumbuana na kupingana kama ilivyotokea kwenye kadhia ya umeme.
            Tano, natabiri kuwa wasanii wengi watazidi kuigiza kila upuuzi kutoka ng’ambo kama vile kutoga masikio, kujichota tattoos, kufuga vijibwa aina ya Chihuahua na upuuzi mwingine huku wengine wakizidi kudorora kisanaa. Wapo watakaopukutishwa na mibwimbwi na misifa huku wengeni wakipotea toka kwenye tasnia.
            Sita, natabiri kuwa litatokea tetemeko kayani litakalosababisha kiama cha mafisadi hata wale ambao hukuwategemea kutokana na uzito wa nyadhifa walizowahi kushika kayani.
            Saba, natabiri kuwa upingaji utazidi kutifuana na kuimarika taratibu ingawa hautaweza kuungana tokana na kushukiana, kuchuuzana hata kutaka kutumiana kama ambavyo imekuwa siku zote. Wale wanaosema baadhi ya vigogo wataramba matapishi yao ni waongo. Wanene waliotabiriwa kurejea wataendelea kung’ang’ania huko kama luba. Cha mno, upingaji utazidi kujipinga kwa kutetea yale uliyokuwa ukipinga hasa kuhusiana na ufisadi.
            Nane, natabiri  kuwa matapeli wa kidini wa ndani na nje ya kaya watazidi kuongezeka na wengi kuumbuka kama vile kukumbwa na kashfa za ulevi, ngono, kuigiza ulemavu na kujifanya wameomba na kupona; hata idadi ya wanaopwakia usanii wao itazidi kupungua huku serikali ikizidi kuwachunguza wengi kwa kujihusisha na biashara haramu ya bwimbwi na wizi wa sadaka. Wapo watakapofikia makufuru ya ajabu kama vile kutoza ada kwa sala ukiachia mbali wengine kujifanya wameparalyse na kujiombea na kupona wakati ni usanii mtupu.
            Tisa, natabiri kuwa biashara ya mihadarati itaongezeka huku wauzaji wakibadili mbinu. Hata hivyo, baadhi yao ima wataacha au kukamatwa ndani ya mwaka huu. Wapo wauza bwimbwi watakaokufa tokana na laana ya biashara hii haramu. Kuna wakubwa wengi wanaotumiwa na wauza bwimbwi wataumbuka na kutumbuliwa.
            Kumi, natabiri kuwa kiongozi mmoja king’ang’anizi na kikongwe kuliko wote atagombea tena urais na kuzidi kusababisha sintofahamu nchini humo au kufa kabla ya kugombea. Na hapa kaya mnene mmoja atatishia magazeti kutokana na kumnyima raha huku mengine yakifilisiwa kinamna kwa kunyimwa matangazo ukiachia mbali kuminywa kwa njuluku kiasi cha wachovu kuacha kununua magazeti. Hapa ndipo waandikaji wengi watajikuta wakitolewa sadaka na wamilkiji wa vyombo husika.
            Kumi na moja, natabiri kiongozi mmoja mkongwe wa upinzani kwenye kaya ya jirani atashinda urahis na kumuondoa mwana wa mfalme aliyeko kwenye ulaji.
 Kumi na mbili na mwisho,  najitabiria kuwa ujiko wangu utaongezeka kutokana na kutabiri mambo yanayotokea na si kujigonga kisiasa wala kurithi toka kwa dingi yangu kama wale wanaosifika kwa urongo na upuuzi.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: