Thursday, 26 January 2017

Kikwete hakustahili kuwa Mkuu wa UDSM

             Baada ya rais John Magufuli kumteua rais mstaafu Luteni Kanali mstaafu, Jakaya Kikwete kuwa mkuu wa chuo kikuu cha Dar Es Salaam (UDSM) wanaojua namna Kikwete alivyokacha nafasi hiyo walishangaa sana. Inakuwaje mtu aliyekacha nafasi husika akiwa na madaraka afae kwenye nafasi aliyoikacha mwenyewe? Je nini maana ya kustaafu? Je hakuna watu wengine, tena wenye sifa, ambao wangeweza kuteuliwa? Mie naona kuteuliwa kwa Kikwete ni tatizo. Kwanza, kama nilivyosema hapo juu, hana sifa za kuwa mkuu wa chuo kikuu nje ya urais. Uzoefu wake wa kuacha nafasi hiyo unaweza kusema mengi. Pia anapopewa kazi kama hiyo, ina maana anapokea mishahara miwili yaani marupurupu na stahiki za rais mstaafu na mkuu wa chuo. Ukitaka kuona tunachomaanisha kuhusu kutofaa kwa Kikwete kuwa mkuu wa chuo, juzi alifanya kama alivyofanyiwa kwa kumpa mkataba wa mwaka mmoja rafiki yake Profesa Lwekaza Mkandala alipotimiza umri wa kustaafu. Je hapakuwapo na maprofesa wengine wenye siha ya kuweza kushikilia wadhifa huo au ni yale yale ya kutumia ofisi na nafasi za umma kufadhiliana? Kwani lazima Kikwete au Mkandala? Hii si haki. Inakuwa kituko kwenye taasisi ya kisomi kama UDSM kuendeshwa kisiasa kiasi cha watu binafsi kuigeuza kama taasisi isiyo ya kisomi. Nadhani, kwa aina ya taasisi, haikupaswa ku-recycle watu au kuwa na watu ambao ni recycled. Taasisi inayozalishwa wasomi kila siku haiwezi kukosa mtu wa kufaa kuwa mkuu wake hadi aliyestaafu awe-recycled. Kwa maana hiyo, rais afikirie kufuta huu mkataba wa nyongeza aliopewa Mkandala na rafiki yake Kikwete. Pia kwanini Magufuli asiige mfano wa Mwl Julius Nyerere wa kuwa mkuu wa chuo kikuu hiki muhimu na cha kwanza yeye mwenyewe badala ya kuendeleza utamaduni ulioanzishwa na watu waliokuwa wakiogopa kwenda kule kukalishwa kitimoto kushiriki midaharo? Magufuli ni msomi.
            Tokana na mfumo wa chama kimoja, tulizoea, na kusimikwa ufisadi na ubinafsi baadaye, kupeana kazi kwa kujuana na kulindana. Hivi karibuni rais John Magufuli alisikika akisema hakuna mtu atakeruhusiwa kuwa na vyeo viwili kwa wakati mmoja. Hii maana yake ni kwamba mtu anaposhikilia nafasi mbili, licha ya kupokea mishahara zaidi ya mmoja, anawanyima wengine fursa ya kuajiriwa. Hili moja, je hali inakuwaje anapoteuliwa mtu aliyekwisha kufanya kazi na kustaafu huku wakiachwa wale ambao hawajawahi hata kupata fursa hii?
            Tangu aingie madarakani, rais Magufuli amefanya mambo mengi mapya na makubwa. Hata hivyo, inaonekana anaanza kukwamishwa na mazoea kiasi cha kuanza kujipinga kuhusiana na haki za ajira kwa watanzania. Kwani akiwa rais ameishawateua watu waliostaafu tena wasiofaa kuwa wenyeviti au wajumbe wa bodi. Chukulia Anna Abdallah  kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya Makumbusho. Huyu alishashika kila wadhifa kuanzia ubunge hadi uwaziri. Kama ni kuchuma ameishachuma vya kutosha. Mwingine ni spika wa bunge mstaafu, Anna Makinda ambaye aliteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya NHIF. Huyu kama si tamaa, ameishachuma vya kutosha. Kama Abdallah alishakuwa mbunge, waziri hadi spika. Hata umri wake si wa kuutumikia umma bali kulea wajukuu. Mwingine ni  Augustine Mrema aliyeteuliwa kuwa mwenyekiti wa Parole wakati ima wahusika walishastaafu au wana nafasi nyingine kama Mrema kama siyo kuendeleza ukale na ubinafsi wa chama  kimoja ni nini? Je uenyekiti na ujumbe wa bodi upo kuhifadhiana kwa wanasiasa au kwa minajili ya utendaji bora kwenye mashirika.
            Ukiachia mbali bodi za mashirika, uchochoro mwingine ambao umekuwa ukitumiwa na serikali kufadhiliana ni ofisi za balozi zetu nje.   Unashangaa kuona mtu anastaafu mfano jeshini hapohapo hata kabla ya kufika nyumbani anateuliwa balozi. Unajiuliza; kwani hizi nafasi ni za rais binafsi kiasi cha kuacha vijana wengi waliojaa wizarani na mitaani wenye ujuzi wa kuweza kuwakilisha nchi?  Tunao mabalozi wangapi wazee waliokwishastaafu jeshini au kwingineko lakini wakateuliwa kwenye nafasi kama hiyo inayohitaji watu wenye kuchemka na wenye nguvu? Mfano mwanajeshi na ubalozi wapi na wapi kama tutatukuwa wakweli? Wengine wanastaafu na kuteuliwa wakuu wa mikoa au wilaya. Je hii si kuwanyima kazi watanzania wengine wenye haki na uwezo wa kushika nyadhifa hizi? Kwanini tusibadili sheria na kuweka vipengele vilivyo wazi kuwa watu ambao wameishafanya kazi na kustaafu wasiruhusiwe kuteuliwa kwenye nafasi zozote? Tokana na serikali ya hovyo na goigoi iliyopita, tumejaza watu wa hovyo kwenye ofisi zetu za ubalozi nje. Walioteuliwa kutokana na kujuana.  Hawa nao wanapaswa kutumbuliwa tu ili kuepusha hasara kwa taifa. Kwani, walipewa mamlaka wasiyo na sifa wala uwezo nayo.
            Tumalizie kwa kuwataka rais na wananchi kuhakikisha unapangwa utaratibu wa kuepuka ajira na uteuzi ambao si chochote bali recycled, sina neno la Kiswahili.
Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: