Tuesday, 10 January 2017

Nchemba, wako wapi wauza unga!

            Kuna mambo rais John Magufuli amefanikiwa kwa asilimia kubwa tangu aingie madarakani tena kwa muda mfupi na kasi ya ajabu. Magufuli anasifika kwa kutofumbia macho uzembe, matumizi mabaya na kwa kiasi fulani ufisadi. Hata hivyo, pia kuna mambo ambayo rais Magufuli anaonekana kushindwa kabisa kiasi cha kuonyesha ima kuishiwa pumzi au kuyakwepa akilenga kufunika kombe ili mwanaharamu apite.
            Leo tutaongelea moja ya mambo yanayoonyesha kumshinda rais Magufuli pamoja na wasaidizi wake ambalo ni kadhia nzima ya biashara ya mihadarati. Si kupiga chuku wala uzushi kukiri kuwa kwa sasa kuna kila dalili kuwa serikali ya awamu ya tano imeshindwa wazi mapambano dhidi ya biashara hii hatari na haramu.
            Maneno ya hivi karibuni ya msaidizi mkuu kuhusiana na mapambano dhidi ya mihadarati, Waziri Mambo ya Ndani ya Nchi, Lameck Mwigulu Nchemba yanaonyesha na kuunga mkono dhana hii kuwa serikali imeshindwa mapambano dhidi ya biashara ya mihadarati. Nchemba alikaririwa na vyombo vya habari hivi karibuni akisema “inasikitisha na haivumiliki kuona nguvu kazi ya Taifa inapotea huku wauzaji wakinufaika kwa pesa haramu, ifahamike wazi vita ya Serikali dhidi ya wauzaji ni kubwa kuliko wanavyofikiria.” Ukiyafanyia uchambuzi maneno ya Nchemba, licha ya kuwa maneno ya kukata tamaa ni maneno ya mtu aliyeshindwa kabisa kiasi cha kuishia kulalamika kana kwamba hana uwezo wala nyenzo za kupambana na kadhia na jinai husika. Sasa kama Waziri mwenye kila aina ya zana za kupambana na uovu analalamika, hawa wa chini hasa wahanga nao wasemeje? Kwa vile Waziri ni msaidizi mkuu wa rais, maneno yake ni ya bosi wake pia. Je kweli tumeshindwa kwa sababu hatuna uwezo au ni kwa sababu ya kuendekeza ufisadi na woga wa kawaida tu? Niliwahi kuonya kuwa tusipoangalia, biashara ya mihadarati itageuka balaa kubwa kuliko hata ukimwi kutokana na wanaopaswa kupambana nayo ima kuogopa au kuwa wanufaika wa jinai yenyewe. Nilizidi kupata wasi wasi pale rais Magufuli aliposema kuwa hana mpango wa kufukua makaburi kwa vile anaweza kushindwa kuyafukia asijue kufanya hivyo ni kuonyesha udhaifu wa serikali yake dhidi ya majanga mengine kama mihadarati. Nilihoji; kama rais anashindwa makaburi, je angeweza mihadarati? Maneno ya Waziri wake sasa yamethibitisha hofu yangu.
            Tukiachia mbali woga na ukosefu wa ithibati ya kupambana na mihadarati kama janga la kitaifa na kimataifa,  tuangalia upande wa pili ambao ni urahisi wa kupambana na kadhia husika. Nasema wazi kukwa ni rahisi ya kukomesha dawa za kulevya kama serikali itafanya yafuatayo:
            Mosi, ihakikishe wale wote wanaoshukiwa wanachunguzwa bila kujali hadhi zao kisiasa na kimaisha hata wawe ni marais.
            Pili, ifahamike kuwa ni rahisi kuwajua wauza mihadarati au wanufaika na makuwadi wao. Kwanza, wana mali nyingi zisizoweza kutolewa maelezo sahihi ya upatikanaji wake. Pili, wengine wamejificha nyuma ya shuguli nyingi halali kama vile dini, biashara na hata siasa.
            Tatu, ukiachia mbali dalili zitokanazo na wauzaji, makuwadi au washitili wao wa kisiasa, kuna namna nyingine rahisi ya kuwabaini wauza unga. Ukitaka kuwabaini basi kamata watumiaji ilil wakuonyeshe wapi wanapata unga na nani anawauzia. Changamoto ambayo akina Nchemba wanapaswa kushughulikia ni kwanini watumiaji wajulikane, wauzaji wasijulikane? Ukitaka kujua ni wapi kuna paka wengi, angalia palipo na panya. Haiwezekani tushindwe kuwabaini na kuwashughulikia wauza mihadarati wakati tunao vijana wengi watumiaji waliotamalaki mitaani kwetu. Tunamdanganya nani na kwanini wakati kila kitu kiko wazi na rahisi? Je hapa tatizo ni kuwabaini wauza unga au ukosefu wa ujasiri na utayari kuwakabili? Tukubaliane kuwa kinachogomba si kuwabaini wauza unga bali utayari wa kufanya hivyo.  Wapo na wanawahonga viongozi. Rejea kashfa ya shisha.  Yameishia wapi baada ya kuwekana sawa? Mnamdanganya nani? heri mhalalishe hiyo haramu ili kijulikane kuliko kula huku na kule.
            Turejee kwa Nchemba, kulalamika hakutoshi. Kamateni wala na wabwia unga mtawapata wauzaji kirahisi ukiachia mbali kuwa kuna vigezo vingi vya kuwabaini ingawa wanajulikana. Pia ifahamike kuwa suala la mihadarati si suala la Wizara ya Mambo ya Ndani pekee. Linapaswa kuhusisha wizara karibia zote muhimu na za mbele zikiwa ni zile za Afya, Fedha, Katiba na Sheria, Vijana na Usalama. Wizara ya Afya inaweza kusaidia kubaini watumiaji ambao wanaweza kuielekeza Wizara ya Mambo ya Ndani kuwakamata. Wizara ya Fedha kupitia mabanki inaweza kutoa taarifa za watu wanaowekeza fedha nyingi bila maelezo au wenye kutia shaka. Wizara ya Vijana inaweza kuainisha ni vijana wangapi wameathirika, kiasi gani na walipo ili kubaini maeneo sugu. Na wizara ya Usalama inaweza kutumia taarifa zilizokusanywa kwenye asasi na wizara nyingine na kuzifanyia uchunguzi kubaini chanzo na ukubwa wa tatizo. Wizara ya Katiba na Sheria ina wajibu wa kuhakikisha majaji na mahakimu wanaopatikana na makosa ya kuhongwa na wafanyabiashara ya mihadarati wanafukuzwa kazi mara moja na kufikishwa mahakamani.
Kwa ufupi, kupambana mihadarati ni rahisi. Hakuna sababu ya Waziri kulalamika. Kama ameshindwa kazi aachie ngazi wenye uwezo wachape kazi.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.

No comments: