Wednesday, 25 January 2017

Mpayukaji arejea toka Gambia kumtimua Jammeh

          Baada ya kuupa tafu upingaji nchini Gambia na kumtupa nje imla wa huko wa siku nyingi Yaya Jammeh akagoma kukitoa, ilibidi nirejee tena kumtimua tena kwa aibu. Hii ni baada ya jamaa kujifanya hamnazo akajipiga ntama na kutaka aendelee kukinajisi ki nchi hiki kiduchu kule Afrika ya Magharibi. Baada ya kuupa mbinu upingaji kuungana na kumteua Adam Baro kuwa mgombea wake na kushinda, nimeamua kuupa tafu upingaji wote barani Afrika ili kuondokana na utawala msonge na wa kikale ili kuleta maendeleo.
            Nilipiga kampeni kwa marafiki zangu wanene kama vile Mahamadu Bahari na Alpha Shamba Konde na bi Nkubwa Helena Salifu kunipa tafu ya ndata kumchakaza na kumnyaka jamaa na kumtupa lupango. Nilipofika kule, nilikwenda kuonana na Yaya na kumkumbusha namna tulivyomfanyia kitu mbaya Idi Amini yule dada wa Uganda tuliyempa kichapo hadi akatimkia kwa Mwamari Kashafi zama zile akiwika asijue naye ataishia pakanga.
            Baada kumbana habithi huyu ambaye alikuwa amekamia kutoacha madaraka kwa kumtishia kichapo toka kwa ndata wa washirika zangu, ilifikiwa uamuzi kuwa aamue kusuka au kunyolewa. Kwa kujua kichapo kilivyo kikali hadi kuweza kusababisha maafa hata kifo, habithi huyu aliamua kumwaga manyanga na kuachia ngazi huku akielekea ukimbizini akingojea kujua kama ICC itampa mwaliko wa kwenda kulala The Hague akishirika karamu na akina Badboy Gbagbo na Chazi Teila.
            Pamoja na kusherehekea ushindi wa demokrasia nilivyochangia kule Gambia, napenda kutoa taarifa kuwa ving’ang’anizi wa madaraka kuanzia Kusini hadi Kaskazini na Mashariki hadi Maghabiri wakae mkao wa kuliwa hasa ikizingatiwa kuwa wachovu sasa wameamua kuwafanyia kweli wezi na maimla wao. Nimegundua siri ndogo ya kuwabwaga madikteta. Ni kwa wapiga kura kujiandikisha kwa wingi huku wapingaji nao wakiungana kimakwelini na kuondoa upuuzi kirahisi tena mara moja. Kuna jamaa yangu aliniacha hoi. Alidai kuwa maimla wengi barani Afrika sasa wanamlaani Jammeh kwa kundaa uchaguzi bila kuwa na namna ya kuchakachua na kuibuka mshindi tenakwa kishindo kama siyo kitsunami. Waduwanzi hawa wanashangaa namna mtu tena mwenye uchu wa madaraka kuweza kuandaa uchaguzi halafu akashindwa kuuchakachua; wasijue kuwa za mwizi ni arobaini na zikifika huwa hakuna ujanja.  Hii ndiyo maana nawaambia wazi wazi kuwa siku zao zikifika iwe ni kwa heri au shari watafurushwa au kunyotolewa roho kama rafiki na baba yao Kashafi alivyofanyiwa.
            Cha mno hasa hapa Bongolalaland ni kwa wapingaji kujipanga upya wakijenga hoja na kuungana na si kuunda ushirikiano. Mtazidi kugalagazwa huku mkilalalamika na kuzua. Kwa mfano, lazima mrejee kwenye hoja yenu ya kupambana na ufisadi badala ya kubabishwa na mafisadi wachache kuwa watawawezesha kuchukua dola.
            Katika kusuluhusiha mgogoro wa Gambia niligundua kitu kimoja cha kustua. Licha ya kuwa kihiyo asiye na elimu yeyote, kumbe Yaya Jamaa alikuwa kichaa hakuna mfano. Aliwakua akitembea na mifimbo, mishanga na kitabu cha dini moja ambayo sitaki kuitaja japo inajulikana akijipachika kila sifa na vyeo wakati sifa kuu aliyo kuwa nayo ni mwehu. Alijiita Alhaj, Daktari kama Njaa Kaya huku akikwepa kutumia cheo chake cha kijeshi cha Luteni Kanali, Profesa, kama wale waganga wa kienyeji huku akijifanya amegundua tiba ya miwaya asijue yeye mwenyewe hana tofauti na miwaya alivyowatesa Wagambia. Mara nyingi vihiyo kama hawa hupenda vyeo vikubwa vya kisomi wakati walikimbia umande. Nani mtu mwenye akili timamu anaweza kujipachika sifa za kisomi kama daktari wakati hajausomea huo udaktari?
            Wapo wengine wanaodai kuwa huenda hakuwa mtoto riziki hasa ikizingatiwa alivyopenda kuvaa magauni na kuwa na mwili mkubwa kuliko wake. Wengine wanadai alikuwa akificha mavazi ya kuzuia shaba. Kwa vile alikuwa akijua angeweza kurambwa shaba wakati wowote tokana na uduwanzi wake. Alijiita shehe na kutangaza Gambia kuwa taifa la kiislamu huku mkewa akishindwa hata kuvaa ushungi wa kawaida! Kuna jamaa alinitonya kuwa jamaa huyu–kama rafiki yake Kashafi ambaye wanae walikuwa wakikata kalaji kama hawan akili nzuri–anakunywa kama hana akili nzuri. Kuna ukweli kwenye madai haya hasa ikizingatiwa kuwa jamaa alikuwa anajifanya kuijua dini kuliko hata watasha wenyewe wenye dini ukiachia mbali baadhi ya kaya zao kutawaliwa kidini. Utawala wa kidini tena dini yenyewe nyemelezi na mswahili wapi na wapi? Angekuwa msomi angeanzisha utawala dini za kiasili za Kiafrika badala ya kupwakia vya wengine asijue vingemuumbua na kumuonyesha kama mnafiki na limbukeni wa kutupwa. Mbona sasa hakukimbilia kwenye kaya za kidini kama kweli alikuwa ni mtawala wa kidini? Usanii mwingine bwana ni wa kishenzi hakuna mfano.  Acha waitwe watumwa tokana na kupwakia vya watu huku wakivitukana na kuvidhalilisha vyao. Hamuwezi kuendelea kwa kuiga vya wengine. Angalia machainizi na Wajep wanavyozidi kupeta tokana na kuheshimu asili zao.
            Kwa vile ndiyo nimeshuka toka kwenye pipa, acha nikitoe niende zangu kujiweni kupata update ya kilichoendelea wakati nilipokuwa nje ya Kaya. Nasikia wapo watu tena wazima wanashindania kutangaza baa la njaa wasijue wao ndiyo baa lenyewe!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
 

No comments: