Tuesday, 10 January 2017

Kijiwe na Mikakati ya Mwaka Mpya

            Baaada ya kufanikiwa kumaliza mwaka 2016, Kijiwe kimejiandaa kuleta mapinduzi kwa kupambana na changamoto mbali mbali kama vile kupambana na ufisadi na ufisi; kuhimiza matumizi bora ya mali za umma;kuwapayukia viongozi wazembe; na kuondoa ubabe wa kisiasa.
            Msomi Mkatatamaa anaingia, kama kawaida yake, ana jarida moja maarufu la kimataifa la Uongozi liitwalo Global Leader. Analiweka mezani baada ya kuamkua huku akijiweka vizuri kwenye benchi tayari kulianzisha. Anakohoa kidogo na kuangalia huku na kule na kusema “herini ya mwaka mpya wapendwani wote. Nashukuru kuwaona wote mkiwa timamu na tayari kuukabili mwaka mpya kwa nguvu na akili mpya ila si kwa ari, kasi na nguvu mpya vilivyoishia kuwa usaliti na uzandiki kwa kaya yetu tukufu.” Anakohoa tena na kuendelea “hebu jamani leteni mipango yenu ya mwaka mpya kama wana kijiwe ili lau tuidurusu na kuitafakari pamoja na kuamua nini tufanye kwenye mwaka huu tuliouanza.”
            Kabla ya kuendelea, Kapende anamchomekea “kwangu mwaka huu ningependa uwe wa kuleta uwajibikaji wa kweli na sawa kwa walevi wote bila kulindana wala kuwekana sawa kama ilivyo sasa ambapo kashfa na makaburi maarufu yanaendelea kupeta huku wakubwa wakituweka sawa kuwa mambo ni sawa wakati si kweli.”
            Kabla ya kuendelea, Mbwamwitu anachomkea “una aya za kuunga mkono madai yako au ni rongorongo na politiki?”
            “Mijitu mingi kwa kushindwa kubadilika, unadai aya kwenye mambo ya siasa au ni usugu wako wa kwenye mihadhara ya vihiyo wasiojua kitu chochote wajifanyao kujua dini za wenzao wakati zao zinawashinda? Omba ushahidi upewe lakini si aya. Hakuna aya hapa na hatuzitaki.” Anajibu  Mipawa akionyesha wazi kuwa na hasira na kutopendezwa na masuala ya dini kwenye siasa.
            Msomi anarejea “sameheaneni ili msamehewe. Si vibaya kuonyesha hisia za mchovu hata kama hazikubaliki. Basi ili kuokoa mjadala, Kapende omba ushahidi na si aya.”
            Kapende anakula mic huku akitabasamu “nilifanya makusudi ili kuzuia wachovu kuleta dini kwenye mjadala huu adhimu ndugu zanguni. Ninchotoka kuongelea hapa ni uwajibikaji wa pamoja tena kwa usawa kwa ajili ya mustakabali wa kaya yetu.”
            Kabla ya kuendelea Mpemba ananchomekea “wamaanishani wakati twaaambwa wote tuwajibike wakati wakubwa wakiwajibika pia? Hebu tupeni maelezo lau tuelewe unichomaanisha shehe Kapende.”
            “Ninapoongelea uwajibikaji namaanisha uwajibika wa kweli. Kwa mfano, hadi sasa hatujui madingi wetu wote watatu wana utajiri kiasi gani, wameupataje, wanautumiaje na wana mpango gani kutumegea nasi ili kutuonyesha mapenzi na uwajibikaji wao.” Kapende anajibu huku akitabasamu.
            Kanji anakula mic “veve Pende iko chokozi sana dugu yangu. Sasa nataka tajiri ya bana kuba na bi kuba uende kuiba tajiri yao? Veve mbona hapa nataja tajiri yako dugu yangu?’
            Mipawa anakula mic “utajiri wa mheshimiwa Kapende unafahamika. Hivyo hana haja ya kuutaja hasa ikizingatiwa kuwa yeye si kiongozi.”
            Mgoshi Machungu anakatua mic “wagoshi mimi sihitaji hata kujua utajii wa rahis na makamu wake hasa ikizingatiwa kuwa ni watendaji wema wenye historia safi. Ningependa kujua utajii wa watanguizi wao ambao wameiingiza kaya yetu kwenye umaskini na kuwa shamba la chizi visivyo na kifani. Cha mno ningependa kujua utajii wa vitegemezi na vitegemezi vya Njaa kai ii kuwawajibisha bia kuindana kama iivyo.”
            Msomi anarejea “hapa ndugu yangu Mgoshi unataka kufukua makaburi na ushindwe kuyafukia kama jamaa. Kama tungekuwa tunawajibishana vilivyo na kwa haki, Njaa Kaya na ukoo wake wangekuwa Segerea wakinonihino kwenye debe wakingojea Pilato awafunge maisha au kuwanyonga na kunawa maji kuwa dhambi zao hadaiwi. Hata hivyo, nani amvishe paka kengele wakati tuliowategemea wameonekana kugwaya na kujifanya hawaoni wala hayawahusu wakati wanaona na yanawahusu?”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anakula mic “mie msinikumbushe yule mama mwalimu mwenzangu tena kihiyo kutengeneza njuluku hadi akamiliki shule yake binafsi. Hamkusikia walivyozuia mizigo yake bandarini na kuanza kubadili lugha kuwa hakuwa na mizigo wakati tunajua kuwa biashara yake maiaka yote imekuwa ni kuhujumu kaya na kutumia ofisi ya dingi kujineemesha kama mama Anayo Tamaa Makapi? Mimi nmependa ya Dokta Kanywaji kumzuia bi mkubwa wake kujiingiza kwenye uchuuzi wa kipuuzi kwa mgongo wa kukuu hata kama ana madhaifu yake kama kuwalinda majambazi na vibaka hawa wakubwa.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu “mie naona tudhamirie mwaka huu kufukua makaburi lau hawa wezi tunaowajua tuwawajibishe ili kutoa somo la uwajibikaji kwa wachovu wote badala ya kuhubiri maji na kunywa mvinyo kama ilivyo. Tunataka uwajibikaji hasa kurejesha nyumba za wachovu zilizoibiwa na kutwaliwa na Dugong Denjaman Makapi ambaye naona siku hizi hasikiki baada ya kuadhirika kiasi cha kutegemea hisani ya dingi ambaye ni dogo kwake. Ama kweli hujafa hujaumbika! Nani alitegemea mjivuni kama Denjaman kuufyata hivi tena kirahisi. Angejua kila lenye mwanzo lina mwisho wala asingepoteza muda kujidai asijue ni dalili za uvivu wa kifikiri.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si akapita Njaa Kaya akitoka kuzurura! Sauti zilisikaka, msulubishe huyo Vasco da Gama!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.

No comments: