Wednesday, 4 January 2017

Kijiwe chashangaa utendaji wa kizimamoto


            Mgoshi Machungi anaonyesha kuuanza mwaka kwa hasira. Anaingia akiwa anasonya na kuzungusha kichwa kana kwamba ataua mtu leo. Anaamkua na kusema “wagoshi, mmesikia hiki kizungumkuti cha kupanda na kuzuiwa kupandisha umeme? Hivi tinakwenda wapi kama kaya jamani? Yaani tinapeekwa peekwa kama hatina akii!”
            Msomi Mkatatamaa anamjibu “kaka unaongelea haya maigizo na usanii! Mie sishangai. Kama wamekataa kuwajibishana vilivyo, unategemea nini? sasa wameanza kujichanganya, kutuchanganya na kuchanganyana. Wanaanza kushikana uchawi na kujivua nguo hadharani. Wanafanya mambo utadhani lisirikali si moja. Ngoja sasa niwape ishu kwa undani. Japo wamebana na kusema hatawapandisha bei za umeme, watapandisha tu hasa ikizingatiwa kuwa hawataki kushughulikia chanzo cha tatizo. Badala yake nao wanakuwa sehemu ya tatizo badala ya kuwa suluhisho la tatizo. Wanawavutia muda. Kilichofanyika ni kupima maji na ku-pre-empty ili kuona reaction yenu. Mkishawekwa sawa umeme utapanda tu.”
            Kapende anakatua mic na kuronga “nami naamini umeme utapanda tu hasa ikizingatiwa kuwa Dokta Kanywaji ameshindwa kufumua mikataba ya kijambazi na kuwatumbua waliosababisha kadhia hii. Yaani tunazidiwa na vikaya kama Ulundi, pamoja na migogoro yao, vinaweza kuwapa wachovu wake umeme! Tunapelekwa wapi na kwanini. Tunaswagwa kama kondoo wanaofikiri kwa makamasi badala ya ubongo!”
            Mipawa naye anakula mic “kuna jamaa yangu amenitonya kuwa hawa hawa wanaozuia kupanda kwa bei ya umeme ni wale wale wasiolipia ankala zao zitokanazo na matumizi mabaya na ya kizembe kwenye ofisi za umma.  Wambie walipe malimbikizo yao uone kama umeme utapanda. Wambie wapiga marufuku vijikampuni vya kitapeli kama AiptL uone kama umeme utapanda. Wanashindwa kushughulikia mambo ya wazi kamahaya; halafu inataka kuwatwishi nzigo wachovu. Hii ni haki jamani?”
            “Yakhe maneno yako yankata wallahi.  Nahisi hata kumwaga chozi kwa ninavooona haya mambo tena ya hovyo kwa kaya kama yetu ilopata uhuru wake miaka mingi ilopita. Twafanyiwa utwahuti kana kwamba tu hamnazo! Hapa lazima tuwabane wawajibishane; hata kama rahis alisema hawezi fukua makaburi kama hili la Tanisco. Sasa kama yeye ashindwa sie wanyonge tufanye nini? kama ashindwa wakati anavyo vyombo vya usalama na kila aina, huyu mchovu wa kawaida ende wapi na kwa nani?” mpemba analalamika huku akijiweka vizuri kwenye benchi.
            Kabla ya kuendelea, Kanji anaamua kumchomekea na kusema “Ami acha mie nichomeke veve hapa. Hii nauma sana roho kama naona witu va howo nafanyika kwa kaya yetu. Mimi iko changanya sana.  Kama hii nasema hii na ile na sema ile siju vananchi ya kavaida naeleva nini. Iko kuwa kama yote iko chizi nafanya mambo ya howo bila aibu.”
            Da Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kula mic “wenzenu wanafanya siasa kwenye mambo nyeti kiasi cha kutuacha tukisulubiwa na hofu na ugonjwa wa moyo. Unawezaje kuongeza bei ya umeme bila kuongeza mapato ya wachovu binafsi kama vile mishahara? Huu ni uuaji ambao unapaswa kupigwa marufuku kama alivyofanya mtukufu rahis. Mie nampongeza sana rahis kwa hatua zake za kupiga marufuku ulanguzi wa umeme. Huu si upandishaji wa bei bali ulanguzi. Sina lugha nyingine ya kutumia hapa kusema ule ukweli.”
            Mheshimiwa Bwege anaamua kutia guu na kusema “ninachohofia hapa si kupanda bei za umeme bali ugumu wa maisha utakaotokana na ulanguzi huu kama alivyouita da Sofi. Naunga nawe da Sofi; huu ni ulanguzi wa hali ya juu. Ni jinai isiyo ya kawaida.”
            Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomekea Mheshimiwa  Bwege na kusema ‘chonde chonde Mheshimiwa. Eti unaungana na da Sofi! Unamaanisha nini hapa kaka; hebu tueleze tu-comprehend vizuri. Kwanini usimuunge mkono badala ya kuungana naye tena hadharani?”
            Da Sofia anampuuzia Mbwamwitu na kuendelea kuchonga “nadhani sisi kama waathirika tuache masihara na kuamua kutafuta suluhu ya kudumu badala ya hizi suluhu zimamoto. Huwezi kuzuia ulanguzi wa umeme bila kuzuia wizi wa miaka nenda rudi ambao tumekuwa tukifanyiwa na matapeli waliopewa dili za kuzalisha na kulangua umeme.” Anapiga chafya na kuendelea “mie nadhani jibu tunalo waathirika wa kadhia hii ya ulanguzi wa umeme. Kwanini tusiandamane na kwenda kufunga viwanda vya wizi kama hii AipTl ambayo imekuwa ikiiba njuluku zetu na kusababisha ulanguzi wa nyenzo hii muhimu kwa maisha yetu? Kwanini hata rahis hatawatumbui hawa au hawagusiki tokana na uzito na mtandao wao? Lazima tujue mbivu na mbichi kama waathirika. Hapa lazima tuwekeze kwenye umoja wetu na kugomea ulanguzi huu kwa kutoa tahadhari kuwa kuna uwezekano pakachimbika bila jembe hapa kama wataendelea kutuchezea makidamakida kama makinda. Sisi ni wachovu wazima na si makinda.”
            Baada ya kusikiliza maoni ya kijiwe, Mgoshi anarejea na pendekezo babu kubwa. Anasema “kwa vie tinajua iipo tatizo, kwanini tisiandamane kuanzia hapa ii wahusika wapate taifa kuwa tinaweza kubadii kila kitu siku moja tu? Tunawashutumu woga kwa kutochukua hatua; acha sisi tichukue hatua hizo kuanzia hapa sasa hivi.”        
            Kijiwe kikiwa kinanoga si ukapita mgari wa AipTl. Acha tuupopoe kwa mawe!
Chanzo: Tanzania Daima leo Jumatano.

No comments: