Sunday, 15 January 2017

Magufuli ataweza kutumikia mabwana wawili?

      

 

              Hakuna ubishi. Rais John Magufuli ana kibarua kigumu. Hii ni kutokana na mfumo mbovu aliorithi bila kuwa tayari kuufumua na kuufuma upya kisheria zaidi ya kufanya hivyo kisiasa. Juzi akiwa mkoani Simiyu, utata na mparaganyiko wa mfumo umefichua ukweli kuwa Magufuli sasa anao mabwana wawili wa kutumikia yaani utawala wake unaotaka kuwakomboa wananchi, na kuulinda ule utawala mbovu uliowafikisha wananchi anapotaka kuwatoa Magufuli. Moja ya vilio alivyosikia toka kwa wananchi wa Simiyu ni ukosefu wa maji. Katika kutoa majibu mujarabu Magufuli aliamua kuwatoa mbele wahusika ili wawape wananchi majibu stahiki. Mmoja wa watumishi hao alimwambia rais kuwa tatizo la ukosefu wa maji kwa makao makuu ya mkoa  yaani mji wa Bariadi ni kutokana na kukwamishwa na mwekezaji ambaye eneo lake ni kilima yanapopaswa kuwekwa matenki ya maji ili yasambazwe.
            Baada ya kuelezwa hivyo, rais aliamua kutolea uvivu uwekezaji wa kijambazi ulioingiwa na mtangulizi wake, luteni Kanali Jakaya Kikwete kwa kuamuru matanki yawekwe;na kama mwekezaji atapinga afutiwe leseni ya uwekezaji. Wananchi walishangilia na kupongeza hatua hii bila kufikiri madhara inayoweza kulisababishia taifa huko tuendako.
            Kwanza, sijui kama rais alijiridhisha kuwa kuna upenyo wa kisheria wa kufanya aliyoamuru au aliamua kuvunja sheria kwa kutumia madaraka makubwa aliyo nayo.
            Pili, sijui kama rais alijipa nafasi ya kumjua mwekezaji husika na angalau kumsikiliza kabla ya kutoa hukumu ya upande mmoja. Tungependa kumjua na kujua namna alivyowekezewa hiyo ardhi na lini.
            Tatu, mwekezaji naye ana haki ya kusikilizwa kuliko kutoa amri baada ya kusikiliza upande mmoja. Maana bila kufanya hivyo, Tanzania itaonekana kama kigeugeu inayohubiri uwekezaji na uchumi wa viwanda wakati ikipingana na sera yake yenyewe.  Hii inaweza kujenga picha mbaya kiasi cha kuwatisha wawekezaji jambo ambalo litakuwa kikwazo kwa mafanikio ya sera za rais Magufuli.
            Nne, kuna haya ya kujua ukweli kama kweli mwekezaji alifuata taratibu zote–au hakufuata utaratibu–na  inakuwaje leo rais aamue kutishia kufuta hati yake? Je rais amefuata sheria katika kutoa amri yake; baada ya kushauriwa na wanasheria au ametoa tamko na amri vya kisiasa vinayopingana na sheria kiasi cha kuwa tatizo baadaye?
            Tano, tunapaswa kuangalia tatizo ni nini? kuna wakati wengine tunawalaumu wawekezaji wakati matatizo ni yetu. Sioni kama Magufuli anaweza kufikia anakotaka bila kufumua na kuufuma upya mfumo wa hovyo wa sasa aliorithi toka kwa serikali ya mtangulizi wake Luteni Kanali mstaafu Jakaya Kikwete ambayo ililsifika kwa ulegelege na rushwa na matumizi mabaya na ukosefu wa umakini. Sitegemei Magufuli afanikiwe bila kuanzisha mfumo wake mwenyewe unaoendana na dira yake. Hapa la kufanya ni moja; ima Magufuli aanze kujenga misingi ya utawala wake kwa kupambana na maovu na waovu wa awamu zilizopita au anyamaze amalize muda wake kama wenzake. Maana haiwezekani kuwatumikia mabwana wawili yaani kuwakomboa wananchi  huku ukiwakingia kifua waliowafikisha kwenye mtego unaotaka kuwakomboa.
            Sita, nitatoa mfano mmoja hapa. Uwekezaji mwingi uliofanyika tangia wakati wa serikali ya awamu ya pili hadi ya nne mwingi ni wa kijambazi. Hivyo, utamkwamisha Magufuli kutokana na kuwepo sheria za hovyo zinaoulinda. Wakati ule hapakuwapo na maadili ya uongozi ambayo Magufuli analenga kuyarejesha. Hata ukiangalia wajumbe wa kamati ya Maadili ya Viongozi aliyorithi toka kwa Kikwete ina sura za kifisadi zinazojulikana.  Mfano kuna mjumbe mmoja Hilda Gondwe ambaye anadaiwa kujiuzia gari aina ya Toyota Landcruiser la Mkoa wa Kilimanjaro kwa bei ya kutupwa. Sijui kama bado ni mjumbe na kama bado ni mjumbe hili linatosha kuwasha taa nyekundu kwa wahusika kumsimamisha na kumchunguza.
Ukiachia mbali na huyo, ukienda mahakamani ambako wawekezaji watakwenda kufungua kesi za madai ya kuvunjwa mikataba au  kufutwa leseni zao na kusababishiwa hasara, wamejaa majaji vihiyo na mafisadi kibao. Watakwenda kule watahonga na kushinda kesi wakiilazimisha serikali kuwalipa mabilioni. Fumua mahakama zote kwanza ili upate watu waadilifu na wenye uchungu na taifa lao wanaojua kazi zao waliosoma vilivyo siyo walioghushi kama alivyowahi kudai mwanasheria Tundu Lissu. Hapa narejea ushauri wangu ambao huwa nikiutoa. Majaji au mahakimu wote wenye tuhuma za ubadhilifu, rushwa na ufisadi wanapaswa kuondolewa ofisini. Marehemu baba wa taifa alikuwa na kisa kimoja ambacho alipenda kukitumia alipokuwa akiongelea usafi wa kimaadili. Alizoea kusema kosa la mke wa Kaisari si kutenda uovu ambao kimsingi ni uzushi bali kushukiwa. Mke wa Kaisari hapaswi kutuhumiwa kwa uchafu achia mbali kuutenda. Sasa inakuwaje tunapokuwa na watu waliotuhumiwa wazi wazi wakaendelea kukalia viti vya kutoa haki wakati wao ni wavunja haki na wachafu?
            Tumalize kwa kumshauri Magufuli achague wa kutumikia kati ya mabwana wawili yaani wananchi, na viongozi wastaafu waovu, wateule wao, mfumo wao mbovu na maafisa wengine wa umma wenye kutuhumiwa kutenda uovu na ukosefu wa maadili mbali mbali.

Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: