Monday, 23 January 2017

Barua ya wazi kwa mheshimiwa Godbless Lema

Mpendwa Godbless,
            Naamini hujambo huko uliko kwenye mazonge ya kufungwa bila kuhukumiwa. Najua ni machungu kiasi gani unapitia wewe, familia, marafiki na chama chako bila kusahau wapiga kura wako na watanzania wapenda demokrasia ya kweli na utawala bora nchi nzima.
            Wapenda amani, demokrasia na haki tunajua kinachoendelea; ni kinachokusudiwa kwa kunyimwa dhamana na kufungwa kwa muda mrefu bila maelezo ya kina. Waingereza huiita hii character assassination ambapo zandiki hulenga kukufanya uonekane kama mtu asiye na heshima wala maana kwenye jamii. Pia unaweza kuita kinachoendelea, licha ya kuwa uvunjaji wa sheria na haki za kiraia za kikatiba ni kile waingereza huita breaking someone’s spirit ambayo ni hali ya kumweka mtu kwenye mateso na mazingira ya kumfanya aondoe matumaini na kujiona si chochote si lolote. Wewe nakujua; ni mpiganaji asiyetishwa wala kukatishwa tamaa. Nakujua kupitia vyombo vya habari. sikujui personally. Hata hivyo, licha ya kuwa mwandishi, msomi na mchambuzi, ni mfuatiliaji wa mambo yanayofanyika nyumbani japo naishi ughaibuni.
            Mheshimiwa Lema, niliguswa sana na kinachoendelea nchini ambapo kuna wimbi la ajabu na hovyo la kuwafunga wabunge wa upinzani. Sina maana ya kusema kuwa nyinyi ni malaika. Je kwanini wabunge wa upinzani? Je tuna majambazi tena yanayojulikana mangapi yamejazana bungeni na hayaguswi kwa vile hayapingi wenye mamlaka? Hivi wale waliopewa fedha ya Escrow si majambazi wa kawaida hata kama hawatumii bunduki bali kalamu? Je walioshiriki ujambazi wa ununuzi wa rada na ndege ya rais wakajipatia mabilioni ya shilingi si majambazi hata kama wanaitwa waheshimiwa? Je hapa tunamdanganya na kumkomoa nani na hadi lini wakati ukubwa una mwisho? Wako wapi akina Benjamin Mkapa waliotuita wavivu wa kufikiri? Wako wapi akina Basil Pesambili waliotutaka tule majani ili wafanikishe jinai yao? Wako wapi majambazi wa EPA na Kagoda? Wako wapi waliohujumu UDA na kuitoa kwa wenzao?
            Mheshimwa Lema, najua ukipata waraka huu utafarijika japo kwa siku moja kujua kuwa wapo wanaothamini mchango wako. Ninachoweza kusema ni kwamba wanaweza kuua na kutesa mwili lakini si roho wala mawazo yako. Akina Nelson Mandela walipitia huko. Akina  Walter Sisulu, Oliver Tambo, na wengine wengi walipitia huko. Je walikatishwa tamaa na wakandamizaji wao? Je walisaliti mawazo, misimamu na imani zao? Hasha. Badala ya kuwavunja moyo na kuwafanya wajione hawafai, walizidi kuimarishwa na kusimamia kile walichoamini. They can destroy your corporeal world but not your spiritual one. Sitatafsiri hii. Orodha ya wahanga na mashujaa ni ndefu. Akina Edward Moringe Sokoine, Steve Bantu Biko, Solomon Kalushi Mahlangu, Edwardo Chivambo Modlane, Samora Moise Machel, Josiah Mwangi Kariuki, Pio Gama Pinto, mtemi Mkwawa, Milambo na wengine wengi waliuawa na wakandamizaji. Hata hivyo, bado tunawakumbuka na kuwaenzi kwa kujitoa kwao mhanga kwa ajili ya demokrasia na haki. Bado historia zao zimeandikwa kwa wino wa dhahabu si kwa sababu nyingine bali kupambana na ukandamizaji na kujitoa mhanga kwa ajili ya watu wao. Wako wapi akina Christopher Mtikila, Kassim Hanga, Major Tito Okello na mashujaa wengine? Nani huyu hataonja mauti?
            Mheshimiwa Lema, japo ujumbe huu ni wako, si wako peke yako; ni wako na mkeo, watoto wako, wazazi wako, ndugu zako, wapiga kura wako, marafiki zako na wapenda haki wote nchini na duniani kwa ujumla. Sitajadili kesi unayopambana nayo mahakamani. Ni kinyume cha sheria. Badala yake nakuandikia kama binadamu ambaye hujafa wala hujaumbika. Nani anajua mwisho wake hasa katika safari ya kisiasa? Je mbora kati yetu ni nani kati ya wazandiki, mafisadi, maimla na wababaishaji na wapigania haki?  Najua fika, kuna mambo yasiyo ya maana yanaweza kuwa yanaendelea kisiasa pamoja na kuwa na serikali inayochapa kazi. Nilishangazwa na kifungo chako kisicho cha kawaida na kile cha mwenzio mheshimiwa Peter Lijualikali ambaye naye na familia yake, wapiga kura wake, marafiki zake, ndugu zake na wapenda haki watafarijika na ujumbe huu.
            Shujaa na kipenzi cha dunia Nelson Mandela aliwahi kusema “ bindamu anaponyimwa haki ya kuishi maisha anayoamini, hana chaguo zaidi ya kuwa mhalifu” hata kama kwa kubambikiwa kama ilivyo kuwa kwake alivyoitwa gaidi na magaidi, mhalifu na wahalifu, mtu hatari na viumbe hatari na majina mengine mengi.
            Nichukue fursa hii adimu na adhimu kumuomba rais John Pombe Magufuli asiruhusu washauri wabaya kuichafua serikali yake. Asiruhusu siasa za visasi na ukandamizaji nchini. Asiruhusu siasa za upendeleo na upatilizaji. Sote ni wana wa nchi hii na tuko safarini ambayo mwisho wake hakuna ajuaye. Siasa si vita ya bunduki bali vita ya hoja. Tupingane na kutofautiana bila kukomoana wala kuumizana. Huu ni utamaduni tulioachiwa na baba wa taifa marehemu Julius Kambarage Nyerere ambaye wanyonge humuenzi kila siku bila kukoma hata kama walevi wa madaraka na mafisadi wanamkashfu na kumng’ong’a kwa kutenda tofauti na  haki na usawa wa binadamu visivyojali upinzani wala serikali tawala. Tufikie mahali tukomae kisiasa na kufanya vitu kama watu wazima na wenye akili.
            Mpendwa Lema, leo naishia hapa nikizidi kukuombea ushinde mtihani huu na kuvuka salama huku ukipiga moyo konde. Kwani yote yana mwisho. Haya ni mapito; na kila binadamu anayo mapito yake.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili jana.

No comments: