The Chant of Savant

Wednesday 18 January 2017

Magufuli hana haja ya kutishia vyombo vya habari

            Taarifa za vyombo vya habari zilizomnukuu rais John Pombe Magufuli akiyaonya magazeti mawili kutokana na kile anachosema ni kuandika habari za uchochezi si njema kwa taifa  tena la kidmokrasia kama Tanzania.
            Vyombo vya habari, sawa na Magufuli, vinatekeleza wajibu wake kisheria. Hivyo, hakuna mwenye mamlaka kisheria kuvitisha au kuvilazimisha vifanye anavyotaka. Je Magufuli anaweza kukubali kutenda kazi zake kulingana na matakwa ya vyombo vya habari? Nadhani, Magufuli anahitaji ushauri tena mzuri kuhusiana na namna vyombo vya habari vinavyofanya kazi. Hana haja ya kuviona kama adui kama anatimiza wajibu wake kisheria au pale vyombo vya habari vinapotimiza wajibu wake hata kama hapendi kinachoandikwa.
            Uzoefu unaonyesha; hakuna mtawala aliyeshindana na vyombo vya habari akashinda; hasa ikizingatia; wote wapo kwa mujibu wa sheria. Vyombo vya  habari vipo kwa ajili ya wananchi na si watawala. Pia vyombo vya habari vinapotokea kukiuka sheria, kanuni na taratibu, kuna utaratibu wa kisheria wa kushughulikia hili; na si kutunishiana misulu na kutishana. Sidhani kama wote tunaweza kuangalia mambo kwa namna moja tukawa salama. Binadamu ni tofauti na wanyama ambao huwa hawabadiliki tokana na kutojaliwa utashi katika maisha yao.
            Hata Yesu alisema “kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?” Wakorintho 12:19. Kama vyombo vyote vitaisifia na kukubaliana na kila inachofanya serikali, mawazo mbadala yatatoka wapi? Jamii isiyokosoana haiwezi kukithi matarajio ya wanajamii wake hasa ikizingatiwa: tuna vionjo na vipaumbele tofauti kama raia wa taifa moja. Kama alivyo na malengo na mipango yake na vyombo vya habari kadhalika. Itakuwa ajabu kuona vyombo vyote vya habari vikisifia kila anachofanya Magufuli. Isitoshe, vipo vyombo vya habari vilivyoanzishwa na kulipwa kwa ajili ya kusifia serikali hata ikifanya mambo tofauti na inavyotakiwa. Pia, vipo vyombo vya habari vinavyojikomba kwa serikali ili vikumbukwe kwenye ulaji. Hivi ni vyombo vya habari uchwara vinavyotumiwa na waganganjaa kupatia kitumbua hata kwa kupinda na kupotosha maadili (ethics) za uandishi . Hivi ni vyombo vya habari vilivyojaa makanjanja wanaotumia kalamu zao kutafuta vyeo na ulaji rahisi. Tuliyaona wakati wa utawala uliopita. Baadhi ya waliodhaniwa kuwa waandishi nguli walijidhalilisha na kujitoa mwili na roho kuandika upuuzi wa kusifia upuuzi ili watupiwe vyeo kama vile ukuu wa Wilaya, Ukatibu katika ofisi za chama tawala na upuuzi mwingine. Pia, vipo vyombo vya habari ambayo hupenda kuviita mbwamwitu vikilinganishwa na vile mbwa wa kufugwa visivyokuwa kujikomba lau vipate tenda, matangazo au wanaovitumia wapewe vyeo hata kama hawana sifa wala stahiki.
            Magufuli alikaririwa akisema “hayo magazeti kila ukisema hivi yanapindisha, siyataji kwa sababu yanajifahamu lakini yajue kwamba siku zake zinahesabika. Serikali ninayoiongoza haiwezi kukubali amani kuvurugwa.” Kupindisha ni neno tata. Yanapindisha nini na kwanini? Je amani inaingiaje na upindishaji? Hivi rais akisema uchumi umekua, kwa mfano, magazeti yakasema unadumaa, yanatishia amani? Hapa kinachotakiwa linapotokea jambo kama hili ni kwa wawili kuthibitisha madai yao. Simple. Huwezi kulinganisha Tanzania na Rwanda kuhusiana na kilichotokea mwaka 1994 kwenye mauaji ya kimbari. Kilichosababisha mauaji haya ni mabaki ya ukoloni na utawala mbovu. Vyombo vya habari vinatupiwa lawama kwa vile vilitumiwa na wanasiasa wakabila na wasiotenda haki.  Kwa waliosoma historia ya Rwanda, mauaji ya kimbari yaliasisiwa na wakoloni wa Kijerumani pale walipowadanganya Watutsi kuwa ni bora kuliko Wahutu yakaendelezwa na watawala wa Kibelgiji waliochukua nchi ile baada ya vita ya pili ya dunia chini ya kile kilichojulikana kama tutsification (Prunier 2009: 3 aliyekaririwa kwenye Ibreck 2010: 2). Huu ni ukweli (a set of facts). Kuna methali ya kiingereza isemayo Truth is a spectre that scares many (ukweli ni jinamizi linalotisha wengi). Wanaohofia mauaji ya kimbari wanakwenda mbali zaidi ya wanavyopaswa ima kwa kutojua au kwa woga au hila ya kutafuta kisingizio. Kilichosababisha mauaji ya kimbari zaidi ya mabaki ya ukoloni (colonial carryovers) ni ubaguzi na ukosefu wa haki. Huwezi kuwabagua watu tokana na asili au imani yao ukawa salama. Kinachotakiwa nchini si kutishana bali kutenda haki kwa mujibu wa sheria. Huwezi ukabagua magazeti na kutishia kuyakandamiza yakakupenda. Kila binadamu amejaliwa akili na utashi wa kuchagua, kuchuja na kudurusu mambo. Kama vyombo vya habari vitapindisha ukweli vishitakiwe na si kutishiwa kufungiwa wala kufutwa.
            Kusema kuwa  baadhi ya vyombo vya habari vinaandika habari za kichochezi ni kupindisha na kupotosha ukweli anaodai rais unapotoshwa na vyombo vya habari. Kuna msemo kuwa there are three sides to every story: yours, theirs and the truth. Huwezi kuchochea watu wakakusikiliza kama hawana lao. Kusema kuwa watanzania ni viumbe wa kuchochewa na kutenda ni kuwageuza hamnazo na wasioweza kupembua. Mfano, huwezi kuandika kuwa rais yuko uchi wakati amevaa suti ukasikilizwa au kuaminiwa. Lazima tukiri kuwa kuna tatizo. Mfano, serikali yoyote inayotaka kusifiwa bila kulaumiwa ina matatizo. Kama binadamu ambao tumejaliwa udhaifu (fallibility) tukubali. Kuna sehemu tunakosea; na kuna sehemu tunapatia. Huu ndiyo ukweli na ndiyo majaliwa ya binadamu. Hekima ya kawaida inasema ni heri akukosoaye kwa haki kuliko akusifiaye ujinga.
            Tumalizie kwa kumtaka rais Magufuli aangalie upya kitisho chake dhidi ya baadhi ya vyombo vya habari. Tanzania ni mali yetu sote kwa sawa. Pale atakapofanya vizuri ataelezwa.  Kadhalika, pale atakapokosea atakosolewa tu. Asiyekosolewa ni Mungu tu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

No comments: