The Chant of Savant

Sunday 18 June 2017

Bila katiba mpya Magufuli anajipiga mtama


            Kupiga mtama ni neno la mtaani lenye kumaanisha kupiga ngwara. Kwa kishona humaanisha ujuzi au maarifa na maumivu ayapatayo mtu kidoleni hasa unapojikwaa. Leo nitatumia neno ngwara kuonyesha namna Tanzania, kwanza, ilivyohujumiwa kiasi cha rais John Magufuli kuuliza”nani alituroga Tanzania?”
Nitajaribu kudurusu mambo au sababu zinazoikwamisha Tanzania au tuseme uchawi –kwa wale wanaoamini katika kurogwa kiasi cha kutaka kuombewa badala ya kuambiwa ukweli kuwa sisi ni sehemu ya tatizo. Hivyo natoa yafuatayo:
Mosi, urathi wa au mabaki ya ukoloni au colonial carryover. Baada ya kupata uhuru na kurithi mfumo mbovu wa uongozi wa ima kuiga au kudandia, tulijikuta tukijenga matabaka ya watu miongoni mwa raia wetu. Hii unaweza kuiona kwenye sheria zinazoongoza nchi yetu kuhusiana na makosa ya wizi mkubwa na mdogo. Mtu akiiba kuku anafungwa miaka mingi kuliko anayeiba mabilioni. Wakoloni waliweka mfumo huu ili kuwafunga waswahili pale wanapowadokolea huku wakiwalinda mawakala wao ambao walikuwa wakinyanya fedha nyingi jambo ambalo tuliliendeleza hadi leo.
Pili, ni ile hali ya nchi kuendesha na katiba zisizotokana na matakwa wala utashi wa wananchi au superimposed constitution. Katiba ya Tanzania haijawahi kutokana na wananchi. Badala yake ima ilitokana na mkoloni–baada ya majadiliano katika jumba la Lancaster–au chama kimoja–katiba ya jamhuri ya muungano ya mwaka 1977 iliyotokana na vyama vya Tanu na ASP. Kihistoria Tanzania imekuwa na katiba tano, yaani Katiba ya Uhuru (1961-62), Katiba ya Madaraka au Jamhuri (1962-64), Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (1964-77) na Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977 ambayo iliundwa baada ya vyama vya ASP na TANU kuunganishwa na kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo imekuwa ikifanyiwa marekebisho na kujaa viraka kiasi cha kujitenga na wakati na matakwa ya watanzania.
Matumizi mabaya ya madaraka ya baadhi ya viongozi wetu. Rais wa Tanzania yupo juu ya katiba. Unategemea nini unapomuweka binadamu juu ya sheria zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka. Anayebishia hili arejee historia ya Tanzania aone namna serikali za kuanzia awamu ya pili hadi ya nne zilivyoshiriki na kuhalalisha ufisadi kiasi cha kuzaa kadhia ya ufisadi wa kutisha kama unavyoendelea kuibuliwa na serikali ya awamu ya tano. Tokana na rais kuwa juu ya sheria, karibu awamu zote tajwa zilitegemea utashi wa rais kuendeshwa. Mfano, rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliporuhusu kile kilichotafsiriwa kuwa RUKSA, wengi hawakujua madhara yake. Kimsingi, hapa ndipo mizizi mikubwa ya ufisadi ilipojikita nchini. Haina maana kuwa hapa mwanzo hapakuwapo na rushwa. Ilikuwapo; ila mwalimu Julius Nyerere alijitahidi sana kupambana nayo chini ya mfumo wa Kijamaa ambao ulimpa uwezo wa kumwajibisha yeyote aliyeshuku alikuwa fisadi.
Alipoingia Benjamin Mkapa–hasa muhula wake wa mwisho–viwango vya ufisadi vilikua zaidi hasa ilipobainika kuwa kumbe kuna watu waliomtumia yeye au mkewe kujinufaisha kwa kutegemea ukoo au nepotism. Rejea kashfa ya kuuzwa kwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambapo ushahidi ulionyesha kuwa waliokuwa makuwadi wa walioinunua walikuwa washirika wa shemejize rais. Hata huu wizi mkubwa katika sekta ya nishati na madini chanzo chake ni kwenye serikali hizi mbili. Pamoja na kwamba ufisadi ni kizalia cha mfumo wa kipebari usio na huruma, kuna ushahidi mkubwa kuwa mabaki ya ukoloni nayo yamechangia sana hasa nchi zinapokuwa zinaendeshwa na katiba zisizotokana na watawaliwa au hoi polloi.
Tuje kwa Magufuli ambaye ameonyesha ujasiri na uzalendo wa hali ya juu unaoandamana na uchungu wa kuona Tanzania ikichezewa na kuliwa mbele na nyuma. Je atafanikiwa kwenye mapambano yake bila kuwa na katiba wezeshi na wananchi? Jibu analo Magufuli ingawa hataki kulikubali na kulitumia. Hapo tarehe 12 Juni, 2017, akipokea taarifa ya pili ya makinikia, alikaririwa akisema “ndugu zangu watanzania nimewambia nafanya hivi kwa ajili yenu…kazi [urais] ni ngumu sana… ndiyo maana tunaomba mtuombee…mimi muda wangu utapita.” Magufuli anakiri kuwa atapita na mfumo anaousimamia hauwezi kujiendesha. Kinachoshangaza ni namna anavyosuasua  au kuahirisha katiba mpya wa wananchi ambao licha ya kutumia fedha zao nyingi na muda, ilishafikia pazuri; na ilishapata maoni yao. Kwa wanaojua mchakato huu ulivyotekwa, kuvurugwa na kuchakachuliwa wanajua fika waliofanya hivyo hawakutaka iwatupe korokoroni tokana na ufisadi uliasisiwa na kusimamiwa na awamu zao. Sijui Magufuli anahofia nini wakati alishalionyesha taifa uzalendo wake? Pia, kama rais anajua kuwa atapita, sasa anashindwa au kuchelea nini kurejesha mchakato usiochakachuliwa wa katiba iliyopendekezwa na watanzania kwa maslahi yao na vizazi vijavyo; siyo kama kujipiga mtama? Wakoloni kwa kujua walichowatendea wengine, waliamua kuachana na katiba za kizamani na kutunga katiba ambazo zinaendesha nchi zao bila kutegemea utashi wa rais au awamu kama ilivyo Tanzania na nchi nyingi za kiafrika.
Tumalizie kwa kumtaka Magufuli atumie ujasiri, usongo na uzalendo alioonyesha kwenye kupambana na ufisadi, kurejesha katiba ya wananchi ili isaidie si kupambana na ufisadi bali kuuondoa kutokana na kuwa na vifungu vinavyoshughulikia ufisadi na maadili ya viongozi kivitendo na kisheria. Bila katiba mpya ya wananchi, Magufuli atashindwa na anajipiga mtama kama wasemavyo watoto wa mjini.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

No comments: