Saturday, 10 June 2017

Taasisi ya kuzuia rushua inaponuka rushua!

     Image result for photos of dr hoseah     Juzi tulibigwa na butwaa tukalewa bila kunywa. Si baada ya kigogo wa Taasisi ya Kukuza, sorry, Kuzuia na Kupamba, sorry, Kupambana na Rushua kukutwa na mimali ya mabilioni tofauti na stahiki yake. Leo sitaongelea mambo yaliyoko kwa pilato. Nitadurusu kilevi yanayowachanganya walevi kiasi cha kutaka tugawane kaya kila mmoja ajue njia yake kama mambo yenyewe ni hivi. Natamani tugawane kaya ili nipige zangu majuu lau nitanue kama wao watanuao wakutumia kodi za walevi. Nadhani Njaa Kaya na walevi wenzake ambao kitaalamu huitwa globetrotting parasites the boozers feed as they feed on them tunaelewana hapa.
            Nikirejea, huyu parasite mwingine, pamoja na kunaswa ntegoni, wapo wengi. Utawaona wakitukoga mitaani utadhani ukwasi wao halali. Ajabu nasi ni wa kulaumiwa. Tunapataje jeuri kuchoma vibaka tunagwaya kuwachoma mibaka iliyotamalaki kayani?
            Leo acha niwachomee kwa kutumia utafiti nilioufanya kayani kwa muda mrefu. Haya ndiyo matokeo yatokanayo na samples kidogo toka maeneo mbali mbali ya ofisi za umma. Katika utafiti wangu niligundua kuwa pale Bandarini wapo wengi tu. Wapo vijana wadogo–tena wenye elimu kiduchu–hasa wa vitengo vya makontena na mafuta wanavyomilki midude ya kutisha kuanzia akaunti nono, mahekalu, migari ya bei mbaya na mali nyingine fichi. Nenda TrA uone wezi hawa wanavyolipwa kodi ambayo ilipaswa kwenda sirikalini; viwanja vya ndege maarufu hutumika kupitisha bwimbwi. Wapeleleze wafanyakazi wa maeneo yale, utashangaa ukwasi waliokwishapunyua kwa walevi. Huwa nashangaa Usalama wa kaya kuacha kupambana na mipapa hii hadi wanageuka Uhasama wa Kaya (UK).
            Pekueni mikataba ya kijambazi inayoangamiza kaya kiasi cha kutufanya kushindwa kukata kanywaji. Nenda kwenye wizara ya viwanda muone madudu yanayoendelea kule ambapo viwanda vilibinafsishwa na kuishia kung’olewa mashine au kugeuzwa mabohari yakufichia wakimbizi wa kiuchumi toka ugabacholini na kwingineko. Nendeni uhamiaji ambapo pasi za kaya zinauzwa kwa magabacholi, wanigeria hata wasomali kama njugu. Nenda gesi la polish muone vijana wadogo wanavyomilki mimali haramu ya kutisha. Nenda mbuga za wanyama na kwenye wizara ya utalii uone wahalifu wanavyouza mali zetu kwa wachukuaji kuanzia wanyama hadi vitalu. Hivi ile kesi ya kutorosha wanyama hai iliishia wapi; au ndiyo huko kuendelea kuliwa tusistuke wala kulalamika? Nenda kwenye mahakama zetu zinazosifika kuuza haki japo wanaojihusisha si wote; mahospitali yetu uone midawa inavyouzwa; machimbo uone walivyofurika wageni walionunua vibali. Nenda mikoa ya mipakani uone wahamiaji haramu wanavyotanua. Nenda kila mahali, kama akili yako ni timamu, utalia sana kwa namna unavyoliwa mbele na nyuma.
            Leo ni mwendo mdundo. Nenda Masaki, Msasani, Oyster Bay, Mikocheni,Msasani, na maeneo mengine wanakokaa wazito muone mijengo iliyoporomoshwa bila maelezo. Ama kweli kaya yetu ishauzwa. Kwa walevi wasio na chochote wanapaswa kulia au kuamua kufanya kweli kuhakikisha wanawatokea wanaoibia kaya na kuwaponda na michupa yao. Nenda mipakani muone mipaka ya kaya ilivyogeuzwa maduka ya hawa wadukuzi wa njuluku zetu.
            Mie si bingwa wa kulalamika; nashauri yafuatayo:
            Mosi, tungeni sheria ya kumtaka kila mlevi kutangaza utajiri au umaskini wake na namna alivyoupata; akishindwa ukwasi utaifishwe huku akifikishwa lupango kutubia udokozi wake.
            Pili, taasisi ya UK isipoteze muda kuchunguza wanasiasa na wakosoaji; iwapeleleze wakwasi wezi. Hii ndiyo ilifanya mzee Mchonga kufanikiwa kwenye utawala wake kabla ya kuhujumiwa na wakoloni.
            Tatu, itungwe sheria ya kuhakikisha kila mlevi anajaza taarifa za mapato yake kila mwaka ili kujua kilichoongezeka na kilichopungua.
            Nne, tunga sheria za kufilisi na kunyonga wote watakaobainika wanaibia kaya. Tujifunze toka Uchina ambako ukipatikana umeibia kaya wanakufanyia kitu alichofanyiwa Saddam Hussein baada ya kuvunja ndoa yake na Wamarekani.
            Mwisho, uwepo utaratibu wa walevi kuwaripoti wenzao wanaojua wanapunyua njuluku zao. Lazima kila mmoja awe askari wa mwenzake bila kujali cheo, rangi wala ubashite, kujuana na upuuzi mwingine. Ngoja niende kupata kanywaji ili nichaji bongo tayari kuendeleza utafiti.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: