The Chant of Savant

Wednesday 7 June 2017

Kwanini Twaliwa Mbele na Nyuma Hivi?


            Mpemba anaingia akiwa na bashasha kuashiria ana jambo la kukiambia kijiwe. Baada ya kuamkua anasema “wallahi sikujua kuwa tumeliwa sana tena sana na kirahisi hivi. Twaliwa kama kwamba hatuna hata ilm wala akili! Yakhe twaliwa tena kijinga kweli kweli.”
                        Kabla ya kuendelea Mbwamwitu anamchomeke “mnaiwa vipi na nani na kwanini? Mbona sikuelewi eewi au nawe unataka kuanza mambo ya popobawa? Hebu tieeze tikueewe angau tiweze kumisaidia isiendee kudhaiishwa kwa kuiwa hivyo. Hujui kuwa inauma?”
            Mpemba anajibu “yakhe wankosea adabu na hishima sasa. Washangaani wakati ushaambwa kuwa kaya yaliwa kila upande mbele hata nyuma au wewe si mmojawapo? Kama wewe huliwi mboni juzi nilikusikia mwenyewe ukilalamika? Hukusikia yule kidhabu profedheha Muongo alikilalama aonewa. Kama si kututia madole huku nnini?”
            Mgoshi Machungi anamchomekea Mbwamwitu “hayo mambo ya kuiwa na popobawa yenu. Mie anie mtu hajitaki au anataka timpige zongo? Huyo Muongo akiiwa sawa. Kwani ameyataka mwenyewe kwa tamaa na ujinga wake.”
            Baada ya kugundua kuwa hawajamwelewa Mpemba anakula mic “nisemapo twaliwa namaanisha kama kaya. Hivi haya madini yanoibiwa na njuluku zinizoliwa si mali yetu? Hamkusikia kuwa hata kwenye mbolea nako wapiga njuluku?”
            Kapende aliyekuwa akibofya ki-Sumsung six anaamua kula mic “nadhani tuwe wakweli. Hapa anayeliwa siyo sisi bali wao tuliowapa madaraka wakaamua kujitoa waliwe na hao mabwana wao wanaoitwa wawekezaji wakati wachukuaji na wezi watupu. Sisi tuliwe tuna nini cha kuliwa wakati waliojaza kila kitu ni wao wenye maulaji yao. Huoni wanavyonenepeana wengine hadi kuanza kustukiwa kuwa si watoto riziki kama Bashite?”
            Mijjinga anatia timu “naafiki maneno yako dokta Kapende. Wanaoliwa ni wao; na wala wasituingize kwenye uchafu wao utokanao na upogo, ujinga na ubunga. Unaambiwa jitu lina PhD lakini ukiangalia linayofanya unashangaa lilisoma wapi na nini? Sikujua kuwa hata wasomi wangeliwa. Kama wameshindwa si waombe msaada kijiweni wasomi wa kweli tuwasaidie kuondokana na aibu hii?”          
            Msomi Mkatatamaa anaamua kutia buti “mna haki ya kusema msemayo kutokana na yatendekayo. Badala ya wajalaana kuwa makini na kumakinika wameachia makinikia, madini, njuluku hata raslimali. Hapa wasiliwe kwanini? Mie nasema tena kwa sauti na herufik kubwa, wanaliwa tena sana sana tu. Maana haiingii akilini waache kuliwa wakati wanaruhusu kaya yao iliwe. Ikiliwa kwanini wao wasiliwe? Bila kuliwa wasingeruhusu wizi huu wa mchana uendelee. Bila shaka vichwani mwao wanaliwa tu. Nadhani salamu hizi zinapaswa kupelekwa kwa Ben Makapi aliyetumia makapi yake kichwani; na kwa uvivu wake wa kufikiri, kuiingiza kaya kwenye mkenge huu wa kuliwa mbele na nyuma. Heri angeliwa yeye na mkewe mbele na nyuma kuliko kaya.”
            Anapiga chafya na kujifuta pua na kuendelea “kama dokta Kanywaji anata kututendea haki, basi aachane na Makapi. Badala ya kumkingia kifua kama Bashite, ampeleke lupango. Hapa atake asitake, atafukua makaburi na kuyafukia. Maana yananuka kweli kweli.”
            Mipawa aliyekuwa akijaribu kumchomekea Msomi bila mafaniko, sasa kapata upenyo. Anakula mic “Msomi nakubaliana nawe. Hakuna haja ya kuandikia mate ilhali wino upo. Badala ya dokta Kanywaji kulalamika, afanye kweli. Kamata Chinga Makapi na washirika zake mahabithi sweka lupango. Hapa tutakuelewa na kitaeleweka kuwa uko makini na si makinikia. Mengine tutajua baadaye. Vingenevyo naona kama michosho ya kibashiteshite au vipi huku kaya ikiendelea kuliwa mbele na nyuma, kulia na kushoto kana kwamba haina viumbe wenye akili, just common sense.”
            Kanji anaamua kutia guu. Anamwangalia Mgoshi; anatabasamu na kuendelea “hii taseme mimi jua hapana pendeza vengi kama veve Goshi Chungi. Kama nasema kaya naliva sitaki tukana bali sema kweli moyoni yangu. Sasa kama dini yote nasafirishwa nje na hapana juluku sirkali napata siyo liva hii? Kama siyo liva hii nini? mimi naona vote nasiriki jinga hii naliva bele na nyuma hata kama hishmiwa. Hiyo ndiyo chango yangu leo.”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anamchomekea Kanji na kusema “jamani hebu achaneni na mambo ya kuliwa. Badala yake tutoe mapendekezo ya kuondokana na hali hii au vipi? Mie naona tuchangishane njuluku kahawa na kuagiza smelter ili tuokoe njuluku zetu huku tukiwaza namna ya kuwanyonga wote waliotuingiza kwenye kadhia hii.”
            Mheshimiwa Bwege anakula mic “mie sina huruma na mijizi na mafisadi hata kama ina madaraka. Heri ipelekwe lupango ikaliwe huko huko badala ya kuendelea kula matunda ya kuhujumu kaya yetu. Leo sintosema mengi. Napanga kuitafuta mitoto isiyo riziki kama Muongo, Makapi, Njaa Kaya, Ni Zero Kadamagi, Endelea Chenga na mingine lau tuiifanyie kitu mbaya. Maana haina maana wala sababu ya kuendelea kula mali zetu badala ya kuliwa lupango.”
            Wakati kijiwe kinaanza kunoga si likapita shangingi la Endelea Chenga! Acha tumkwide shati kabla ya ndata kumuokoa!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.
 

No comments: