Sunday, 30 July 2017

Kwanini Hamad na Lipumba wamejivika kitanzi?

Image result for photos of lipumba and hamad
 
            Bila shaka wapenda demokrasia na mabadiliko nchini watakuwa wanasononeshwa, kushangazwa hata kuchoshwa na mgogoro usio na tija kwa taifa kwenye Chama Cha Wananchi (CUF) ambapo mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba na Katibu mkuu Seif Sharrif Hamad wamo kwenye mbio za kukiua chama; sijui wapate nini na kwanini na faida ya nani zaidi ya uroho wa madaraka; na kutoweza kuona mbali. Siamini kama Hamad na Lipumba hawajui wanachofanya pamoja na madhara yake ya muda mfupi na muda mrefu. Sijui kama kuna mshindi katika mtanziko huu wenye kila ishara za kuua chama na kudhoofisha upinzani kwa ujumla. Je wawili hawa wanatumika au wameamua kujitumia ili watesi wao waendelee kupeta kama wasemavyo watoto wa mjini?  Hii si mara ya kwanza wala ya mwisho kuwashauri wawili hawa kuwa wanachofanya hakiendani na dhana nzima ya upinzani na demokrasia ya vyama vingi. Sijui kama wanaangalia walikotoka ili wajue waendako au wanakwenda waendako kinyumenyume wasijue wanarudi nyuma.        Je Hamad na Lipumba watapata faida gani zaidi ya kugeuzwa vikaragosi kisiasa kiasi cha kutumika kama wenzao walioua vyama au kushindwa kuvikuza? Kwanini hawajifunzi toka kwa Augustine Mrema na yaliyompata baada ya kuua vyama kadhaa akaishia kuwa kiraka kisiasa? Je katika mkasa huu wa kujitakia nani wa kulaumiwa baina ya wawili hawa? Tuwalaumu wote au mmojawapo? Je wawili hawa wameweka maanani maslahi mapana na ya muda mrefu ya wananachama wa CUF? Je ugomvi wa wawili hawa unafichua kile kilichofichwa muda mrefu kuwa wanatumiana bila kujua au kwa kujua kila mtu akingojea zamu yake kama ilivyotokea kwa Lipumba baada ya kumfukuza Hamad na baadaye wabunge wote waliokuwa wakimuunga mkono? Je kinachoendelea ni ushahidi kuwa wawili hawa wameishi kwenye ndoa ya mashaka ukiachia mbali kuwa kwao cha muhimu ni madaraka kuliko maslahi mapana ya wananchama? Je kinachoendelea ni ushahidi kuwa chama hiki ni mali ya watu binafsi tena wawili lakini si wanachama?
            Kwa wanaojua historia ya CUF na kilichompata mwanzilishi wake, James Mapalala ambaye kimsingi kilimpata sawa na kilichompata Hamad ambaye alimpoka chama, hawashangai kinachompata Hamad kwa sasa. Ukiishi kwa upanga, utakufa kwa upanga. Ukidhulumu utadhulumiwa na ukipiga utapigwa. Kawaida, unavuna ulichopanda.
            Wanaojua namna Hamad alivyokuwa akikigeuza chama kama akaangaye samaki, wapo waliokuwa wakishangaa na kutoshangaa kilichompata hatimaye. Maana wakati akiwa ndiye kila kitu kwenye chama enzi zile, wengi walikuwa wakihoji; inakuwaje mtu mwenye shahada moja amtumie profesa wasijue kuwa naye aliyeonekana kutumiwa alikuwa akipiga mahesabu yake akimtumia aliyedhaniwa kumtumiwa kwa namna yake. Ni bahati mbaya sana. Hamad alidhani atamtumia Lipumba atakavyo kufikia malengo yake binafsi asijue na mwenzie alikuwa naye akipiga mahesabu yake. Ni sawa na kale ka mchezo ka Magomeni ambapo matapeli wawili walifanya biashara huku mmoja akimuuzia mwenzie cheni feki asijue amelipwa fedha feki. Ngoma droo. Kwanini dhana hii? Hamad, siku zote, aliekeza nguvu zake Visiwani huku akimweka Lipumba kama kikaragosi cha kuaminisha Bara kuwa Hamad alilenga kufanya siasa za Muungano. Rejea alivyoamua kuingia serikali ya Umoja wa Kitaifa (GNU) Visiwani bila kutaka irudufiwe Bara. Rejea kulalamikia kuibiwa urais Visiwani lakini si Bara. Hamad anapaswa aambiwe. Janja yake haitamfikisha mbali. Pia Lipumba aelezwe, wanaomshabikia na kumtumia kwa sasa, wakishamalizana naye watamtupa kama ganda la muwa la jana. Kwa vile wawili hawa wameweka historia (precedent) mbaya, sitashangaa siku moja Lipumba, kadhalika, akanyang’anywa chama kama alivyomfanyia Hamad sawa naye alivyomfanyia Mapalala.
            Wawili hawa wanapaswa kufahamu kuwa chama si kama mpira wa kunyang’anya kufikia kufunga magoli. Chama ni tofauti kabisa. Ni rahisi kukibomoa na vigumu kukijenga. Hili liko wazi; na naamini wawili hawa wanalijua. Sema wanajifanya kutoliona au wanapofushwa ima na uroho wa madaraka au mipango binafsi fichi.
             Kitu kingine wanachopaswa kufanya wawili hawa ni kuonyesha njia na kuwa sehemu ya suluhu ya matatizo yanayoikabili CUF ambayo, kimsingi, walianzisha wenyewe. Wasiendelee kujiruhusu kuendelea kuwa tatizo badala ya jibu la matatizo ya chama. Niliwahi kushauri kuwa wanachama wa CUF warejeshe chama chao mikononi mwao kwa kuhakikisha wanawafukuza wawili hawa ili kuendeleza yale waliyodhamiria kwenye kuanzisha na kujiunga na chama hiki kikiongwe nchini. Kama kweli Lipumba na Hamad wako serious na siasa za upinzani zinazolenga kuikomboa Tanzania nzima, wanapaswa kukaa kitako kwenye meza ya duara na kuzika tofauti zao kama njia mujarabu ya kutatua matatizo yanaoendelea kukidhoofisha na hatimaye kukiua chama. Kama haiwezekani basi mmoja akubali kushindwa aanzishe chama kingine kuliko kung’ang’ania chama kimoja mnachozidi kukidhoofisha.
            Tumalizie kwa kuwaasa Hamad na Lipumba kuwa wakiendelea na mchezo huu walioanzisha, watakuwa sawa wanaojivisha kitanzi. Mwishowe, watakufa wote. Hakuna atakayejeruhika; kwa vile hakuna wa kukata kitanzi walichojivisha kabla ya kuwaua kikatili. Hata hivyo, Hamad na Lipumba wanao uwezo wa kuchagua kifo kisiasa badala ya kusuluhisha tofauti zao na kusonga mbele.
Chanzo: Tanzania Daima J'pili leo.

No comments: