Saturday, 22 July 2017

Wanaopinga si wapumbavu bali wasiotaka kupingwa

Juzi walevi tulipigwa na butwaa. Si baada ya muishiwa mlevi mkubwa wa ulaji kupayuka kuwa sisi tunaopinga–mambo yanapokwenda ndiyo siyo–eti ni wapumbavu! Kama siyo kukaza roho, huenda hali ingekuwa tofauti baada ya walevi wote kushika michupa yao na kuingia mitaani kutaka tubadili katiba na kuondoa kinga kwa viumbe kama hawa wasiojua kuwa bila sisi wao si lolote si chochote. Tunawalisha, kuwavika, kuwatibia ughaibuni na anasa za kila aina dunia bure tena kwa kazi bure waliyofanya japo si wote halafu wanatutapikia hivi. Shame on you Dugong Makapi. Kama siyo upumbavu, hapa upumbavu wa walevi uko wapi?
            Baada ya kuinyaka kwenye runinga namna jamaa alivyopayuka, nilijikuta nikisema “how dare you Dugong?”  Jamaa huyu Tunituni mwenye uvivu wa kufikiri aliudhika kusikia eti baadhi ya walevi wanampinga kaisari anapozidisha mambo. Kwa wenye akili na hekima na si wajivuni, malimbukeni na wavivu wa kufikiri, kukosoana, licha ya kuwa chemi chemi ya maarifa, ni ustaarabu wa hali ya juu uliojikita kwenye demokrasia; ni uwazi hasa katika kuendesha mambo ya kaya. Anayetaka asikosolewe asijiingize kwenye utumishi wa umma na aache upumbavu wa kuona wanaomkosoa kuwa maadui au wapumbavu.  Hivi kweli kukosoa ni upumbavu kweli?  Nadhani upumbavu ni kutokubali kukosolewa hasa tukizingatia kuwa ni Mungu pekee asiyekosolewa. Binadamu ana nini cha mno hadi asikosolewa; wakati kila sekunde ipitayo hutenda madhambi na kukosea?
             Natoa tahadhari mapema. Msitake kututia madole mkadhani hatujui madhambi yenu. Nani alijua kuwa waungwana kama Luis Inacio Lula da Silva aliyeifanyia makuu Brazil angeburuzwa kwa pilato? Kama kuchokoana dili, chokochoko kanchokoe pweza; ila si walevi watakatifu na wachapa kazi wanaolisha kila aina ya kupe kayani.
            Kifalsafa, binadamu ni kiumbe dhaifu kuliko hata wanyama; ila amewazidi kwa sababu ya sanaa ya mawasiliano ambayo sasa wengine wanaanza kuitukana kwa kuitumia vibaya kama huyu mlevi mkubwa aliyejivua nguo hadharani na kuonyesha alivyo mbumbumbu wa demokrasia. Muishiwa huyu mkubwa bingwa wa kutukana walevi wapumbavu asijiangalie sana. Tatapinga pale tutakapoona tunaburuzwa kama kutaka tuwasamehe wezi na majambazi wakubwa waliotumia ofisi zetu kujinufaisha; wakati sisi tukimenyeka bila sababu zaidi ya upumbavu na uroho vyao. Mfano mdogo, ni pale kaisari alipotuasa tuwaache mafisadi wakubwa waliotuuza kwa wachukuaji wapumzike wakati walituibia mmojawapo akiwa huyu aliyeonyesha umamuma wake wazi wazi. Go tell it to the birds; lazima wasulubiwe. Pia, waachwe wabebe misalaba yao kama alivyosema mwana wa Adam kuwa kila mtu atauchukua mzigo wake mwenyewe.
            Mjivuni huyu na mvivu wa kufikiri amesahau kuwa tunayajua machafu yake kuanzia unyakuzi hadi uvivu wa kufikiri hadi akazidiwa kete na bi nkubwa aliyemuingiza kwenye umachinga akiwa patakatifu pa patakatifu. Kama upumbavu wetu ni kumvumilia, basi patachimbika bila jembe. Mbona muishiwa huyu hataki kujifunza yaliyojiri hivi karibuni kule kwa walevi wa Korea ya Kusini na Brazil ambapo walaji wakubwa mmoja alihukumiwa miaka tisa na ushei; huku mwingine akinyea debe. Anadhani sisi ni mabunga yasiyobadilika au mawe? Akome na kukomaa.
            Huyu dingi hajui kuwa tunajua anavyotuingiza hasara kwa kulipwa mabilioni ya njuluku wakati alipaswa awe Ukonga akifanyia kule vitu vyake na wenzake kama akina Seti na Rugetumbuliwa; kama siyo akina Hasi Kiti… Hakuna ukumbaff kupita kiasi kama kujisahau; na anayefanya hivyo akadhani wote tumesahau. Tunakumbuka Kiwila, ANbeni, Tanpawa, NBC, Fosiniki EOTf na maulaji mengine mengi aliyoasisi na kutupiga njuluku zetu ukiachia mbali uwekezaji wa kichukuaji na kijambazi. Ni bahati mbaya kushindwa kujua kuwa aliyeko juu mngoje chini au ikizidi mpandie. Hajui kuwa walevi tunaweza kumpandia na akaishia kubwagwa chini bila kutarajia? Bora azibe domo lake chafu kabla hatujamshukia ili apatilizwe na kusulubiwa kwa madhambi yake.
            Buda huyu au dingi, kama wasemavyo manyang’a, bingwa wa kupayuka amesahau kuwa zake zilikwisha zamani kiasi cha kuishi akitegemea kukingiwa kifua na kaisari junior kwake ili tusimfikishe kwa pilato akanyolewa bila maji. Kama amesahau au anajisahaulisha, namshauri asome waraka huu tena aukariri ili akijisahau uwe unamkumbusha kuwa walevi si wakumbaff, hawajawahi kuwa wakumbaff wala hawatakuwa wakumbaff kama yeye. Mijitu mingine bwana kwa kujisahau, yaani jamaa limesahau lilivyomhangaisha mzee wetu Musa kulipigia ndogo ndogo zama za kinyago cha mpapure! Ama kweli ukishangaa ya tumbili utaona ya nyani! Na ama kweli nyani haoni nonihino lake. Nimalizie. Walevi wapingaji si wapumbavu bali upumbavu ni kutokutambua mchango wao na ukweli kuwa kukosoana ni demokrasia na ustaarabu. See you next week guys.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

No comments: