Thursday, 4 November 2010

Hata majina ya marehemu yalikuwapo vituoni

BAADA kumaliza ligi ya uongo na ahadi hewa wa kuusaka uongozi, kuna jambo sikulitarajia ingawa lilitokea. Nikiwa na hamasa ya kuchagua ukombozi na kuuzika upuuzi na ufisadi, siku ya tarehe 31 Oktoba nilidamka kwenda kupiga kura nisijue nitapigwa na butwaa na kuishiwa kuliwa na kubambikiziwa wezi wa kunila zaidi!

Kuna kipindi ukiiangalia hii dunia unaweza kuichukia wakati si mbaya bali walimwengu. Sijui ni wangapi yaliwakuta kama haya yaliyonikuta kaya nzima.

Je, huu nao si mtaji wa kurejesha wachovu ambao wengi wao wanaweza kupeta wakiwamo hata wale mafisadi papa na wanaonuka? Kwa mtu ambaye nguvu zangu na akili zangu zinajipa imekuwa hivi. Je, hao vikongwe na wenye welewa kidogo ilikuwaje?

Siku moja kabla ya kipute chenyewe nilikwenda kwenye kituo changu cha kupigia kura cha kwa Mfuga Mbwa ingawa siku hizi nimehamia Kigogo Mwisho. Nilijilaumu. Kwani licha ya kulipa nauli na kupoteza muda wangu jina langu halikuwapo.

Ajabu majina ya marehemu yalikuwapo yote. Walipiga vipi kura na kumpa nani kula usiniiulize na unajua kilichotokea. Hivi huyu atakayeshinda kwa kutegemea kura za maiti naye atajisifu na kujiona ni kiongozi halali wakati ni haramu?

Baada ya kutokuta jina langu, nilipiga mguu kwenda kwa wakubwa wa uchakachuaji (National Electoral Counterfeiters (NEC) na kuulizia kulikoni hata jina langu silioni.

Majibu waliyotoa hata kuku hawezi kufikiri kuyatoa achia mbali kuyatoa. Ajabu bado wapuuzi hawa wanalipwa njuluku zetu! Yaani tunawalipa waongo kutuongopea na kutuwekea misukule yao!

Hakuna kilichonikera nusu kujinyotoa roho kama kusikia wapuuzi fulani wakijisifu upuuzi eti wamekuza demokrasia wakati wameidumaza na hatimaye kuiua kabisa ukiachia mbali kuidhalilisha.

Demokrasia au ghasia? Mara utawasikia na kuwaona mitaani wakijinyevuavua-'wamechukua wakaweka tukachukua na kuchakachua waa'.

Demokrasia gani watu tunakatwa majina na marehemu wanabakizwa ili kutumiwa kuchakachua na kuula kwa kuiba kura? Demokrasia gani kampeni zinaendeshwa kwa wizi na matumizi ya udugu, ufamilia, udini, usanii, uongo, mamluki, makanjanja na ufisadi?

Hata hamuogopi Mungu ingawa mliwahi kujipachia kuwa chaguo lake msijue ni la mafisadi na shetani mwenyewe? Hivi kuwatumia marehemu si kuwadhalilisha ukiachia mbali kujidhalilisha? Anayewatumia marehemu kufikia malengo yake naye ni marehemu ambaye alipaswa kuzikwa tu.

Bahati mbaya tunatawaliwa na marehemu kisiasa kwa sera zao mfu na mgando, bila kusahau ufisadi wa kunuka! Je, tuendelee na ibada hizi za sanamu?

Leo watu wazima hata kama tu walevi tunaambiwa eti uchumi umekuwa simply because fisadi mkuu na familia yake wanashiba wakati si kweli?

Anayebishia hili aende vijijini aone watu wanavyoishi kwenye mbavu za mbwa huku wezi wachache wakitanua na vimada wao.

Madame Rahma Haruusi Kharous wa Kissie upo japo unajificha kwenye ufadhili wa michezo na kujifanya mtafiti wa mawese wakati tunajua wewe nesi. Du! Ona sasa ulevi ulivyo balaa. Naona nimevuka mipaka. Badala ya kujadili uchakachuaji najadili u hovyo! Hata hivyo nondo imefika na wahusika wameipata hata kama hawatajibu. Wajibu nini wakati nao ni marehemu wa ndoa?

Turudi kwenye uchakachuaji na uchafuzi. Hakuna kinachozidi kunikera kama kuona wezi na majambazi wa ufisadi na kura kujisifu eti wamepata ridhaa yetu.

Ridhaa gani wakati hatukupiga kura? Je kosa letu ni kuwaacha kufanya ufisadi wao hadi kufikia kunadiana hadharani tukiwa mashahidi? Je, walevi wataendelea kuvumilia huu upuuzi hadi lini?

Kana kwamba madhambi na dhuluma walivyowatendea walevi havitoshi, wameongeza na hili la kuiba haki yetu ya kupiga kura kwa kuhofia tungewaangusha.

Je, umma wa walevi utajitendea dhambi ya kujitia kitanzi kwa kusamehe upuuzi huu? Je, huu nao ujanja au kuishiwa? Je watawala wazalishwao na jinai hii waharifu wa kawaida? Je, namna hii walevi hawajatawaliwa na genge la mafia?

Je, tutaendelea na usanii huu wakati tukijua waathirika wakubwa ni sisi hadi lini? Ni swali ambalo kila mlevi anapaswa kujiuliza.

Kwanini tusitumie ulevi wetu unaotuwezesha kuzungumza kiingereza ambacho huwa hatuwezi kabla ya kulewa, kuondoa balaa hili la kujitengenezea? Hakika hii ni kucheza na mauti.

Lazima tukubaliane. Watu wanaoshinda kutegemea misukule, maruhani, marehemu na upuuzi mwingine kama huu nao ni maruhani, misukule, wafu na waharifu wa kawaida wasiopaswa kuwa kwenye ofisi za umma. Je, ni wangapi wanaona hivi ili wawatoe mkuku?

Ndiyo maana kaya yetu inachezewa na wachukuaji na mafisadi. Hii ni kutokana na kuongozwa na marehemu, misukule, maruhani na upuuzi mwingine.

Ruhani aweza kuwa mtu anayetumia familia kama nguvu yake ya kisiasa. Msukule aweza kuwa yeyote anayetegemea nguvu na pesa za mafisadi kupata maulaji ya utawala.

Marehemu aweza kuwa yule anayeendesha kijiwe kwa sera marehemu na mambo mengine kama hayo. Je, hawa na haya hawapo miongoni mwetu? Je ni marehemu gani anaweza kumkomboa aliye hai wakati ameshindwa kujikomboa mwenyewe?

Ni uongo kiasi gani kwa marehemu kuamini atamkomboa aliye hai sawa na aliye hai kuamini atakombolewa na marehemu?

Ama kweli Yesu mwana wa seremala alijua. Alisema waache wafu wazike wafu wenzao. Je, nasi umefika wakati wa kuwaambia tuwaache wafu wawatawale wafu wenzao?

Je, wale ambao si wafu watapata wapi ukombozi? Je wataendelea kujitoa huku mambo yakizidi kuharibika au watachukua hatua mujarabu?

Je, chanzo cha haya yote ni nini kama si watu kuogopa kufa hadi kutawaliwa na marehemu? Heri kufa ukipambana kuliko kuishi kama punda kihongwe bingwa wa kubeba kila mizigo.

Juzi tumewaona marehemu wengi wakiwapigia debe marehemu wenzao. Tumewaona makanjanja na wasomi nepi wakijivua nguo kuhakikisha marehemu wenzao wanapita ili wapete nao. Tumewaona wengi tena ambao ungedhani walikuwa hai kumbe walijifia zamani.

Marehemu hawa wanawauza walio hai kwa vile wao hawana hasara. Wafe mara ngapi? Waweza kuwa hai kimwili lakini ukawa mfu kimaadili. Na hawa ni wengi sina mfano.

Wapo kila mahali kama majani yaliyopukutika. Wapo maofisini, makanisani, misikitini, vyuoni na kwingineko.

Wako vijijini na mijini. Wako nawaona kila mahali. Wamezagaa kama uchafu kwenye mitaa ya Bongo. Ukichanganya na mainzi mafu yaliyowazunguka hicho kinyaa Mungu ajua.

Turejee kwenye uhalisia na ukweli bila kuugopa wala kuupindisha. Hivi mtu anayewanyima haki walio hai akajificha nyuma ya usanii wa kuwatumia maiti hajaishiwa kiasi cha kutostahili hata kuishi kufanya kile anachofanya?

Je, huu si ushahidi kuwa kumbe kaya inaweza ikatawaliwa na waharifu huku walevi wakitegemea waharifu hawa wauondoa uharifu wakati wao ni tunda lake? Je, namna hii kaya kuna siku itafika huko Kanani au Golgotha?

Ngoja nivuke barabara haraka kabla ya mataa kuzima na hawa wehu wa dala dala kuninyotoa roho.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 3, 2010.

No comments: