Friday, 5 November 2010

"Ushindi" wa Kikwete ni mea maxima culpa na aibu

Kibaraka wa Kikwete, Luis Makame mwenyekiti wa Tume ya Uchakachuaji akimkabidhi bosi wake cheti cha kuwaibia urais watanzaniaJapo Jakaya Kikwete, chama chake na waramba viatu wake hasa mafisadi, watajiridhisha kuwa ameshinda kuwa rais wa Tanzania, ni aibu na matusi kwa demokrasia kwa utawala mchovu kurejea madarakani. Ni hatari na balaa. Hatutaki kuwa watabiri. Watanzania ndani ya kipindi kifupi watagundua kosa lao kuvumilia uchakachuaji uliorejesha utawala huu wa kifisadi usio na lolote la kuwafanyia bali kuwaibia.

Tusitoe madai bila ushahidi. Nani alitegemea kuwa watuhumiwa wa ufisadi kama Andrew Chenge, Edward Lowassa,Nimrod Mkono, Rostam Aziz na wengine wangerejea? Nani alitegemea watuhumiwa wa kughushi vyeti vya taaluma kama Emanuel Nchimbi, Makongoro Mahanga, Mary Nagu, Victor Mwambalaswa na wengine wangerejea bungeni? Nani angeamini kuwa mtuhumiwa kama Chenge angediriki hata kugombea ubunge. Ili alitumie kufanya nini zaidi ya kuwalinda na kuwapa ulaji mafisadi wenzake? Haya ndiyo mauzauza ya mfumo mbovu na mchafu wa Tanzania.

Japo watu wengi wakiwamo wasimamizi wa kimataifa wameshauri Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakubali matokeo yaliyochakachauliwa, ni jinai namna gani? Kisingizio na sababu uchwara inayotolewa eti AMANI. Amani gani bila kutenda haki? Amani gani kuwavumilia wezi wa kura na mafisadi? Amani gani ndani ya jinai kila aina na ufisadi ukiachia mbali ukosefu wa visheni na sera bila kusahau uadilifu? Huu ni upuuzi.

Wanaoshangilia ushindi wa CCM wanashangilia ufisadi na maangamizi yao wenyewe ima kwa makusudi au bahati mbaya.
Ushindi wa Kikwete, CCM na waramba viatu wake si chochote wala lolote bali MEA CULPA.
Tungekuwa na watu wanaojali mstakabali wao na taifa, watu kama Kivuitu Kiravu na Luis Makame na Kikwete wao wangetafuta sehemu ya kujificha pale People's power ingeanza kuwasulubu. Natamani watanzania waamke toka kwenye usingizi huu unaowafanya makondoo na kuku. Je ukuku na ukondoo vinalipa. Majirani zetu ambao tulizoea kuwacheka wanatucheka kwa ukondoo wetu.Heri wao tuliwaita mbwa mwitu na mafisi lakini wanatuzidi wamejikomboa ikilinganishwa nasi tulio kwenye kongwa za mafisadi na mabwana zao. Je tutaendelea na kitanzi hiki hadi lini? Tafakarini.

2 comments:

Anonymous said...

Mpayukaj, I salute you my fellow comrade.

"When Good People Dont Take Actions Bad People Rules"

Sisi ni kondoo Mafisadi ni Mbweha, wakati wowote Mbweha wakitaka mmoja wetu anageuzwa mbaniko kwa shibe yao mbweha. Mbweha hawa wakishiba hujilaza vivulini na kustarehe vile wapendavyo. Kibaya kuliko vyote Mbweha hawa wakiwa vivulini wakifaidi matunda ya Uharamia wao kondoo wenzetu hujipendekeza kwao na kujiweka karibu nao huku wakijua wazi kwamba kitendo hicho hakiwapi status ya kuwa mbweha wala hakiwazuii mbweha kuendelea kuwaweka katika kundi la kondoo.
Unyonge wa kutojua kwamba wao ni kondoo na bora zaidi kuliko mbweha wote kwa pamoja ndo uwafanyao kujitia unajisi na kulala pamoja na mweha na hata kujaribu kujiona mbweha.

Aliyewaumba kondoo aliwaumba kondoo wenye pembe na wale wasio na pembe. Muumbaji pia aliwapa vichwa vigumu na uhodari wa kuvitumia kama silaha. Pembe na Vichwa vya kondoo ndiyo mitaji yao.
Wataalamu wa uchumi wanasema ukiwa na ndimu jenga uchumi wa ndimu usiote kujenga uchumi wa dhahabu usokuwa nayo.
kama mbweha wameweza kujenga himaya ya Makucha na meno! Kwa nini sisi kondoo tusijenge Himaya ya Vichwa na Pembe kwani ndo mitaji tuliyo nayoo.
Meno yetu hayajachongoka kama ya mbweha ni wazimu kujaribu kuyatumia kujenga himaya yetu ya kikondoo. Miguu yetu na mikono yetu ni kwato tupu hatuna makucha kama ya mbweha, haita faa kitu kujenga himaya ya makucha. Kuna ubaya gani kutumia pembe zetu dhidi ya mbweha. Himaya ya vichwa na Pembe na kwato na uwingi wetu kondoo ndiyo silaha yetu kubwa.Silaha nyingine kubwa ni milio yetu ya M-ee-ee-ee-ee-ee-eee kila mbweha atupigapo kucha. yaani mwenzetu mmoja akilia mlio wa Mee eeee sisi wote ni lazima tuitike mEEEEEEEEEEEEEEEEEE! kwa pamoja

kuna kondoo wenzetu baada ya kulala kitanda kimoja na mbweha eti wanadai tukubali yaishe kwani mbweha ni mbweha uje mwaka 2015 wataendelea kutesa. Kwa maoni yangu ya kikondoo nasema Bora na Bora ni sawa kabisa na hafifu na hafifu. Bora ni bora kwa sababu hafifu amekubali kuwa hafifu. hafifu akisema sasa basi ubora wa Bora hutoweka.

Kondoo mmoja safi ni Bora kuliko kundi lote mbweha tusisahau hilo daima.

Tumesahau visa vya kondoo waliopambana na Simba wakawashinda kwa Knock out wakawakata shingo zao na kuchuna ngozi zao na kuzifanya mazulia ya kukanyagwa kwa miguu.

Tumesahau historia ya kondoo kama sisi waliojitolea muhanga kupambana hadi kufa ili jamii ya kondoo wote ionje tamu ya uhuru.

Mbweha wanajua uwezo wetu ndiyo maana wanamwaga propaganda kila kona kwamba tuangalie sana maneno tusemayo na vitendo tutendavyo kwani tutapelekea kumwaga damu ya kondoo wengi bure.

Wasicho kisema wazi au kukiweka bayana ni idadi ya kondoo wenzetu walokufa kibudu ili kunenepesha mashavu yao, wake zao, mabinti zao na vimada wao.
Kondoo hana haja ya kuua kondoo mwenzi wake kwa sbabu kondoo hali nyama.
Mbweha wanasabau ya kuua kondoo kwa sababu kuishi kwao kunategemea uwepo wa kondoo. Mbweha ni tegemezi na huo niudhaifu. Uwepo wa kondoo hautegemei uwepo wa mbweha.Kondo si tegemezi.

Kwa akili yangu ya kikondoo naona ni vema nife nikitetea haki yangu ya kikondoo kuliko kusubiri mauti inifike kwa njia ya makucha ya meno ya mbweha, kisha kiwiliwili changu kushibisha matumbo ya jamii ya mbweha.

Si semi eti kwa vile tunahasira basi tunaondoka na mihasira yetu ya kikondoo na kuanza kuwapa kichapo cha pembe mbweha wote.

Ni muhimu kwa kila kondoo kukaa chini na kutafakari uwezo wake kabla haja chukua hatua ya kuwatia adabu mbweha.

Wakatiwote ni vema kutumia kwanza sauti zeti za m-ee-e-eee kabla ya kutumia pembe zetu.

Mbweha ni waoga kweli kweli wa sauti za kijumla za kondoo. Sauti za kondoo wengi pamoja ni sawa na pembe moja kubwa ilochongoka vema ipigayo na kuchoma bila kuchoka.

Mbweha ni waoga sana wa umoja wa kikondoo, ni taabu sana kwao kushughulikia umoja wa kikondoo.

Wanatuona kondoo wanatuita kondoo wamesahau kwamba kondoo wana pembe.

MADELA WA- MADILU

NN Mhango said...

Ndugu MADELA WA-MDILU ujumbe wako ni mzito kwelikweli. Sina cha kuongeza zaidi ya kuusoma zaidi na zaidi lau nami niambue chochote.
Umeandika kwa hisia. Hili ni jambo jema katika uandishi. Kwani humuingiza msafiri kwenye mtumbwi wako na kusafiri naye.
Laiti ungepata nakala ya kitabu changu cha NYUMA YA PAZIA, basi mambo yangenoga. Kwani siku zote najaribu kuandalia makao UKOMBOZI wa kweli wa MTANZANIA. Na hili haliwezekani bila kujitambua na kujikomboa kiakili.
Kila la heri ndugu yangu.