How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

How the Berlin Conference Clung on Africa: What Africa Must Do

Wednesday, 10 November 2010

Uchakachuaji kila pahala, tunapelekwa wapi?

BABA yangu mzee Msemahovyo kumbe alinidanganya! Si alinifundisha kuwa mvumilivu hula mbivu! Maskini hakujua mambo yangebadilika na mvumilivu kuishia kupigwa mibomu ya machozi na kuchakachuliwa kura na kula yake!

Mie nitamfundisha kijogoo wangu Kapayukaji kuwa aliyeko juu mpandie kama ambavyo Silaha atawapandia Nambari chakachua wahedi.

Hivi kaya hii inapelekwa wapi? Mama akienda mwanamanyala kujifungua anachakachuliwa mtoto na kubambikiziwa asiye wake.

Ukienda polisi unachakachuliwa na kubandikiwa kesi za madawa na upuuzi mwingine. Ukienda banki kubwa watu wanachakachua na kutoka na EPA! Tukubaliane. Hii kaya ya Danganyika sasa imeongeza sifa. Ni kaya ya Kuchakachua. Sijui tuiite Chakachua au Fisidika? Mie sijui.

Baada ya kushuhudia kufuru, uonevu, jinai na mazabe mengine ambayo sikutegemea kuona kwenye uhai wangu, nilikaa pembeni na kutafakari nini cha kufanya kuepuka kurudiwa. Nafanya hivi kuepuka kujidanganya kama kaya na wanadamu. Nafanya hivi si kwa kumuudhi wala kumfurahisha yoyote bali Mungu na taifa.

Hii yote inatokana na walevi kupiga kura kwa ufanisi na amani vya hali ya juu lakini uhasama wa taifa wakazichakachua ili kumbeba msukule wao. Simtaji jina. Kwani hata kuku wanamjua. Kama humjui basi utajiju mwenyewe.

Tusipojiangalia vizuri, tutaiweka kaya njia panda na kuitapakaza damu bila sababu. Kwanini uroho wa kikundi kidogo cha waharifu utufikishe huku? Lazima watu wenye akili na udhu kama mimi waonye na kuonyesha njia. Acheni jinai hii Njaa Kaya na wenzako. Mtaipeleka kaya kuzimu kwa tamaa na upogo na upofu wenu.

Kutokana na taaluma yangu ya utafiti na upayukaji, nimegundua kuwa kaya yetu ina matatizo mengi, kubwa likiwa ni waharifu wachache kugombea ulaji hata kwa gharama ya damu ya walevi wasio na hatia.

Watu wako tayari kuwanyotoa wenzao tena wasio na hatia roho ili waendelee kuinyonya na kuinajisi kaya. Wameigeuza kaya mateka wao kiasi cha kudhani bila wao haiwezi kuwepo wala kutawalika. Huu ni upuuzi na kujidanganya vya hali ya juu. Na anayeamini katika jinai hii ya uchakachuaji ameisha na kuishiwa na hatufai hata alazimishe vipi.

Hili halikubariki wala kuvumilika ingawa kuna wapuuzi wanatushauri tuvumilie wakati tunapukutishwa kama majani. Kwanini hawa watanguliza matumbo wasivumilie. Kwanini sisi kuwavumilia watu wasiotumilia kwa miaka yote waliyotuguguna?

Kuondokana na adha ya niliyoshuhudia wakati wa harakati za uchakachuaji ili kuwezesha misukule na marehemu kuwala walevi, nimegundua kanuni rahisi. Japo wanafiki ambao kimsingi ni madikteta na wezi wa kawaida hawapendi waambiwe ukweli kuwa ni waharifu na wanafiki, kuna haja ya kujikaza kisabuni na kutangaza ufalme kwenye kaya yetu ili kuepusha vita ya mibomu na mibunduki niliyoshuhudia.

Nani angeamini kuwa watu tusio na hatia tungepigwa mibomu ya michozi ili kuachia wezi waibe kura zetu? Nani angeamini kuwa walevi wangekatana mapanga na kuchomeana nyumba kutetea haki zao?

Nani angeamini kuwa, kwa upande wa pili, kuna walevi wendawazimu na vyangudoa ambao wangeweka maisha yao hatarini kuwatetea majambazi wa kisiasa kama ilivyotokea kule Musoma, Buzwagi, Shinyanga na kwingineko?

Ajabu na aibu ni ukweli kwamba kuna wenzetu ambao wako tayari kuwaumiza wenzao wakiwatetea mabwana zao wanaowalipa makombo yatokanayo na jinai ya kutusaliti na kutuchuuza!

Nani angeamini kuwa kodi ya walevi ingetumika kununua mibomu ya michozi na kuwalipa wahuni waliotupiga mabomu badala ya kununua madawa na vifaa vya elimu?

Nani angeamini kuwa deni la nje la walevi lingeumka kugharimia upuuzi huu? Halafu wanaotenda jinai hii bado wanajiaminisha na kutuaminisha kuwa wanafaa kututawala! Thubutu! Hatukubali kutawaliwa na wezi na wachakachuaji hata watutishe vipi. Hapa ndipo tunapopaswa kumuunga mkono shujaa Silaha aliyeamua kuwekea ngumu jinai hii hadi kieleweke.

Kama tutashindwa kusimama na kuondosha jinai hii na genge hili basi tufanye jambo moja kieleweke. Kuondokana na hili japo ni aibu, nashauri: tutangaze ufalme ambapo mfalme Njaa Kaya na malkia zake wa uharibifu kina Shari Salima na Rahma Kasigasiga wawe malkia.

Njaa mwenyewe aende kwa shoga yake Mswati kujifunza jinsi ya kutawala kifalme badala ya kutegemea mafisadi na majambazi waitwao uhasama wa taifa.

Mambo hayaishii hapa. Lazima mwana wa mfalme Riziki Njaa Kaya awe mwana mrithi wa mfalme. Mambo namna hii yatanoga na kuepusha hujuma za kipuuzi kwa watu wasio na hatia.

Ingawa sipendi wafalme kutokana na kuwa madikteta na wanyonyaji wa kawaida wasio na lolote la maana zaidi ya kujikweza na kuvuna wasipopanda, kwa hali iliyojitokeza sina namna. Badala ya kuwa na rahisi aliyezalishwa na uchakachuaji wa kina Kivuitu Kiravuuu na Louis wa Ukame, heri tuwe na mfalme na washauri wake kina Ewassa, Endelea Chenga na wengine.

Najua wasomaji wangu wengi watashangaa kwanini shujaa na jabali kama mimi nabwaga manyanga. Sijabwaga manyanga.

Naona huruma jinsi walevi wanavyoteswa. Nawatukana kwa kutaka tuwe na mfalme ili wachukie na kukataa na kusimama na kupata haki kwa njia ya kidemokrasia.

Baada ya wahusika kukataa zoezi la uchaguzi basi tutumie lile kali la migomo na maandamano tuone kama hawatang'oka na tukawa huru. Tena nataka hapa nieleweke. Sifanyi uchochezi.

Wanaofanya uchochezi ni wale wanaotuchokoza kwa kufanya uchakachuzi na matumizi ya maguvu tena kwa vyombo vyetu vya umma wa walevi.

Najua fika kuwa kuwa na mfalme ni matusi ingawa tulishatukanwa sana tusi hili kwa kisingizio cha uchaguzi. Nani hajui kuwa walevi, kwa miaka mitano iliyopita, walitawaliwa na ufalme wa familia fulani iliyojificha nyuma ya chama?

Nani hajui kuwa kwa sasa mkuu wa kaya hajulikani kati ya mwanae yeye na mkewe ukiachia mbali wafadhili wake ambao ni mafisi na mafisadi?

Nani hajui hili nimjuze vilivyo? Nani anabishia hili aje na hoja za kupiga na si mizengwe ya kutishia waandika magazeti ilhali wao waliwatumia wale wale kuwachafua wenzao japo hili halikufua dafu?

Nani hajui kuwa tuna watu wachafu patakatifu pa patakatifu wakifanya kila aina ya uchafu? Nani hajui kuwa hawa wezi waliingia huko kwa pesa ya HEPA na Richmonduli? Nani hajui kuwa hawana lolote zaidi ya ajenda ya siri ya kutufanya shamba la bibi kwa ajili yao na vimada wao?

Ni upuuzi watu wazima kufanya mambo ya kitoto. Ngoja niondoke hapa karibu na ofisi ya kuhesabia kura wasijenipiga mibomu mingine.
Chanzo: Tanzania Daima Novemba 10, 2010.

No comments: