Monday, 8 November 2010

Uchakachuaji, amani gani inaletwa na dhuluma?
Watanzania tuna tabia ya kujisifia upuuzi hasa watawala wetu. Huwa tunaona fahari hata kusifiana upuuzi na ujinga. Utamsikia mtu akisema Tanzania ni nchi ya amani wakati haina haki! Hivi amani inaweza kuwapo wapi bila kuwapo haki?

Hali hii imejitokeza baada ya watanzania kujihimu na kupiga kura kwa wingi ingawa ziliishia kuchakachuliwa kiasi cha kupachikiwa washindi ambao kimsingi walishindwa.

Hakuna kitu kilinifurahisha na baadaye kunisikitisha kama jinsi uchaguzi (uchakachuaji) ulivyoendeshwa na hatimaye kuharibika.

Kwa aliyefuatilia, siku ya kwanza ya uchaguzi, licha ya kuanza kwa vituko hapa na pale na wapiga kura na umma kuvivumilia, angalau wananchi walipiga kura kwa amani. Uchaguzi ulionekana kuwa uchaguzi kiasi cha kutia moyo. Lakini baada ya tume ya uchaguzi kuanza mizengwe na uchakachuaji, maana nzima ya uchaguzi ilikufa hapo hapo na kuzaliwa dhana chafu ya uchafuzi na uchakachuaji. Baada ya hapo, usalama wa taifa kama inavyodaiwa, wachakachuaji wenyewe wanaotaka kurejeshwa madarakani wameuharibu uchaguzi kiasi cha kuwa vurugu ujuha na jinai nyingine.

Hii imepelekea chama kikuu cha upinzani Chadema kusema wazi kuwa hakitatambua matokeo ya kupikwa na watawala wa kupachikwa na kundi la wasaka ngawira na wateule wa yule yule anayebebwa bila hata chembe ya aibu na kujali mstakabali wa taifa.

Tumekuwa tukionyana kuepuka yaliyojiri nchi jirani kama Burundi Kenya hata Rwanda bila kujingalia vizuri tabia na mienendo yetu! Ni unafiki kiasi gani?

Sikutegemea mtu ambaye aliingia madarakani akiitwa chaguo la Mungu, kugeuka ghafla na kuwa chaguo la wachakachuaji na mafisadi. Sisemi haya kumkejeli mgombea wa CCM Jakaya Mrisho Kikwete. Nina sababu nuzuhu.

Kwanza, ukiangalia hata namna alivyofanya kampeni kwa kutegemea mke na mtoto wake na genge lenye kutia shaka hasa pesa iliyomwagwa bila kuelezwa ilikotoka, inatosha kukuonyesha ni kiasi gani maji yalishazidi unga. Ukirejea nyuma kutathmini aliyofanya angalau nusu ya aliyoahidi, huoni kitu. Ukiangalia namna kampeni zake za kutumia magazeti nyemelezi na wachumia tumbo kuwachafua wenzake, unagundua ni kwanini madai kuwa ameiba kura yana mashiko tu.

Pili, ukiangalia ahadi za wazi za uongo alizotoa tena lukuki unajua fika kuwa jamaa alikuwa akitafuta kupata ngwe ya pili ikulu kwa kila namna bila kujali kama alichokuwa akifanya kinawezekana.

Tatu, ukiangalia chama chake kinavyozidi kuunga mkono kila upuuzi wa tume ya uchaguzi, unagundua fika jinsi ambavyo wako nyuma ya kila kinachofanyika kiasi cha kushindwa kuelewa nani mwenye mamlaka nchini kati ya chama na tume ya uchaguzi.

Na hata ukiangalia matamko na uendeshaji wa nchi, hutashindwa kumaizi kuwa CCM ina nguvu na ushawishi kuliko serikali. Reja CCM kuamrisha benki kuu kuruhusu ujambazi wa EPA ambao kama ambavyo imekuwa ikidaiwa bila kukanushwa ni mtaji uliomwingiza madarakani Kikwete anayetuhumiwa kuvuruga uchaguzi na kuiba kura na chama chake kisikanushe.

Inashangaza kusikia watawala wa CCM na hata washirika zao toka Ulaya wakiwahimiza watanzania kukubali matokeo yaliyochakachuliwa eti kwa kisingizio cha kulinda amani na mshikamano wa taifa. Kwani mwenye dhamana ya kuwezesha kuwepo amani ni wananchi na wapinzani tu? Kwanini CCM waibie watu wasiogope amani itatoweka? Na ni wapi kunaweza kuwapo amani ya kweli bila kutenda haki?

Anayelitakia amani taifa hili ni yule atakayetenda haki. Na kutenda haki katika uchaguzi ni nguzo ya amani na mshiamano lakini si kuwavumilia waharifu fulani waendelee kufanya uharifu. Kinyume cha hili wa kulaumiwa ni hawa hawa wanaolalamikiwa ambao wanaweza kutumia raslimali za taifa ukiachia mbali kuiba ili waweze kuendelea kuwa madarakani. Huku ni kuishiwa kwa kila hali na watu wa namna hii hawafai kukaa madarakani hata kwa nukta moja?

Rais atokanaye na wizi wa kura ni mwizi na fisadi wa kawaida tu na atakapokuwa madarakani atawajali na kuwatumikia waliomwezesha kuchakachua na si wananchi waliomnyima kura hadi akategemea uchakachuaji. Hivyo,

kumruhusu mtu wa namna hii ainajisi nchi kwa miaka mitano ni upumbavu ambao hata kuku hawezi kufanya. Katiba yetu inasisitiza haki. Maadili yetu yanatufundisha kuifia haki. Sasa ni wakati wa kuyaweka haya kwenye matendo ili liwe somo kwa dunia.

Hivi inaleta picha gani kusema eti wapinzani wapokee matokeo hata kama wanachoambiwa wapokee ni matusi kwao na hujuma kwa taifa? Je kwanini wananchi walipoteza muda wao kwenda kupiga kura ilhali matokeo yalishajulikana? Kweli kulikuwa na haja ya kupoteza pesa na muda kwenda kupiga kura ambazo zisingezingatiwa na uamuzi kuzitegemea? Tujalie wapinzani wajifanye mabwege wakubali kuibiwa na kupokea matokeo ya kupikwa. Je hii haiwezi kumaanisha kuwa wapinzani ni wapuuzi, mataahira, waongo na matusi mengine kama hayo? Kwanini wakubali kuibiwa kirahisi hivi na mchana kweupe tena haki yao ya kikatiba? Je huku si kuwachokoza na kuwaangusha watanzania? Kwanini watu, hasa hawa wanaojitia kuwa wafadhili na wasimamizi wetu, hawataki kusikiliza madai ya upande wa pili? Je wanataka kutupandikizia rais kama walivyotupandikizia magavana wakati wa ukoloni? Watanzania tusikubali kudanganywa wala kutishiwa nyau. Maana hii nchi ni yetu sote kwa sawa. Kwanini amani yetu itegemee woga badala ya misingi yake?

Inshangaza kuona uchaguzi unaharibiwa nasi tunashauriwa tukae kimya na kubariki wizi na uchakachuaji! Anayetushauri hivi hatutakii mema hata kidogo. Hata hivyo ulitegemea nini kampeni kusimamiwa na watu wenye rekodi chafu za uovu ambao hata ndege anaujua?

Nani alitegemea wapiga kura wa Tanzania wawe majuha kuchagua mtu aliyebariki wizi wa EPA. Bila aibu hata kuchelea kuwa wanachosema kina walakini, wanatushauri tukubali kuingizwa mkenge kwa mara ya pili! Nani anatulazimisha kuwachagua watu wanaowastahi wezi wa EPA ambao waliitikia wito wa rais wa kurejesha fedha hizo kabla ya Novemba 31 mwaka juzi.

Je serikali ambayo, kimsingi, ni Kikwete aliyewahi kusema eti aliwashauri wezi wa EPA warejeshe pesa ya wizi, ilifanya hivyo kama nani na kwa msingi gani kama siyo kulea na kuficha ufisadi wanakosema wapinzani? Hili ndilo watanzania walipinga kupitia sanduku la kura.

Mambo yaliyowaudhi wananchi hadi wakatoa adhabu ni mengi. Walizingatia yafuatayo na kuyatolea majibu kwa kutoichagua CCM.

Hawakusahau maneno ya rais aliyemaliza muda wake. Rais aliwaambia warejeshe pesa kama nani wakati kazi hii ni ya mahakama kama yeye si mshiriki na mnufaika wa wizi wa EPA-kama wanavyodai wapinzani? Je kwa kufanya hivyo, licha ya kuvunja katiba na sheria, rais hakusaidia mafisadi kuendelea kuiba wakijua hakuna wa kuwagusa-kwani, ama wapo juu ya sheria au kuna mtu wao aliye juu ya sheria wa kuwalinda kwa sababu azijuazo? Je huu si ushahidi tosha kuwa Kikwete hajapambana na ufisadi kama anavyojidai?

Kwanini rais aingilie mamlaka na uhuru wa mahakama huku akipindisha na kuvunja sheria kama hakuwa na maslahi au kuwa mhusika kamili? Je huu si ushahidi tosha kuwa rais na chama chake hawafai na hawako pale kwa manufaa ya umma bali ya mafisadi wanaowakingia kifua? Je kwa ushahidi huu wa mazingira haitoshi kusema kuwa Kikwete hafai na amewaangusha wananchi vibaya? Je mtu akisema Kikwete Toka anamkosea adabu au kumuonea? Kikwete toka hii inatosha. Na tuseme tena kwa kupaza sauti sana.

Kuthibitisha ushiriki na unufaika wake, licha ya kuvunja sheria, rais alificha hata majina ya hao mafisadi na wezi waliorudisha hiyo pesa. Kwanini na anaogopa nini? Je mtu au wapinzani wakisema kuwa rais aliamua kuwaokoa watuhumiwa kwa vile ni washirika na wawezeshaji wake atakuwa anadanganya? Kama kusema hivyo ni uongo, ukweli ni upi zaidi ya huu?

Kama rais wetu na serikali yetu wamegeuka mabwana na mabibi huruma, mbona hatuioni hiyo huruma kwa vibaka tena wa kutengenezwa na serikali yenyewe iliyomo kwenye kitanda kimoja na mafisadi?

Nani angemchagua rais kama huyu ambaye hata aliogopa kushiriki midahalo ukiachia mbali kutofanya lolote la maana kwa miaka mitano? Hawa wanaotwambia tukubali matokeo bila kuzingatia haya ni maajenti wa maafa ya taifa.

Hata kama CCM 'imeshinda' uchaguzi huu kama mazingira yanavyotengenezwa, haitakaa iwe salama zaidi ya kuwa kongwa na aibu kwa taifa. CCM haiwezi kupitisha watuhumiwa wote wa list of shame kugombea urais na ubunge ikawa salama. Hebu watetezi wa uchakachuaji huu watueleze. Watuhumiwa wa list of shame waliotajwa wazi wazi wako wapi zaidi ya kuendelea kuhifadhiwa na CCM na serikali yake? Je kwa kuendelea kuwahifadhi na kuwapitisha kugombea na hatimaye kuwawezesha kushinda ili kuongoza nchi yetu siyo ukweli kuwa CCM inaongozwa na list of shame? Ziko wapi kesi zilizotishiwa kufunguliwa na watuhumiwa akiwamo rais Kikwete ambaye aliamua kukaa kimya? Je huu nao ni uongo na lugha ya matusi? Je vitu hivi havitoshi kuvuruga amani?

Kuna haja ya kuacha kuogopana na kuongopeana. Tuwaeleze wahusika (watuhumiwa) waache urushi, visingizi, utoto na uhuni. Waeleze wanachojua kuhusu tuhuma zinazowakabili. Kutokuwa tayari kueleza haya ndiyo uongo wa mwaka unaofanywa na CCM ambayo, siku zote, imewachukulia watanzania kama mataahira, majuha na shamba la bibi la kufanyia madili yao ili kuendelea kuwa madarakani ingawa siku zao zinazidi kuhesabika.

Kama CCM inakanusha kuwa haikutumia pesa ya wizi wa EPA kuingia madarakani mwaka 2005, mbona haijawahi kueleza vyanzo vya pesa yake iliyotumika kununulia madaraka? Kwanini kila wakitajwa wawezeshaji wa wizi huu mfano Kagoda CCM na serikali hupata kigugumizi kama hakuna ukweli?

Hata hivyo, akiwa Morogoro, mgombea urais wa Chadema, Wibrod Slaa alimshukia Mwenyekiti wa kampeni za CCM, Abdulrahaman Kinana ambaye amekuwa mstari wa mbele kutuaminisha CCM itashinda kwa haki, akimtaka aleze jinsi alivyo na mkono mchafu kwenye biashara ya makampuni ya meli. Inaonekana Slaa alikuwa akimbipu ili kumvutia pumzi na kuona atakavyojitetea badala ya kupoteza muda kupaka rangi upepo kwa kuwaandama wapinzani wakati anayepaswa kuandamwa ni yeye.

Tumalizie kuwataka wasomaji wajiulize swali moja kuu. Kwanini tukubali matokeo tusiyoridhika nayo na ambayo hayatokani na utashi wetu kikatiba? Pia Kinana aulizwe. Ni kwanini Kinana anapata muda wa kuwatetea wenzake kabla ya kujitetea mwenyewe? Je anafanya hivyo ili kufaidi ulinzi wao kama rais mstaafu Benjamin Mkapa?

Kwa waangalizi wa kimataifa wanaotushauri upuuzi, waambiwe waache. Maana mwenye stahiki ya kuamua hatima ya Tanzania ni watanzania wenyewe na si watawala na mawakala wao wala wageni.

Chanzo: Gazeti la Dira ya Mtanzania Novemba 8, 2010

2 comments:

emu-three said...

Duuuh! Hiyo nayo, lakini mmmmmmh, ngoja nifikiri kidogo, sasa wewe unasema tusikubali matokeo...mmmh, katiba inasemaje? manake yamehstangazwa na `tume' iliyokubalika `kikatiba' tufanyeje...mmmh, mimi sielwei hapa, hebu tusaidie `mhariri'

NN Mhango said...

Emu 3,
Asante kunitembelea na kuacha duku duku lako.
Nitakujibu kama ifuatavyo japo kwa ufupi:
Katiba haina nguvu kuliko wananchi. Kama wananchi hawakubaliani na matokeo bado wanaweza kuyakataa. Kenya hali ilikuwa kama kwetu na watu waliyakataa matokeo na matokeo yake ni kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo imewezesha kupatikana kwa katiba mpya.
Kimsingi katiba zote za nchi za kiafrika zina clause hii ya kusema kuwa matokeo yakishatangazwa hakuna awezaye kuyapinga. Walisahau kuwa umma wenye katiba na nchi unaweza kuyapinga kama ilivyotokea Zimbabwe ukiachia mbali Kenya.