Monday, 29 November 2010

Je Kikwete ameamua kufa na watu wake?
Baada ya minong'ono, umbea na kila aina ya bunia hatimaye rais Jakaya Kikwete ameunda serikali yake. Amefanya kitu ambacho wengi hawakutegemea. Pamoja na kulalamikiwa kwa muda mrefu kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri, amelipanua. Haijulikani kama hii inatokana na kiburi, kulipa fadhila au mahitaji ya wakati.

Wengi wanaona kama hapakuwa na sababu ya kupanua baraza la mawaziri sambamba na kuanzisha mikoa na wiliya nyingine mpya. Maana kufanya hivi kunazidisha zigo kwa walipa kodi wetu maskini. Bahati mbaya si rais wala washauri wake walioliona hili kutokana na ukweli kuwa hata kila kijiji kingekuwa mkoa wao bado wanapata marupurupu yao. Rejea pesa nyingi ya bajeti kuishia kwenye kuendesha serikali kubwa isiyo na ulazima badala ya kutumika kwenye shughuli za jamii na maendeleo.

Leo tunathamini nafasi za kisiasa kuliko hata elimu afya na ustawi wa watu wetu? Je hawa ni watu wetu kweli?

Kimsingi upanuzi wa serikali na mikoa haulengi kuwanufaisha wananchi zaidi ya wale walio karibu na bwana mkubwa ambaye amejenga mazingira ambapo karibu kila mtu anajipendekeza kwake ili akumbukwe kwenye karamu hii ya kuuangamiza umma.

Ukiangalia baadhi ya wateule wa rais unashangaa mantiki ya kuwateua hata kama ana mamlaka kikatiba. Ni juzi juzi aliukatisha umma wa watanzania kiasi cha kutaka kumuadhibu kwa kumnyima kura kabla ya kuokolewa na tume yake ya uchaguzi. Aliushangaza na kuuchokoza umma alipowapigia kampeni watuhumiwa wa ufisadi ulioliingizia taifa hasara kubwa sana.

Kana kwamba hii haitoshi, juzi amewateua baadhi ya watuhumiwa wa kughushi vyeti vya kitaaluma pamoja na umma kupigia hili kelele. Hii maana yake ni kwamba rais anatoa taarifa kuwa kwake kutenda ufisadi si tatizo pale autendaye anapokuwa mtu wake.

Hivi inaleta picha gani kwa rais kuteua watu kama Mary Nagu, Makongoro Mahanga, William Lukuvi,Emanuel Nchimbi ambao hawajawahi kujisafisha kutokana na kashfa ya kughushi vyeti vya taaluma? Je hii si kuhalalisha kosa la kughushi hasa linapotendwa na watu wa karibu yake? Je hii haipingani na utawala bora na wa sheria?

Kwa kuangalia jinsi rais alivyoendelea kuwabeba watu wake, ni dhahiri kuwa Kikwete ameamua kufa nao liwalo na liwe.

Kwa upande mwingine rais ametumia udhaifu wa watu wetu wasioshinikiza kufanyika kitu kuendelea kuwalinda watuhumiwa ambao kama kungekuwa na utawala wa sheria, walipaswa kuwajibishwa katika ngwe iliyopita. Lakini nani atamwajibisha nani iwapo rais naye alitajwa kwenye list of shame na hakukanusha wala kutoa maelezo na anaendelea kudunda baada ya kushinda kwenye uchaguzi wenye kila aina ya utata na hakuna anayeingia mitaani kumpinga?

Je umma utaendelea kuwa mashahidi wa mateso na kudhulumiwa na kikundi kidogo cha watu hadi lini? Je kwanini hatumbani rais akatupa sababu za kuwabeba watu wenye tuhuma nzito za jinai? Je rais wa namna hii licha ya kupatikana kwa utata yuko ofisini kwa ajili yetu au watu wake?

Ingawa rais Kikwete hupenda kujionyesha kama mtu msikivu, rahimu na aliye karibu na watu, matendo yake yanamwonyesha kama mbabe na asiyejali umma unasema nini ukiachia mbali kuwa mugumu wa kujifunza na kubadilika.

Je rais kuendelea kuwateua watu wenye madoa, anaandaa mazingira, huko tuendako, kuwarejesha na wengine walio karibu naye kwenye uteuzi ili waweze kuendelea na harakati zao za kuwania ukuu baadaye? Maana ukiangalia umma unavyoendelea kunyamazia jinai hii ya kuteua watuhumiwa wa kashfa za jinai, unagundua kuwa kama rais ataamua kuwarejesha marafiki zake waliotimuliwa kutokana na ufisadi na rushwa, umma utaendelea kulalamika bila kuchukua hatua.

Japo hili laweza kuonekana kama uvumi na hofu tu, kama rais ataruhusiwa kuendelea na ubabe na kiburi hiki, tusishangae wale tuliokwisha wasahau wakafufuliwa na kurejeshwa kwa hadhira na hata baadaye kututawala.

Ukiachana na watuhumiwa wa kashfa ya kughushi, rais amewarejesha baadhi ya mawaziri walioonyesha kushindwa kwenye awamu iliyopita. Kwa mfano, mawaziri Jumanne Maghembe, Shukuru Kawambwa, Hussein Mwinyi, Hawa Ghasia, George Mkuchika, Mathias Chikawe, Benard Membe na William Ngeleja waliboronga.

Maghembe alivuruga kiwango cha elimu huku Kawambwa akipwaya kwenye wizara ya Uchukuzi. Mwinyi atakumbukwa kama waziri wa ulinzi aliyekataa kujiuzulu baada ya kutokea uzembe wizarani mwake na kusababisha milipuko ya mabomu huko Mbagala ambapo raia wasio na hatia waliuawa.

Ghasia , Mkuchika na Membe walipoteza muda mwingi kwenye malumbano ya kisiasa badala ya kufanya kazi huku Ngeleja akiendesha wizara iliyojaza manung'uniko tokana na mgao wa na kupanda kwa gharama za umeme. Orodha haiwezi kukamilika bila kumtaja Sophia Simba bingwa wa kuvuruga utawala bora.

Kwanini rais hakuyaona haya mapungufu? Hakuyaona kwa vile hawa watu walionyesha utii kwake badala ya umma. Hapa ndipo dhana nzima ya rais Mungu-mtu au sultani wa kiswahili inapochimbuka.

Kimsingi, watajwa hapo juu wanaendelea kuwa mzigo kwa bosi wao. Na inaonekana Kikwete ameamua kwa hiari yake na sababu azijuzo kufa na watu wake. Je ana faida gani nao? Jiulize na kutafakari. Je tutaendelea kumruhusu ajifanyie atakavyo kwa gharama ya kodi na ofisi zetu? Ni kutafakari zaidi.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Novemba 28, 2010.

No comments: