Wednesday, 1 December 2010

Kumbe CCM iliingia kwenye uchaguzi na matokeo!


HAKUNA shaka kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kilishiriki uchaguzi kikiwa na matokeo.

Kilishaandaa uchakachuaji baada ya Watanzania kutohongeka kwa ahadi na upuuzi mwingine. Kilishajua walivyokichoka kiasi cha kutegemea nguvu ya ziada ambayo nayo haitasaidia kama umma utaendelea kusimama imara.

Na kama si kuogopa kufikishwa The Hague kwenye mahakama ya kimataifa ya jinai (ICC), kwa kichwa ngumu na ukatili wa watawala na polisi wetu, tungeshuhudia makubwa kuliko haya tuliyoshuhudia. Kura zingeibiwa sana ukiachia mbali watu wengi kuuawa au kujeruhiwa. Maana tamaa ya mali ya watawala wa sasa na genge lao inajulikana fika.

Nani alijua kuwa nyasi zingeangusha vigogo? Wako wapi kina Lawrence Masha aliyekuwa amekaririwa akijisifu kupita bila kupingwa asijue atapigwa chini? Wako wapi kina Basil Mramba, Monica Mbega, Diodorous Kamala, Nazir Karamagi, Batilda Burian, bila kuwasahau kina John Malecela na vigogo wengine wenye nafasi zao?

Kushindwa kwa CCM kulianzia ndani mwake kwenye zoezi la kuchagua wagombea wake pale rushwa na vitisho viliposhindwa kufua dafu ingawa vilitawala matokeo.

Bahati mbaya CCM ilizidi kujipa moyo ikitegemea majimbo yake makuu ya ushindi, yaani Tume ya Uchaguzi, Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na makuadi wengine waliopenyezwa kwenye zoezi zima la uchaguzi lililoishia kuwa uchakachuaji na wizi wa kutia aibu.

Nani alitegemea CCM yenye wagombea wengi wenye tuhuma za ufisadi na kughushi kushindwa? Nani alitegemea Kikwete kushinda kwa kutoa ahadi zaidi za uongo ilhali hajawahi kutekeleza hata moja?

Nani angebariki siasa na sera za ubadhirifu, utapanyaji, kujuana, udugu, ukosefu wa sera na dira na vitu kama hivyo? Nani angebariki rushwa na mawazo mgando yaendelee kututawala ilhali kulikuwa na mbadala yaani CHADEMA?

Umma si haba umeota onyo na tangazo kuwa umechoka na upuuzi wa kurudia kuchagua watu wasio na sifa wala uwezo wa kuongoza bali kuiba.

Tunaambiwa imepoteza majimbo kama 50 pamoja na kutokea wizi wa kura wa kutisha. Je, haki ingetendeka zaidi ya kubaki kwenye vitabu vya historia chafu, CCM ingekuwa wapi?

Kuna watu waliishajibinafsishia ubunge hata uwaziri. Walishajiona kama wao ni kila kitu na bila wao nchi haiwezi kutawalika. Nani angeamini kuwa watuhumiwa wakuu wa ufisadi wangeruhusiwa na chama kinachojinakidi kuleta ukombozi kusimama kwenye uchaguzi?

Pamoja na wengine kupigwa panga la umma, wengi wamerejeshwa na uchakachuaji. Ni aibu na hasara kwa taifa. Ni mwanzo wa kiama chake kama hatutaanzisha kiama chao.

Nani aliamini kuwa mgombea wa CCM rais aliyemaliza muda wake angesimama bega kwa bega kuwashawishi wananchi waathirika wa ufisadi wawachague mafisadi? Pamoja na kutajwa kwenye list of shame na kuuchuna, kwa kusimama na mafisadi naye amejidhihirisha alivyo mmoja wao.

Kuna kitu kimoja ni wazi na kinafurahisha. Kama CCM itaridhiwa itawale kwa ushindi wa kuchakachua, ijue fika 2015 kitakuwa kiama chake taka usitake.

Na kwa mtaji wa watu wachafu walioshinda kutegemea jinai, CCM haitabadilika wala kujirekebisha. Imeishachafuka kiasi cha kutosafishika.

Ingawa wakubwa wetu wamepoteza macho na masikio hasa kuiona haki na kusoma alama za nyakati, tunahitaji kuvunjilia mbali tume ya uchakachuaji na kuliweka chini ya uangalizi jeshi bovu la polisi. Maana wamethibitisha wasivyo pale kututumikia bali kutumiwa na kundi dogo la waharifu.

Ingawa baadhi ya waangalizi wa kitaifa waliusifia uchaguzi kutokana na kudanganywa na utulivu wa siku ya kwanza, uchaguzi haukuwa huru.

Rejea vitisho kabla ya uchaguzi ukiachia mbali uchakachuaji uliofanyika baada ya zoezi zima la uchaguzi. Rejea kucheleweshwa matokeo bila sababu zaidi ya kuyapika na kuwapitisha wateule wa CCM.

Wananchi kimsingi walifanya uchaguzi wa amani tume ya uchaguzi ikawaletea fujo kupitia uchakachuaji na ucheleweshaji matokeo ili kuchakachua kama tulivyoona. Baya zaidi, kama alivyodai mgombea urais wa CHADEMA, Willibrod Slaa, wanaofanya hivi ni Usalama wa Taifa.

Hawa kama tungekuwa na uongozi hata utawala adilifu walipaswa walinde demokrasia na siyo kuwa maajenti wa ufisadi na uchakachuaji. Hawa si usalama wa taifa bala uhasama na zahama na aibu ya taifa.

Kilichotokea baada ya uchaguzi, yaani uchakachuaji wenye kila baraka za CCM, unabadili maana ya jina lake na kuwa chama cha machakachuzi.

Inatisha na kukatisha tamaa. Watawala wanaotokana na uchakachuaji na si ridhaa ya wananchi hawafai na ni waharifu tu. Uchakachuaji licha ya kuwa uhuni ni jinai na utalipeleka pabya taifa.

Licha ya kuilaani jinai hii, tunapaswa kuipiga vita kwa gharama zozote. Tusitishwe na kudanganywa na amani mawenge ambayo hutegemea ukondoo na si utendaji haki. Hatuwezi kuishi kama taifa la kondoo tukafika ilhali tukitawaliwa na fisi na mbwa mwitu.

Kuna haja ya kusimamia haki zetu kwa namna yoyote bila kutishwa wala kudanganywa. Tusiogope mabomu. Watatupiga mabomu lakini si risasi. Nani anataka kwenda kunyea debe The Hague? Na bila ya The Hague vurugu tulizoshuhudia zingeondoka na watu kwa kifo cha risasi za moto.

Hii ndiyo siri ya mafanikio yetu. Na ndiyo maana Slaa kugomea matokeo hajachelewa wala kupoteza. Alluta continua na Mungu ibariki nguvu ya umma dhidi ya nguvu ya mafisadi.

Chanzo: Tanzania Daima Nov. 30, 2010.

No comments: