The Chant of Savant

Wednesday 15 December 2010

Hujuma kwa TANESCO ni ukombozi?



WATANZANIA, tofauti na mataifa mengine, tunasifika kwa ujinga ambao watawala huuita upole na kuthamini amani. Watawala huutumia ukondoo huu kujifanyia wanavyotaka kubwa likiwa ni kushiriki kutuibia bila kuchelea lolote. Jingine ni kutumia vibaya muda na pesa yetu bila kuchelea lolote pia.

Wanakwenda mbali hadi kufikia hata kuchakachua kura zetu nasi tusifurukute. Si umma wala upinzani. Nani hajui kuwa matokeo ya uchaguzi uliopita yalipikwa na Tume ya Uchaguzi ikisaidiana na Usalama wa Taifa kama walivyodai CHADEMA.

Serikali haikukanusha. Hii maana yake ni kwamba madai haya ni ya kweli tupu.

Baada ya uchaguzi kuchakachuliwa na kura kuibiwa, wengi walidhani lau watanzania wangeamka na kudai haki yao yaani uamuzi wao kikatiba kuheshimika. Hawakufanya hivyo! Na pale walipotaka kufanya hivyo, wanasiasa waliwashauri vinginevyo kwa kisingizio cha kulinda amani. Amani gani katikati ya dhuluma ya wazi?

Kabla ya muda kupita, ilifumka kashfa nyingine yaani Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kuamriwa kulipa shilingi 185,000,000,000 kwa kampuni iliyoingia nchini kwa utata mtupu ya Dowans ambayo ni mtoto wa kampuni nyingine tapeli iliyotimuliwa ya Richmond LLC.

Wengi walidhani, kipindi hiki, Watanzania lau wangetoka kwenye lepe lao la usingizi. Kadri mambo yanavyokwenda, hawataamka zaidi ya kuendelea na ‘business as usual’ ya kulalamika bila kuchukua hatua.

Hata hivyo, kuna mabaya yanayoweza kuwa na mema. Kuoza ni kitu kibaya. Lakini bila mbegu kuoza haiwezi kuota na kuchipua. Bila tofali kuchomwa haliwezi kuwa imara. Tunadhani sasa watanzania wataanza kuonja joto ya jiwe la ufisadi wa kimfumo kiasi cha kuanza kufikiri kuamka.

Kwa msingi huo, ni imani yetu kuwa kama wizi huu wa kimfumo utaendelea kubarikiwa na kuendekezwa na kufanikiwa, maumivu yake yatawagusa wananchi kiasi cha kuondokana na usingizi wa pono. Hivyo basi, wanaolitakia taifa hili mema, waombe hawa mafisadi lindwa na shawishi walipwe hadi TANESCO ifilisike na kushindwa kutoa umeme tuona kama watanzania wataweza kuendelea kuvumia kuishi kizani kama mende.

Bahati mbaya sana, watawala wetu walishajenga imani sugu kuwa watanzania hawawezi kuamka kutokana na kushinda jaribio la kuwalazimisha kuishi kizani kwa mwaka na wasichukue hatua. Je watanzania wataendelea kulala wakati mabalaa yanaongezeka? Hili ni swali gumu kujibu.

Kitu kingine kinachosikitisha ni ukweli kuwa, kama alivyosema Spika wa zamani wa Bunge Samuel Sitta, wezi hawa wanatafuta mitaji ya kisiasa. Hii maana yake ni kwamba walioko nyuma ya hujuma hizi wanataka kupata pesa ya kutuhongea sisi wale wale ili waendelee kutula.

Je, tutaendelea kuwa mataahira na panya kiasi hiki? Je tutaendelea kuridhia kuwa kama samaki kwa kulishwa utumbo wetu na kukaangwa kwa mafuta yetu? Samaki ni hayawani. Je twafaa kuwa kama hayawani wakati tu binadamu?

Hakuna ubishi. Amani ni muhimu na lazima. Lakini amani gani inayolinda dhuluma na nakama? Haiingii akilini kulinda amani kwa kujidhuru. Ni mpumbavu gani atafuga wezi nyumbani kwake eti kwa kuogopa kuvunja amani kwa kuwapeleka polisi au mahakamani? Hii si amani ni utaahira. Hii huwa mbaya vitu hivi vinapogeuka mfumo tena hai badala ya kufishwa kwa gharama yoyote hata kwa kuikosa amani lakini haki ikawapo.

Tuombe Mungu watawala wetu wazidi kujiaminisha kuwa wataendelea kuvurunda bila kukamatwa. Mwisho wa jinai hii ni mateso kuuzidi umma nao ukaamka na kujikomboa kwa kuwafurusha toka madarakani.

Hata nchini Romania wakati wa imla Nicolae Causescu hali ilikuwa mbaya kuliko hapa. Mfano wa karibu ni Zaire ya zamani ambapo jambazi Joseph Desire Mobutu aliigeuza nchi kuwa shamba lake la mifugo. Lakini umma ulipochoka kilichotokea inabaki kuwa historia.

Je, hujuma dhidi ya mali na raslimali za taifa inayosababisha umaskini na mateso makubwa kwa jamii inaweza kuwa chemchemi ya kujitambua na kuleta ukombozi wa taifa? Adui yako muombee njaa kwani itamtoa usingizini akahamanike kuondosha njaa.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 15, 2010.

2 comments:

Mzee wa Changamoto said...

Kama mtu hataweza kusoma article yote, basi na asome aya ya kwanza kuwa "WATANZANIA, tofauti na mataifa mengine, tunasifika kwa ujinga ambao watawala huuita upole na kuthamini amani. Watawala huutumia ukondoo huu kujifanyia wanavyotaka kubwa likiwa ni kushiriki kutuibia bila kuchelea lolote. Jingine ni kutumia vibaya muda na pesa yetu bila kuchelea lolote pia."

Jaribu said...

Nimefurahi kugundua blog hii. Kila mtu anajua hii Dowans ni ya Kikwete na hiyo International Chamber of Commerce haina uwezo wa kumhukumu mbwa akae chini. Lakini kila mtu anajizuga kuwa hii mikataba mibaya wakati wanajua kuwa hamna uhusiano wowote na mkataba. "Mkataba" mbaya mwingine ni wa kampuni ya Songas, (Makamba Songa! Kikwete Songa!) ambapo TANESCO lazima iwalipe Songas hata kama umeme wake hawauhitaji. Lakini sasa hivi mitambo ya Songas iko "under maintenance", lakini hawatakiwi kuwalipa TANESCO faini yoyote; isipokuwa TANESCO inabidi wafanye mgao