Thursday, 30 December 2010

Baada ya Dowans nani atafuatia kuchuma?

Ingawa si vizuri kupinga amri halali ya mahakama bila kukata rufaa, kuna haja ya kukuna vichwa upya. Inakuwaje taifa lenye kila wataalamu tena bobozi wa sheria kugeuzwa shamba la bibi hivi?

Taarifa kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara imetoa huku kuwa Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) liilipe jumla ya shilingi 106, 000,000,000 licha ya kuwa pigo na aibu kwa taifa ni hujuma na kashfa nyingine ndani ya kashfa.

Kuonyesha kuna namna, hata baada ya kutangazwa hukumu, si serikali wala TANESCO ameonyesha nia ya kukata rufaa zaidi ya watu wenye uchungu na nchi kuhoji kulikoni? Je kuhoji tu bila kuchukua hatua inatosha? Je kama siyo njama, kwanini serikali imepatwa na kigugumizi hata kuzungumzia suala hili nyeti kabisa? Hawa ndiyo wanataka waaminiwe kurejeshewa pesa ya ujambazi wa rada? Je watanzania wataendelea kurudia makosa?

Je hili tuliite makosa halali ya kisheria au njama za kuendelea kuhujumu taifa letu? Nani yuko nyuma ya kadhia hii? Je hawa wataalamu wa sheria na upelelezi waliojaa serikalini wanalipwa kwa ajili gani iwapo kila siku tunaendelea kugeuzwa na mafisadi kichwa cha mwendawazimu?

Kwa kumbukumbu ni kwamba, kisheria, kila kitu kitokanacho na kitu ambacho ni kinyume cha sheria nacho ni kinyume cha sheria. Whatever is done or acquired by unlawaful means is null and void (and illegal) ab initio. Kisheria hata kiakili za kawaida ujio wa Dowan kurithi mkataba wa kampuni ya Richmond LLC iliyothibitika bila shaka lolote kuwa ya kitapeli unaacha maswali mengi zaidi ya majibu. Je hawa walioridhia kampuni hii kuchukua mahali pa kampuni ambayo ni batili si wa kulaumiwa hata kuwajibishwa?

Nani zaidi ya mwanasheria mkuu wa wakati ule anapaswa kubebeshwa mzigo wa hujuma hii? Nani zaidi ya rais ambaye alishindwa kumwajibisha mwanasheria huyu zaidi ya kumkingia kifua hadi wengine wakastaafu na kupewa marupurupu na mafao lukuki hata ambapo kisheria walishachafuka? Nani zaidi ya wananchi wanaoendelea kukubali jinai hii?

Ilikuwaje wahusika wakakubali kuhamisha mkataba toka kampuni iliyothibitika kuwa hewa na kinyume cha sheria bila kuangalia uhalali kisheria kama hii si hujuma ya makusudi?

Kwanini pale Kamati Teule ya Bunge maarufu kama Kamati Teule ya Bunge ya Mwakyembe ilipofumua siri zote nyuma ya pazia na kugundua kuwa licha ya Richmond kuwa kampuni ya kitapeli ilingizwa kinyume cha sheria, Tanzania iliridhia haraka haraka 'haki' zote kurithishwa Dowans ambayo nayo ni ya kutia mashaka? Rejea kugundulika kuwa anwani zake nchini iliionyesha kuwa ile ile ya Richmond na Kagoda-Kipawa?

Kwanini wahalifu wa Richmond waliachiwa waendelee kulihjumu taifa pamoja na ushahidi na wengine kukiri na kuwajibika kisiasa na si kishria? Je ni yale yale ya EPA au EPA nyingine? Huwezi kujadili yai bila kumjadili kuku. Dowans ni yai viza lililotagwa na Richmond.

Tukubaliane. Tunahujumiwa na wale wale tuliowaamini madaraka. Ingawa mzigo wa Richmond alibebeshwa Edward Lowassa, waziri mkuu aliyetimuliwa, kuna haja ya kuchimbua zaidi. Kwa kumbukumbu ni kwamba wakati wa mchakato wa kuleta Richmond ili kuondoa tatizo sugu la umeme amabalo limegeuka kansa, Kikwete aliwahi kuutaarifu umma kuwa anafuatilia mchakato mzima na hupewa briefings na waziri mkuu. Hii maana yake ni kwamba kila alichofanya Lowassa kilikuwa na baraka za bosi wake na ndiyo maana baada ya kutolewa kafara kuokoa serikali ya rafiki na bosi wake hakuchukuliwa hatua zaidi.

Hebu tusome maneno ya mwenyekiti wa CUF profesa Ibrahim Lipumba aliyotoa tarehe 19 Julai 2009.

“Wananchi, leo nawatobolea siri juu ya Kampuni ya Richmond… mhusika mkuu wa ufisadi wa Richmond ni Rais Jakaya Kikwete. Ukiangalia vizuri ripoti iliyotolewa na Kamati Teule ya Bunge iliyoongozwa na Dk Harrison Mwakyembe, utaona inamhusisha Rais Kikwete na ufisadi huo.”

Lipumba aliendelea. “Kwa ukweli huo, Lowassa yeye katolewa kafara tu na rafiki yake Kikwete, lakini rais huyu ndiye aliyepaswa na mpaka sasa ndiye anayepaswa kuwajibika kwa taifa. Hatuwezi kufika kwa mtindo huu.”

Kuonyesha maneno ya Lipumba ni ukweli mtupu, si rais Jakaya Kikwete wala wasaidizi wake walikanusha! Na hii haikuwa mara ya kwanza kwa Kikwete kuhusishwa kwenye kashfa ya Richmond pamoja na ile ya EPA na asikanushe wala kujitetea. Namna hii maana yake ni kwamba tuna mkuu wa serikali anayesimamia hujuma kwa nchi.

Muulize Kikwete. Kwanini hakuwahi kukanusha kushiriki na kunufaika kwake na kashfa ya EPA ambayo pesa yake inasemekana ilitumika kumwigiza madarakani? Muulize hata mtangulizi na swahiba wake Benjamin Mkapa ni kwanini hajawahi kukanusha kuasisi wizi wa EPA?

Wako wapi watuhumiwa waliowezesha wizi huu kama Beredy Sospeter Malegesi,Johnson Rwekaza, Kagoda, Peter Noni na wengine waliotajwa wazi wazi na kubainika walitenda jinai ya EPA?

Tufike mahali tuache kulindana na kuogopana. Tumwambie rais awajibike na kuwawajibisha wenzake vinginevyo tumwajibishe kabla hujuma hii haijatupeleka kuzimu. Na hii ndiyo siri ya taifa kuwa maskini kuliko hata vinchi vidogo vilivyotuzunguka visivyo na raslimali hata robo yetu. Na hii ndiyo siri ya watawala wetu kutotaka kuandika katiba mpya kwa kuhofia hatima yao kutokana na uchafu wanaoendelea kufanya.

Kashfa hii mpya ya Dowans itufungue macho na kuchochea hasira zetu kama umma kukikabili kikundi cha wezi kinachotupeleka kuzimu.

Inapaswa wananchi wafahamu kuwa serikali haina pesa yake zaidi ya pesa yao. Hivyo pesa itakayolipwa kwa kampuni hii yenye kutia kila shaka ni yao na si ya serikali. Watapandishiwa bei ya umeme na vitu vingine ili kufidia pengo hili. Kama hawajui wajue.

Je kutokana na nchi yetu kugeuka chaka la walaji, nani atafuatia kuchuma kwenye hili shamba la bibi? Je ni mikataba mingapi iliyosukwa kidowans ili ikivunjika wahusika watajirike haraka kwa pesa ya mataahira na mafisadi?
Chanzo:Mwanahalisi Desemba 28, 2010.

2 comments:

Jaribu said...

Sio kama watu hawajui kuwa Kikwete ndio Dowans. Lakini kama ulivyogusia elsewhere kwenye website hii, nani atamfunga sultan, I mean paka kengele? Besides, somebody has to pay for those fancy campaign helicopter flights.

Anonymous said...

Jaribu umesema kweli kabisa. Nafikiri sasa ndio wakati wakutambua wazalendo halisi nje na ndani ya CCM.