Wednesday, 29 December 2010

Hosea unangoja nini TAKUKURU?Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hosea hivi karibuni alijikuta matatani. Hii ni baada ya mtandao wa kufichua usiri na ufisadi wa kimataifa wa Wikileaks kufichua alichoongea na mwana diplomasia wa kimarekani, Purnell Delly mnamo Julai 2007.

Kwa mujibu wa gazeti la The Guardian la Uingereza la 19 Desemba 2010 lililofichua haya ni kwamba Hosea hana imani na bosi wake ambaye anamuona kama kikwazo katika kupambana na ufisadi. Anaonyeshwa kama mtu aliyekata tamaa na asiye na uhakika na usalama wake. Pia anaonyesha kama mtu asiye na mamlaka wala heshima zaidi ya kutumika kama kiraka au kikaragosi tu kwa sababu ya kutaka riziki tu.

Kwa maana hiyo, rais Jakaya Kikwete baada ya kujua hili naye hatakuwa na imani na Hosea tena. Hapa kunajengeka kutoaminiana hata kuogopana na kuweza kuhatarishiana ulaji hata maisha. Na katika vuta nikuvute hii mwenye kuathirika zaidi ni Hosea ambaye maongezi yake yanamwonyesha kama mtu asiyejiamini wala asiye na maadili. Maana angekuwa na vitu hivi ama angemkabili bosi wake na kumpa ya moyoni au kuachia ngazi hasa baada ya kuona anatumiwa na kudhalilishwa. Lakini kwa miaka yote ambayo amekuwa TAKUKURU hajafurukuta zaidi ya kuendelea kujirahisi na kukubali kuendelea kutumiwa.

Ingawa Hosea alikanusha yaliyoandikwa na The Guardian, ukweli ni kwamba hana udhu tena wa kuendelea kuwa Mkurugenzi wa TAKUKURU. Pia hata bosi wake, yaani rais Jakaya Kikwete, hana imani naye tena kama ambavyo amekuwa hana imani na Kikwete kiasi cha kunung'unika. Kwa maneno rahisi ni kwamba Kikwete ni kikwazo katika vita dhidi ya ufisadi.

Je yeye Hosea kwa kukubali kuendelea kutumika asifanye lolote alilotegemewa kufanya hajawa kikwazo katika vita hii dhidi ya ufisadi? Je kunung'unika ni jibu? Kwanini asijiuzulu ili umma umuunge mkono yafanyike mabadiliko kama kweli ana nia nzuri na watanzania?

Pamoja na kukanusha, je Hosea kweli bado anapaswa kuendelea kuwa mkurugenzi wa TAKUKURU wakati amethibitisha wazi alivyoshindwa au tuseme kukwamishwa na rais Kikwete ambaye amekuwa akilalamikiwa kwa kuwakingia kifua washirika zake na marafiki na mabosi wake kama vile rais mstaafu Benjamin, mkewe, vivyele vyake na watoto wake. Rejea kauli ya Kikwete aliyoitoa Machi 2007 alipokuwa akiongea na watanzania waishio Sweden pale mmojawapo alipotaka aeleze ambavyo angemshughulikia Mkapa.

Kikwete hakumung'unya maneno wala kuona aibu ya kutetea ufisadi. Alisema wazi wazi kuwa tumuache mzee Mkapa akapumzike vyema baada ya kutuibia mali zetu. Hata hivyo wengi hawakushangaa kutokana na ukweli kuwa bila msaada wa Mkapa hasa kwenye skandali ya EPA, huenda Kikwete asingeshinda urais. Hivyo, aliamua kulipa fadhila kama ambavyo amekuwa akifanya kwa washirika na marafiki zake wengi wanaotuhumiwa kwa ufisadi.

Muulize Hosea. Kesi ya Kiwira imeishia wapi zaidi ya kusingizia kinga kwa Mkapa? Tulipouliza kama washirika wa Mkapa yaani mkewe wakweze na watoto wao nao wana kinga, hakuna aliyejitokeza kujibu. Hata ukiuliza tena si Mkapa wala serikali, wote watakaa kimya ili umma usahau waendelee kupeta. Nijuacho ni kwamba pamoja na Mkapa na washirika wake kujiuzia mgodi wa Kiwira kwa bei ya kutupwa, waliutumia kuibia pesa ambayo nayo ililipwa na serikali toka hazina. Rejea serikali kulipa mabilioni ya shilingi kwa wafanyakazi wa Kiwira utadhani ilikuwa imewaajiri wakati walikuwa wametwaliwa na Mkapa kama mwekezaji.

Muulize Hosea Kagoda ni nani na amemfanya nini zaidi ya kumjua na kumuepuka kwa kumuogopa bosi wake. Muulize Hosea ambaye alitaka kutumiwa kuhalalisha na kubariki Richmond kwa kuutetea uoza wa aliyeipendelea kuiingiza nchini waziri mkuu mtimuliwa Edward Lowassa. Muulize Hosea, kama kweli ni safi, kama ameishataja mali zake zote bila kuficha.

Wengi wanaweza kudanganyika na kuamini kuwa Hosea alizuliwa. Delly angemzuliaje ili iwe nini wakati akijua fika maongezi yao yalikuwa ni siri za kibalozi ambazo kama siyo kuangukia kwenye mikono ya Wikileaks hakuna ambaye angeyajua akiwamo yeye na bosi wake yaani rais Kikwete. Hivyo kukanusha hakumsaidii na kama ni ubovu kwenye mahusiano na bosi wake umeishatokea. Akubaliane na hili ajiuzulu kabla ya hasira za bosi wake kumuumbua kwa kutimuliwa kwa aibu.

Kumekuwa na shutuma nyingi toka kwa wapinzani wakidai kuwa hata kutokamatwa kwa wamilki wa kampuni ya kijambazi ya Kagoda inayodaiwa kumilkiwa na mbunge wa Igunga Rostam Aziz kumesababishwa na Kikwete kumkingia kifua kutokana na kulipa fadhila. Rejea kumteua mtuhumiwa wa kashfa ya EPA, Peter Noni aliyetajwa na mwanasheria aliyesainisha (attestation) baadhi ya nyaraka za kuhamishia pesa za EPA. Bhindika Michael Sanze toka kampuni ya kisheria ya Maregesi chamber, kuwa mkuu wa benki ya raslimali.

Kitu kingine kinachomtoa knockout kiasi cha kumtupa Hosea nje ya ofisi ni ile hali ya kukiuka kiapo cha utii kwa bosi wake na kutunza siri za ofisi. Laiti siri hizi angezimwaga kwa wananchi ambao kimsingi ndiyo waajiri wa bosi wake, lau wangemtetea. Lakini amekwenda kuzimwaga kwa wageni! Sijui kama Kikwete atamvumilia ikizingatia asivyopenda kukosolewa. Rejea yaliyowapata akina Samuel Sitta walipoanzisha vita dhidi ya ufisadi.

Kwa kukiuka kiapo na kulalamika kwa watu wasio wateule wake na kuonyesha hofu ya maisha yake, Hosea amepoteza uaminifu kabisa. Hivi Hosea atakaa ofisini kufanya nini iwapo ameshindwa hata na mibaka na majambazi ya kawaida yaliyoiba mabilioni ya pesa yetu kwenye ununuzi wa rada na dege feki la rais wakati wanajulikana?

Hata hao wafanyakazi wa TAKUKURU ukiwachunguza kula, vaa yao na mali wanazomilki utakuta nao ni wala rushwa wa kawaida tu kiasi cha kuifanya TAKUKURU kuwa chombo cha kulinda na kudumisha rushwa.

Kutokana na hali hizo hapo juu ni ima Hosea ajiuzulu au ang'ang'anie ili Kikwete amtimue. Pia kwa wananchi kujua kuwa hana ubavu wa kushughulikia ufisadi, wanaweza kushinikiza aachie ngazi huku wakitaka TAKUKURU iondolewe chini ya ofisi ya rais. Maana, kimsingi rais anaitumia kulinda ufisadi badala ya kupambana nao.

3 comments:

Anonymous said...

Hosea hana tofauti na Kikwete na anachofanya ni kumwanga machozi ya mamba wakati naye ananufaika na ufisadi

Nel said...

The website is very good!
Congratulations!
Happy new year!

NN Mhango said...

Nel very many thanks for your visit and congrats. Welcome again and again.
Again, we feel blessed when one drops a comment.
Happy new year to you too.