Wednesday, 29 December 2010

Mafisadi sasa matumbo moto


NGOJA niimbe rap ya rais M7 nijiliwaze kidogo. Maana ukiimba unajisikia kama rais rais hivi.

Natema Akati kaarara, Kaarara nikaza Igara, Igara owa Ntambiko, Ntambiko yampa akasyo, Akasyo nakaha abagyesi, Abagyesi bampa oruro, Oruro naruha Warukoko, Warukoko yampa ihuri, Ihuri nariha abaana, Abaana bamp'engyeya, Engyeya naagiha omukama, Omukama yampa Kasha, Kasha nagishweza omukazi, Omukazi yanzaarira omwana, Namweeta Mugarura Yaagarura eby'ow'ishe n'ishenkuru.

Mp'enkoni mp'enkoni mp'enkoni, Mp'enkoni engarama ziizire, Ziizire niicund'ebinio, Ebinio bya Rutendegyere, Rutendegyere enkuba emuteere, Emuteerere ahaiguru mpariya, Ahaiguru hariyo orwitiri, Orwitire oruzaarwa n'enkura,Enkura eshoroma etegire, Etegire akaara k'embogo, Ak'embogo karimu omwonyo, Omwonyo guruga, Nsharira Nsharira omunda y'engoma, Y'engoma, y'engoma, y'engoma.

Dowans dowans karibu bongo, Bongo wana dola,
Dola za kugawa, Ukiwa na mzito, Dola unachota,
Unaunda Richmonduli, Richmonduli inakupa dowanis,
Dowanis inakupa dola, Dola za kutesa.

Do you want another rap? lol! We koma. Baada ya rafiki yangu M7 kukumbwa na misukosuko kuwa aachie madaraka na amekaa muda mrefu na kuchusha huku akihudumia familia, ukoo na kabila lake, aliamua kujiliwaza kwa kuimba rap.

Hata pale jamaa ambaye ni mwanafunzi wangu, Julian Assange ambaye jina lake haswa ni Assenga alipoamua kudai anahofia imla wa Libya, Muamar Gadaffi anaweza kumnyotoa roho, aliamua kujiliwaza kwa kuimba rap.

Mwenzenu sina hamu na hawa jamaa wa wikileaks. Wanavyotoboa siri zetu sijui kama walevi wakizinduka tutapona. Sasa tazama kuwaogopa naishia kuwa mlevi!

Yaani wanajua hata hawara wa maris wote! Nani angelijua kuwa wangefichua hawara wa imla wa Libya waliyemuita toto la Kiukraini? Jamaa wanajua hata chupi wanazovaa vigogo. Wanajua hata wale wanaotawaliwa ima na mafisadi, nyumba ndogo hata wake zao.

Wanawajua hata wale walikasimu madaraka yao kwenye chupi au vyumba vya kulala kiasi cha bi wakubwa kuwa marais wasiochaguliwa na wenye vyama vyao vya nyuma ya pazia wakihomola nchi za kitwahuti kama hawana akili nzuri.

Nani angefikiri kuwa hawa weaklick wangeweza kujua siri zangu zote ingawa hawajazianika kutokana na kuogopa mwanafunzi wangu Assange nisimuachie laana?

Turejee kwa walioanikwa. Mnene wa Taasisi ya Kuboresha na Kuneemesha Ufisadi (TAKUKUU) ndiye majeruhi wa kwanza kayani. Jamaa walianika alivyonanga bosi wake ukiachia mbali kumlamba uchogo na kumpaka mafuta kwa mgongo wa chupa.

Jamaa kweli alimpaka. Yaani haogopi kumuona bosi wake kama kingpin wa mafisadi yarabi? Kweli wanasiasa ni watu wa ajabu ingawa hawana mikia kama nyani. Hata hivyo hawana tofauti na nyani kutokana na kufanya mambo yao kinyani nyani au monkey business.

Hakuna kitu kilinifanya nicheke si kwa furaha bali uchungu kama jamaa yangu Daktari wa Sharia Eddy Oshea kukimbilia kwenye magazeti kukanusha alichosema.

Jamaa kwa kula matapishi yake ili kulinda ulaji wake mie sina hamu. Amenikumbusha jambazi mmoja aitwaye Johansen Mwananyika aliyekuwa akitaka ninyotolewe roho baada ya kueleza ujuha wake naye akakimbia kukanusha na kutaka kufungia gazeti. Yuko wapi zaidi ya kuishi mafichoni kama Tunituni akilindwa na Njaa Kaya?

Wengi hawakujua kuwa kumbe Oshea ni kama kikaragosi kinachotumiwa na Njaa Kaya kufanya usanii wake. Hana tofauti na kikaragosi cha Joyce Wowowo kwa wale wenye kumbukumbu ya kikaragosi hiki maarufu kwenye jiji la Bongo.

Kilichonikuna ni kikaragosi kutumia kikaragosi wakati vyote ni vikaragosi vinavyochezeshwa na akina Ewassa na Rost na Endelea Chenga.

Una habari kuwa Oshea alikiri kuwa hana ubavu wa kuwagusa mafisadi walioteka kaya na kuigeuza shamba lao la bibi? Nasikia hata kwenye huu ujambazi wa Dowanis ni wao walioko nyuma ya pazia. Mwuulize Papa Six atakujuza
Kwa sasa nina mpango wa kumwandikia mwanafunzi wangu Assange afichue uchafu wao wa Kagoda na HEPA baada ya kugusa ule wa mrada na mdege feki wa bwana rahisi.

Jamaa zangu mabwege kweli. Una habari gabacholi aliyewaunganisha na lile shirika la utapeli wa silaha la kwa mama liitwalo BEA alikwapua dola zaidi ya milioni kumi wakati wao waliishia kupewa kimilioni kimoja kama ilivyokuja kubainika kwa mzee wa madafu Chenga ambaye naye ni kigogo anayemnyima usingizi Oshea?

Kwa kuzingatia niliyonyaka kwenye weacklick ni kwamba Oshea ni kama changu kwani ana mabosi wengi kuanzia mkuu mwenyewe na mafisidunia wenzake. Laiti angekuwa mrume kama mimi ashakitoa zamani huku akimwaga tamaa kwa kuku ili kila mtu adonoe aone nani atafaidi na kufaidiwa.

Kwa vile yeye ni bonge la mroho na mlafu achumiaye pakacha lake liitwalo tumbo, hata mshike pabaya, hawezi kuachia ulaji. Kanikumbusha kisa cha Kanji aliyemwacha bi mkubwa wake achukuliwe na aliyempa mtaji ili biashara yake isidode kwa kudaiwa alipe. Watu wanaopenda vitu hawana utu hata kidogo. Ni watu vitu tena vinyama mwitu waitwao watu wakati si watu bali wanyama mwitu wafananao na watu.

Laiti ningeteuliwa mie kuendesha vita dhidi ya ufisadi licha ya kuwakamata hata walioniteua, ningeamuru kila mtu aniletee maelezo ya alivyopata mimali yake. Baada ya hapo ningeikomba mimali yao halafu nikaishia ughaibuni kwenda kutumbua kama wanavyofanya magabacholi baada ya kuwaliza walevi wa walevi wao watawalao.

Nami baada ya kujua kuwa njuluku zangu zitaibiwa kwa mara nyingine kuwalipa Dowanis, naweza nikaamua kuimba rap. Do yo want another rap?

Yeah Sebo. Walevi itikieni.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 29, 2010.

1 comment:

Anonymous said...

Ee mola asante kwakutufunulia mambo haya. Endelea kutuonyesha huu uozo kwani hakuna anayeweza kushindana na wewe. Sheikh Yahya umeshindwa kuzuia na hili??? Ha ha kweli ukipokonya haki ya mtu you will suffer for the rest of your life. Sinema ndio kwanza inaanza!!!