Wednesday, 15 December 2010

Nimeunda serikali ya ujanja wa kitaifa

Siku hizi nyumbani kwangu kumezuka balaa ambapo kuna dini na vyama tofauti. Hapakaliki wala kulika kitu bila kuonyeshana ubabe na sura za minuno na mibeuo. Kuna Chama Cha Mama (CCM) na cha Concubine Ushered into Family (CUF). CCM ni cha Bi mkubwa wangu na CUF cha Nyumba ndogo. Niwaonye wasomaji kwanza. Msijechanganya hivi vyama vya nyumbani mwangu ni vile vya kaya yenu hata kama vinafanana kwa majina sifa hata majaliwa.

Nimekuwa, kwa kitambo kirefu, nikisikia umbea wa wagombea wakinigombea wapate ulaji. Japo hatukufanya uchaguzi kwa kuogopa kumwagia maji ya moto na michuzi ya chapati, nimeamua kuunda serikali ya ujanja wa kitaifa (familia). Sitaki wala yanikute yatakayowakuta maharamia kama Laurent Gbagbo wa kule nonihino.

Narudia tena kwa herufi kubwa. Vyama hivi havina uhusiano na vyama vya kisiasa vya nchi yoyote juu ya uso wa ardhi na chini ya jua. Na isitoshe hakuna aliye na hati milki ya kutumia vifupisho husika hata vikifanana. Kwa vile mie ni profesa wa sheria, sina shaka na hili na sijavunja sheria ya nchi yoyote. Hata nikivunja sheria, nitakwenda kwa wale wataalamu wa jinai walioghushi vyeti vya kitaaluma na bado wakateuliwa kuula. Hawa wakishindwa nitakwenda kwa wale majambazi wa Downwans wanipe mbinu ya kuchuna buzi bwege kwa kutumia sheria kama walivyowafanyia jamaa wa Mizengwe.

Tuendelee. Ukiangalia sifa za vyama husika, unaweza ukaona ushindani na mikakati ya kumalizana vilivyo vya hali ya juu.

Baada ya kuona mashitaka na lawama haviishi nimekubali yaishe kwa kuweka silaha chini na kukubali kushindwa hasa baada ya mjumbe kutishia kunifikisha kwa mtendaji wa kata.

Kwangu mtendaji wa kata anatisha kama The Hague na ICC yake kwa serikali mbovu za kiswahili. Isitoshe baada ya kuona kule kwa kina madevu wanawekana sawa na serikali za ujanja wa kitaifa kwanini nami nisiige mfano bila kujali kuwa kuna watu watadhulumika na kuudhika? Hapa unachofanya ni kuwapa ulaji viherehere wenye kufikiri kwa kutumia matumbo yao kama jamaa zangu wa kule Zaainzibaa.

Nimeamua kuunda serikali hii haraka. Nafanya hivyo kwa kujua kuwa nikiendelea kuuchuna wale jamaa wa wikileak wanaweza kunivua nguo bure. Isitoshe wakieleza jinsi nilivyolazimishwa na homa na hofu ya The Hague nitakuwa nimeumbuka mzee mzima.

Turejee kwenye serikali ya ujanja wa kitaifa ambayo ni janga kwa bi mkubwa na vitegemezi vyetu.Muathirika wa kwanza ni bi mkubwa mwenyewe mama Kapayukaji almaaruf mama Kidume. Ameathirika sana baada ya mamlaka yake kuyapiga upande na kuwapa nyumba ndogo kama walivyofanya kina Madevu baada ya kusikia kuwa madevu mwenzao aitwaye Mureno Okampo alikuwa akiwanyemelea na kuwapeleka alipompeleka Chaz Teila.

Hii inaitwa umoja wa kitaifa ambapo haramu na halali huwekwa kapu moja. Kwa lugha nyepesi ni kwamba unaharamisha halali na kuhalalisha haramu. Hii haina tofauti na nilivyofanya kwa kuhalalisha nyumba ndogo na kuharamisha uhasama wa nyumba kubwa kwa nyumba ndogo.

Hebu niike hivi. Kama ni kwenye utawala wa kaya, unaandaa uchafuzi na kutumia pesa za walevi. Wanajipendekeza na kuja kwenye vituo vya kupigia kula wengine hawakuti majina yao na wakiyakuta wakapiga kula unachukua unaweka unachakachua waa. Kwani haya hayapo hata kama tunafungana kamba kwa kisingizio cha amani uchwara ya watu wala watu kuwala watu kwa sanaa hii? Soma taratibu bi mkubwa asikusikie akanivisha gagulo. Ukweli ni kwamba mzee mzima nami nimechakachua kinamna.

Wajua ni kwanini naogopa bi mkubwa asikusikie? Siyo tu atanivisha gagulo bali anaweza kunidai fidia ya mabilioni kama wale wezi wa Downwans walivyowaingiza mkenge mabwege fulani. Naogopa madai kama yule mama kachangu na kadungaembe ahubirie maji akanywa mvinyo. Si mnamjua mama huyu tena mbung'o wa kuteuliwa ambaye neno mume wangu kwake ni msamiati mugumu? Hayo tuyaache. Astaghafillullahi nshajitia nuksi kwa kumjadili nuksi huyu. Kwa jina la baba na la mama na la bibi na roho mtakakitu usiamini.

Tuendelee na serikali yangu ya ujanja wa kifamilia sorry taifa langu. Kama hujui ujue. Kutawala na kuwala walevi ni raha na mchezo japo mchafu lakini wa kufurahisha. Ili kuwaweka sawa waathirika wa sanaa zangu ambao ni bi mkubwa na vitegemezi vyetu, nimewafunga kamba kuwa muafaka na kuunda serikali ya ujanja sorry, ya umoja wa kaya ni cheche na chemi chemi ya maendeleo amani na mshikamano. Nao bila hata kufikiria wameshikilia sanaa zangu! Ukitaka kujua nimaanishacho nenda kawaambie ukweli kuwa nimewaingiza mkenge kwa maslahi yangu, watakunyotoa roho bure.

Maskini hawakujua kuwa nimefikia nilipowafikisha kwa sababu kuu mbili yaani kumuogopa Mureno yaani mtendaji wa kata na kulinda ulaji wangu. Ukisikia uchakachuaji wa kisasa na kisasi ndiyo huu.

Zamani kwenye kaya yangu hatukuwa na makamu wangu wala kitu kama hicho. Kwa sasa wako wangapi? Wako wabee au wawili kwa wale wasiojua lugha za kisasa. Baada ya kuwapa ulaji hawa waliokuwa maadui sasa mambo ni mswano.

Siwezi kumaliza stori hii bila kuelezea balaa linaloninyima usingizi. Baada ya kuonja raha na maisha kwa maana ya maisha, sasa eti walevi wa nyumbani kwangu wanataka katiba mpya itakayoninyang'anya ukuu na utukufu wangu. Kwangu niko juu ya sheria jambo ambalo linanifanya niwajibike kwa tumbo langu na nyumba ndogo zangu nyingi. Sasa walevi wangu wamehanikiza kutaka kunitungua kwa kutaka katiba mpya ya kaya. Sina ujanja. Niko kwenye mchakato wa kukubaliana nao kabla siri zangu nyingi hazijafichuka.

Napanga kukubaliana na madai yao. Kwa sababu nikikataa wakaanza kumwagiana mitusi ngumi hata michuzi, Mureno wangu ambaye ni afisa mtendaji wa kata anaweza kunipeleka lupango kwenye ofisi yake ambayo huwa napenda kuiita The Hague. Mie nimeamua kuwa mkweli, kubadilika na kujifunza kusoma alama za nyakati kabla ya kupitwa na wakati hata kama nikiamini katika uchakachuaji. Najua fika. Uchakachuaji si sayansi ya kudumu bali kujidanganya tu. Wenzangu na mie walioko juu mwaambwa. Mkizidi kujifanya mwajua mtaishia pabaya. Mie simo.

Naona wale wana harakati wa kudai katiba mpya wanakuja. Ngoja nijikate kislesi wasijenibana nikajinohino kwenye msuruali wangu. Usimwambie mtu.
Chanzo: Tanzania Daima Desemba 15, 2010.

No comments: