Monday, 13 December 2010

Barua kwa rais Jakaya Kikwete
Ndugu rais,

Samahani sitatumia neno mheshimiwa kutokana na kutolipenda ukiachia mbali kuchukia tabia ya kujikuza na kuabudiwa.

Wala sitakuita daktari bali kanali mstaafu kwa vile udaktari wako ni wa heshima tu.

Kwanza, nikupe pole kwa 'kuchaguliwa kwa kishindo' ingawa si cha Tsunami kama ulivyoahidi, bali cha uchakachuaji. NEC imekuangusha hata taifa. Maana uliotuahidi kishindo cha Tsunami, tunaona kama hukutwambia ukweli.
Naomba niwe mkweli kwako kusema yafuatayo:

Kwanza, sikukupigia kura kutokana na kutoridhishwa na ahadi zako nyingi juu ya nyingine lukuki ambazo hukutekeleza hata moja. Wabaya wanasema: maisha bora yamekuwa ni walio karibu nawe tu.

Pili, ni kutokana na kutowahi kusikia ukiongolea sera zako.

Sababu nyingine iliyonikera ni wewe kukacha mdahalo.

Tatu, marafiki zangu wengi hawakupata hata hiyo fursa ya kupiga kura kutokana na kufanyiwa mchezo mchafu na tume ili kushindisha chama chao.

Nne, kwenye jimbo moja anakotokea rafiki yangu, Tume yako ya Uchaguzi ambayo wabaya wako wanaiita tume ya Uchakachuaji ilitangaza mgombea wa CCM kuwa mshindi ingawa alishindwa wazi kabisa. Na haya ndiyo madai ya majimbo mengi nchini. Hii maana yake ni kwamba NEC imewabambikia wawakilishi wananchi. Na hawa licha ya kutokuwa chaguo la wananchi bali tume, hawawezi kuwawakilisha wananchi wala kuleta maendeleo.

Tano, japo mie si mwanachama wa chama chochote , naungana na wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutokutambua kama rais wangu hata kama utaendelea kulazimisha kunitawala-si kuniongoza. Maana viongozi waliondoka zama za Nyerere. Ukitaka niachane na msimamo huu, kaa kwenye meza ya duara uongee na hawa unaowaona kama adui zako ingawa naamini siyo. Shukuru Mungu una bahati sana ndugu rais. Hivi kama wangeingia mitaani ungefanya nini wakati huu Mahakama ya Jinai ya Kimataifa (ICC) Ilipotandaza nyavu zake barani tena pale nchi jirani ya Kenya?

Japo Chadema wamenyamaza, usijidanganye, ni wanasiasa kama wewe. Ukiendelea kuwazungusha, watabadili lugha na mikakati toka ile ya kuwataka wananchi wawe watulivu na kuwaambia wakaichukue haki yao. Hapa ndipo mapambano hayataepukika. Na yakitokea mapambano, amini mtaishia The Hague.

Pia wananchi wanaweza kupuuzia ushauri wa Chadema wa kutulia wakaamua kutafuta haki yao mitaani. Maana kama ni kupigwa mabomu ni wao waliopigwa mabomu na kunyang'anya ushindi wao na isitoshe wao ndiyo wanaathirika sana kuliko hao wanasiasa. Wazungu hupenda kuweka plan B.

Nawe yapasa uwe na plan B kama ambavyo wananchi pia wanaweza kuwa na plan B.

Tusidanganywe na amani tena ya uongo. Amani gani iwapo matokeo yanatangazwa kwa mabomu ya machozi na utata? Hakuna nchi ilisifika barani Afrika kuliko hata Tanzania kama Ivory Coast. Sasa iko wapi? Je kuna haja ya kwenda kule? Tusijidanganye kuwa kuna amani na mshikamano. Mshikamano gani iwapo kuna wabunge na watu wasiomtambua rais ukiachia mbali waliolazimishwa na tume? Mshikamano gani wa kudanganyana na kuchuuzana tena mchana kweupe?

Tano, japo mie si mshauri wako, naomba nikushauri. Juzi nilishuhudia kitu cha kutia aibu na ghadhabu ambacho kilipunguza heshima na uzito wako. Japo ni haki yao kidemokrasia, wabunge wa Chadema, si haba, wamemekudhoofisha hasa ikichukuliwa ulivyoingia kwa mbwembwe na kishindo mwaka 2005.

Nisisitize. Ni aibu na pili ni pigo la aina yake kwa taasisi ya urais. Hauna tena uzito na heshima ya pekee kama ilivyokuwa awali. Ukichanganya na tuhuma za ufisadi ndiyo usiseme.

Sasa ndugu rais nisikucheleweshe. Naomba nikupe somo toka visiwa vya Zanzibar ambapo kwa miongo zaidi ya miwili tulishuhudia mvutano na heka heka hadi damu kumwagika. Chama cha Wananchi (CUF) kilishikilia ngangari dhidi ya ngunguri hadi sasa kinaanza kueleweka hasa baada ya kuingia maridhiano na hofu ya CCM ya kumwaga damu na kupelekwa The Hague.

Je ndugu rais unashindwa nini kukaa meza moja na Chadema na kumaliza tofauti zenu ambazo kimsingi zimesababishwa na wizi wa kura au uchakachuaji ambao Chadema wanasema ndiyo siri na mtaji wa ushindi wako?

Ndugu rais, dunia nzima sasa inajua kuwa rais wa taifa lililosifika kwa amani ametokana na wizi wa kura. Nashangaa sijawahi kusikia ukikanusha. Si wewe, wasaidizi wako wala chama chako! Sijui hawa mabingwa wa propaganda uzushi na uongo tuliowaona kwenye kampeni kipindi hiki wameishia wapi? Na je wanalipwa kwa lipi kama wanashindwa hata kutoa msimamo wa chama au wewe kama taasisi yenye mamlaka nchini?

Ndugu rais nilikusikia juzi Dodoma ukiwashushua Chadema kuwa hawana rais mwingine isipokuwa wewe na hawana mtatuzi wa matatizo yao isipokuwa wewe. Hii ni kweli. Lakini kama utashikilia mipasho kama jamaa yako komandoo wa zamani wa Zanzibar hutafika mbali.

Kwanza, uchumi wa nchi umo kwenye chumba mahututi ukiachia mbali ripoti ya juzi ya umoja wa mataifa ya maendeleo kuanika uoza wa ajabu. Kwa ufupi ni kwamba ripoti tajwa ilizima tambo zote za kuleta maisha bora kwa watanzania. Sana sana, ukisoma kashfa zinazoanza kuibuka kwa mfano za unyakuzi wa ardhi ambazo zinamhusisha mwanao na asikanushe, waliopata maisha bora ni wale wa nyumbani kwako na marafiki zako.

Na hii ndiyo siri ya watanzania kukupa kura kidogo. Hili nalo ni pigo na tusi kwa mtu aliyeingia akijinakidi kama chaguo la Mungu na watu. Hivi kweli bado wewe ni chaguo la Mungu? Je wale wasaka ngawira na waramba viatu walioandika hata vitabu wakijua fika wanakudanganya, wanajidanganya na kudanganya bado wanakufaa?

Hivyo basi, kama ikitokea mkaendelea kuvutana, kuzungukana na kuhadaana, uchumi wetu na wananchi vitaathirika na kuanzisha fujo.

Naomba nimalizie na jambo moja. Bila kutenda haki ikaonekana ikitendeka, mgomo wa Chadema na hatua nyingine zinazoweza kufuata, vitaua dhana nzima ya amani na utulivu ambavyo wahalifu wengi wanapenda kuvitumia kuwatishia watanzania. Bila haki hakuna amani na amani haiji bali kwa kutenda haki tena kwa wote.

Mwisho, nasikia eti kampuni ya Dowans ni yako, Edward Lowassa na Rostam Aziz?
Kila la heri ndugu rais.
Chanzo: Dira ya Mtanzania Desemba 13, 2010.

No comments: