Wednesday, 19 October 2011

Hatimaye Lowassa afikia mwisho


Kwa waliosoma u kusikiliza hotuba ya mbunge wa Monduli na waziri mkuu wa zamani aliyetimuliwa, Edward Lowassa, watakubaliana nasi kuwa sasa amefikia mwisho. Wengi walitegemea Lowassa angekuja na jipya. Ajabu alikuja na mipasho dhidi ya waandishi wa habari na maadui zake wa kutengeneza.
Hakuna kinachochekesha kama Lowassa kujigonga na kujikomba kwa Kikwete akirai na kubembeleza. Anaendelea kushikilia msimamo wake kuwa yeye na Kikwete hawakukutana barabarani.
Kwa ufupi ni kwamba hakuna jipya alilosema Lowassa zaidi ya kuiangukia CCM. Kimsingi, alichofanya ni kuihadaa CCM kuwa yeye ni mtiifu huku akimwaga sifa kwa Kikwete ili abadilishe uamuzi wa kumvua gamba. Hakuongelea ufisadi wala tuhuma yoyote ya kifisadi dhidi yake. Kabla ya kuandaa mkutano huu, wengi tulimuona Lowassa kama jasiri.Lakini baada ya kumalizika mkutano tumemuona kama mwoga wa kawaida. Na hii ni mara ya tatu Lowassa kuonyesha kuwa ni mwoga wa ajabu. Mara ya kwanza aliionyesha mwaka 1995 pale marehemu Mwalimu Julius Nyerere alipomrushia kimondo kuwa amejilimbikizia utajiri usioweza kutolewa maelezo ambao ni matokeo ya rushwa na wizi. Mara ya pili ni mwaka 2008 alipokurupuka na kuachia madaraka ya Uwaziri mkuu ambao anaendelea kuulilia. Na mara ya tatu ni leo tarehe 19 Oktoba 2011. Kama huyu ndiyo Lowassa wa sasa, kwisha kazi. Maana hana ubavu tena zaidi ya kutumia na kutegemea sanaa ku-survive.

1 comment:

Jaribu said...

All hype and no substance.