The Chant of Savant

Saturday 15 October 2011

Mpayukaji apewa ‘Power of Attorney’ kuibia taifa

BAADA ya wakubwa fulani kuingizwa mkenge na Mpayukaji na kuunda kampuni ya ujambazi ya Richmonduli iliyobadilisha jina na kujiita Downs, anazidi kufanya vitu vyake kama hana akili nzuri!

Msichanganye na TRA tuliyoongelea wiki iliyopita ambapo tulikuwa tukisaidia wafanyabiashara maarufu kukwepa kodi na kugeuka matajiri wa kutupwa kiasi cha kuwa na ushawishi juu ya nani awatawale walevi.

Ili kufanikisha azma ya kuliibia taifa kiulani, mimi na washirika wangu wenye madaraka ambao ni top secret, tutanzisha miradi ya kijambazi mmojawapo ukiwa ni kusambaza kiza nchini. Tutafanikiwa sana hasa kwa kusingizia ukame ingawa ukame wenye haukuwa wa mvua bali uadilifu na akili. Mradi huu tutaupa jina la Downs. Hii ni baada ya wanoko fulani kustukia jina la kwanza la Richmonduli. Ili kufanikisha ujambazi wetu, tuna mpango wa kujipa tenda ya kusambaza zana zote za kuzalisha kiza nchi nzima.

Na kwa kutumia kampuni yangu ya TRA, tutahakikisha tunakwepa kodi. Ili kuhakikisha hili halikwami, tutaagiza mitambo mikangafu toka kwa Joji Kichaka ili itusaidie kufua kiza ambacho kitaenezwa nchini mapema zaidi. Ili kuhakikisha mambo yanakwenda tulivyopanga, tutaipa sirikali shea kwenye kampuni yetu hewa ili kuwafumba macho walevi wapendwa wa Danganyika.

Ili kufanikisha hili, tutasema kuwa taifa linahitaji kiza cha dharura hivyo kila kitakachofanyika kitafanyika kwa dharura. Hii itatusaidia kukwepa vyombo vingine vya dola kama Bunge, tume za manunuzi na vingine kupata muda wa kuchunguza na kupitia michanganuo yetu. Maana bila ya taifa kuwa kizani, wananchi watapata shida ya kukosa usingizi au kulala kwa taabu. Hatutaki wananchi wetu wateseke wakati tuna uwezo wa kutengeneza kiza hata mvua hapo baadaye.

Tunajua katika kufanya vitu vyetu, kuna vyombo vya dola ambavyo havitaridhika kutokana na kutokuwemo kwenye ulaji huu. Hivyo, hima vitapiga kelele kupinga mradi wetu au vitatia veto. Katika kukwepa hili au kulitumia kwa faida, tumeajiri wanasheria mahiri kuandika mikataba ambayo inatupa nguvu kubwa kuliko asasi nyingine za umma. Hivyo kwa kutumia uchochoro huu, tutahakikisha kuwa kama mashirika mengine ya serikali au vyombo vyake vitapinga au kutusimamisha kusambaza kiza, tunakwenda mahakamani na kushinda mabilioni.

Pia tuna mkakati wa kwenda banki kubwa kuchukua mikopo ya mabilioni ambayo yatalipwa na serikali kwa vile ndiyo itakayotudhamini mikopo hii. Hii inatokana nasi kutokuwa na mtaji zaidi ya akili na hila zetu na usuhuba na wenye maulaji kama vile waziri mkubwa. Ambaye tutamwita Eddie Ewassa Ngoyali.

Ili kuhakikisha hatustukiwi, mmoja wetu ataachana na siasa ili kuanzisha mjadala kumhusu huku mambo yetu yakienda bambam.

Hapa tutahakikisha tunawahadaa walevi kuwa nimeacha siasa uchwara kwenda kushughulikia madili yangu. Wao wasivyo na akili waliponiona Igunguli nikitwanga kampeni ya uchafuzi wala walishindwa hata kunizomea!

Kweli walevi ndiyo waliwao! Yaani hawakuwa na hata ubavu wa kuniuliza ni kwanini nilikuwa nikishiriki kwenye kutafuta mrithi wangu kwenye siasa uchwara kama kweli ni uchwara! Laiti wangeniuliza swali hili ningeumbuka hakuna mfano.

Hakika nawasikitikia walevi kila uchao ingawa sina huruma nao. Yaani wanachagua mtu kula na kuwala tena kwa kuhongwa upuuzi kama ubwabwa bado wanashangilia! Hivi nani aliwaroga viumbe hawa wasiotaka kujifunza kukubali ukweli? Tangu lini mtu anayewakilisha tumbo lake akawawakilisha wenye njaa wakati kuna matajiri wa kujaza tumbo lake kama nilivyofanya mimi?

Siku hizi uwakilishi na uishiwa ni madili mtindo mmoja. Mnakodishiwa madege na makampuni ya madini na kwenda kuhomola mkirudi mnawaweka sawa waliwa.

Mnasaini mikataba uchwara na hatari halafu mnahomola kama tutakavyohomola kwenye Richmonduli baba Downs. Upo hapo mshirika? Nani wa kunizuia iwapo nina Powers of Attorneys and attorneys, judges and whatnot? I have tweaked my strategies. I am using the court of law to steal from wajinga. Woooii! Nimesahau na kumwaga umombo nisijue kuwa nilishahama uingerezani na kurudi ulevini Danganyika Danganyatoto Bongolalalaland ya Mafisi na Mafisadi.

Nashukuru Mungu imelipa huku ikila kwao. Si juzi pilato alitoa tuzo la vijisenti kwa mradi wetu wa kiza tuliouanzishia kule Monduli tukauita Rich-Monduli. Mungu anipe nini sorry Mungu atupe nini? Maana nikisema Mungu anipe nini wenzangu wa nyuma ya pazia ambao ni mabosi na waajiri wangu wanaweza kudhani nina mpango wa kuwaacha Solemba. Msihofu wakuu mie ni wenu na bila nyinyi si ningenonihino kwenye debe kule rupango.

Kwa taarifa ya wanoko wote popote mlipo, huu ni mwanzo. Baada ya jaribio letu kufanikiwa na kukwanyua mabilioni, kaeni mkao wa kuliwa. Mtaliwa wote bila kujali mkubwa au mdogo mwanamke au mwanamme na mengineyo. Tutahakikisha tunaingia kwenye orodha ya akina Warren Buffet na Bill Gates kupitia migongoni mwenu. Mbuga za wanyama na wanyama tele, madini, mabenki na madili vipo kwa sana. Mungu atupe nini zaidi ya wadanganyika na walevi?

Acha niwahi nikagawane mabilioni na Ewassa na tukapange jinsi ya kukwanyua mengine.

Are you there guys?

Washirika na wawezeshaji wengine ambao bado wako kwenye powa siwataji.

Imetoka hiyo!

Jamani, leo tusameheane. Nawahi kwenda zangu San Fransisco kwenye mazishi ya genius mwenzangu Steve Jobs muasisi wa Kampuni ya Apple ambayo huwa naihusudu. Pia jamaa huyu naye alikuwa mlevi mwenzetu.

Chanzo: Tanzania Daima.

No comments: