The Chant of Savant

Sunday 9 October 2011

Kikwete kweli kiboko!


Wachambuzi hata wanasiasa wamekuwa wakimshauri rais Jakaya Kikwete kufanya maamuzi magumu ili kuondokana na ulegelege unaoikabili serikali yake na chama chake. Wengi wameandika na kunakiriwa wakifanya hivyo. Kwa kumbukumbu ni kwamba walioanzisha msamiati wa maamuzi magumu ni Mwalimu Nyerere Foundation (MNF) pale walipoona mambo yakwenda siyo. Hawa si wengine bali mzee Joseph Butiku na hatimaye waziri mkuu mstaafu Jaji Joseph Walioba. Wazee hawa hawakutaka kuwa mashahidi wakati mambo yakiharibika ima kwa kuendekeza woga ua takrima na fadhila kama wazee wengine walivyoonyesha. Hawakukubali kuendeshwa na matumbo yao bali vichwa.

Wazee hawa walipomtaka Kikwete afanye maamuzi magumu hasa kuwashughulikia wenzake wanaotuhumiwa ufisadi walisakamwa. Bahati mbaya wazee hawa walipotoa rai hii walizomewa hata na wazee wenzao chamani hasa wale wanaoshabikia mfumo uliopo kutokana na kunufaika nao. Mmojawapo wa aliyewashambuliwa wazee hawa wenye busara ni mzee Peter Kisumu ukiachia mbali waramba viatu wengine wasio na majina.

Hivi karibuni mmojawapo wa wale waliokuwa wakiwakejeli hawa wazee, waziri mkuu aliyetimuliwa na kashfa ya Richmond na swahiba mkuu na mshirika wa Kikwete, Edward Lowassa alibadili mwelekeo kwa kumshauri rafiki yake afanye maamuzi magumu. Alikaririwa akisema: "Mheshimiwa mwenyekiti hivi sasa kuna ugonjwa umezuka nchini kwa viongozi wa serikali kushindwa kutoa maamuzi magumu, bora ukubali kuhukumiwa kwa kutoa maamuzi magumu kuliko kuogopa kuyatoa. Tukitulia, tukiamua naamini tunaweza."

Kwanza hayo maamuzi magumu ni yapi? Na kwanini Lowassa ameliona hili na si wakati alipokuwa waziri mkuu na mtendaji mkuu wa serikali? Je ni kutaka sifa, kulipa visasi au unafiki wa kaiwada?

Japo maneno ya Lowassa ni kweli tupu, uongo ni yeye kusema haya leo wakati akiwa nje akikabiliwa na shinikizo la kuvuliwa kama gamba la chama chake. Kwani Lowassa ni msafi? Mbona yeye na rafiki yake Kikwete wamekataa hata kutaja mali zao? Hili mar azote limekuwa likifutikwa ikiwa ni ishara ya ufisadi wa wazi wa watawala wetu ambao mali zao zinatia shaka. Hakika nao ni uamuzi mugumu japo hasi.

Hapa chini tutaonyesha kuwa Kikwete alishafanya maamuzi magumu japo hasi. Hakuna maamuzi magumu yaliyotaka roho ya mwendawazimu kama kumteua Lowassa kuwa waziri mkuu huku akipuuza historia na miito yote iliyomtaka asijitie kitanzi kwa kutenda kosa hilo. Ajabu alilitenda kabla ya ukweli kumuumbua yeye na mshirika wake ambaye siku hizi amemgeuzia kibao.

Yafuatayo ni maamuzi magumu yaliyofanywa na Kikwete:
Mosi, kutumia hovyo mali na pesa za watanzania na kuweka upenyo kwa makampuni ya kitapeli kama Dowans kuchota pesa ya umma. Rejea ahadi ya kurekebisha mikataba ya kijambazi ya uwekezaji. Aliishia kuingia mingine tata ambayo inaendelea kulisumbua taifa. Nani haoni nchi inavyozidi kuzama kwenye kiza huku kukatwa umeme mara kwa mara ukisababisha maisha kuwa magumu bila sababu za msingi?

Wakati pesa ya kuzalisha umeme tunaambiwa hakuna, rais na wenzake wanapata pesa na muda mwingi kwenda kutumia ughaibuni huku akikwepa matatizo ya ndani. Nani mara hii amesahau alivyotimkia nje wakati wa mauaji ya Arusha?

Pili, kuruhusu familia yake ijiingize kwenye biashara kwa mgongo wa ikulu. Rejea mkewe kuendelea kutumia asasi yake isiyo ya kiserikali lakini yenye kufanya shughuli za kiserikali ikibebwa na serikali kama alivyofanya mke wa mtangulizi wake. Rejea kutajirika kwa haraka kwa mwanae Ridhiwan aliyetuhumiwa hivi karibuni akashindwa hata kujitetea. Isitoshe ni maamuzi magumu sana kuruhusu Ridhiwan aendelee kuuvuruga umoja wa vijana wa chama cha baba yake bila kujali madhara yanayoweza kutokea na matokeo yake huko tuendako.

Tatu, kuweka nchi kizani na asijali huku akiendelea kutoa uongo usioingia hata kwenye akili ya kuku.

Nne, kuanzisha uchakachuaji kwenye uchaguzi ukiachia mbali kuunda mitandao iliyokisambaratisha chama chake.

Tano, kuendekeza visasi kwenye utawala wake. Rejea kuenguliwa kwa spika wa zamani wa bunge Samuel Sitta na kutubambikizia kibaraka wake Anna Makinda ambaye amedhihihirisha udhaifu wake kama ilivyotokea kwa Lowassa.

Sita, kuendelea kuwateua na kuwakumbatia watuhumiwa wa ufisadi mmojawapo akiwa Peter Noni aliyemteua kuwa mkurugenzi wa benki ya Raslimali (TIB) huku akikabiliwa kuasisi na kutekeleza wizi wa EPA kama ilivyodaiwa na mwanasheria Michael Bhyndika Sanze aliyesajiri wizi huu.

Ni maamuzi magumu kiasi gani kwa kiongozi kujiruhusu kuingia na kubakia madarakani kwa kutumia pesa chafu zenye kutia kila aina ya shaka? Anayebishia hili amuulize Kikwete ni pesa kiasi gani alitumia na zilitoka wapi zaidi ya kwenye taasisi za umma hasa benki kuu kupitia EPA?

Nane, kufanya uteuzi wenye kila utata wa watendaji mbali mbali kwa kuzingatia kujuana. Rejea kumteua Mwanaidi Maajar kuwa balozi ilhali anatuhumiwa kuwa mmojawapo wa waliofanikisha wizi wa EPA.

Tisa, kuanzisha jinai ya kutumia vyombo vya habari na wana habari kuwachafua wenzake huku wakimpamba. Rejea kuendelea kumuweka ofisini mtuhumiwa wa ufanikishaji wa kashfa ya Richmond aliyepewa jukumu la kuisafisha Richmond bila mafanikio Salva Rweyemamu. Huyu pia alitumika wakati wa kusaka urais kwa kumjenga Kikwete huku akiwapakazia wengine. Hapa hatujata waandishi wengine kanjanja na nyemelezi waliojazana kwenye ofisi za CCM ngazi ya wilaya. Hapa bado hatujataja magazeti yaliyohongwa kumsafisha Kikwete na kuwachafua wengine yatokanayo na pesa ya EPA.

Kumi, kumkingia kifua mtangulizi wake Benjamin Mkapa marafiki zake na familia yake wasishitakiwe kwa ufisadi waliotenda. Ni maamuzi magumu kiasi gani kwa Kikwete kufanya madudu yale yale aliyofanya Mkapa? Rejea mke wa Kikwete kuendelea kutumia NGO sawa na ile ya mke wa Mkapa kujipatia utajiri binafsi. Rejea Kikwete kuendelea kuzurura nje sawa na alivyokuwa akifanya Mkapa bila kujali maonyo toka kwa watanzania.

Kumi na mmoja, Kikwete amefanya maamuzi magumu kuamua kuwatumikia mafisadi badala ya wananchi. Rejea anavyozidi kuwakingia kifua majambazi wa Kagoda na Richmond huku akiwapumbaza watanzania kuwa atawapeleka Kanani ambako nako hawapeleki zaidi ya Misri. Rejea wale mafisadi na watoa rushwa waliokataliwa wakati wa mchakato wa 2000 walivyorejea kwa kishindo na kushinda ubunge. Je hawa wanaweza kulisaidia nini taifa zaidi ya kuliuza kwa mabwana zao?

Kumi na mbili, pia kuendelea kutotangaza mali zake na wakubwa wenzake ni maamuzi magumu hata kama ya hovyo. Bila roho ngumu nani angeamini kuwa Kikwete huyu huyu ambaye hajawahi kutangaza mali zake angeruhusu serikali yake eti iwahoji ambao hawajajaza fomu! Ni unafiki na maamuzi magumu kiasi gani?

Kumi na tatu, Kikwete kuendelea kutawashughulikia wauza unga, majambazi na wala rushwa ambao alisema ana orodha zao? Je anazuiliwa na nini kama si kufaidika na kadhia hizi?

Kumi na nne, atapaswa afanye maamuzi mengine magumu kutokana kuanza kuumbuliwa na maswahiba zake kama ilivyotokea hivi karibuni kwa Rostam Aziz kuachia ngazi akithibitisha madai yote dhidi yake yalivyo kweli.

Kikwete ameishafanya maamuzi mengi magumu hata kama hayana maana kwa watanzania. Laiti angetumia ithibati hiyo ya kufanya maamuzi magumu ya hovyo kufanya maamuzi magumu ya kweli!

Haya ni maamuzi magumu hata kama ni hasi. Hebu angalia Dowans inavyoendelea kuhomola pesa yetu utadhani hatuna akili wala shida na pesa hiyo.

Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 9, 2011.

1 comment:

Jaribu said...

Dowans ni mwendelezo wa EPA. Ndio hela ya kanga na fulani hiyo inabidi ilipiwe. Toka atoke Nyerere uwezo wa kutawala wa marais wetu umeshuka sana, na huyu wa sasa anachoweza ni kuchota mali ya umma tu. Lets face, jamaa is an idiot. He should not run a small village, let alone a country!