Tuesday, 18 October 2011

Huu ni mtihani mzito kwa Rais KikweteKADIRI siku zinavyokwenda Watanzania wanangoja kwa shauku kubwa kujua mwisho wa tishio la Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa watuhumiwa wake wa ufisadi yaani Andrew Chenge, mbunge wa Bariadi Mashariki, waziri na mwanasheria mkuu wa serikali wa zamani na Edward Lowassa, mbunge wa Moduli na waziri mkuu waliong’olewa madarakani na kashfa ya Richmond.

Kumekuwa na vuta ni kuvute na kurushia vijembe na tambo kwa muda mrefu. Baada ya kujivua gamba kwa mbunge wa zamani wa Igunga na mmojawapo wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi Rostam Aziz, wengi walijua Chenge na Lowassa wangefuatia. Lakini wapi! Kimsingi, huu ni mtihani mzito kwa Rais Jakaya Kikwete mwenyekiti wa CCM na CCM yenyewe. Je, nani ataondoka kwenye kitanzi hiki na kicheko ama kilio.

CCM na Kikwete wako kwenye kitanzi ambacho ni Chenge na Lowassa huku Chenge na Lowassa nao wakiwa kwenye kitanzi yaani kujivua gamba. Kitanzi cha Chenge na Lowassa kilifanywa kuwa dhahiri na hatari na uamuzi wa Rostam kujivua gamba.

Hivi karibuni “magamba” haya yalisikika yakikejeli miito ya kuwataka waachia ngazi. Bahati mbaya au nzuri, CCM haikutaka kutoa majibu kwa kejeli hizi. Je, huu ulikuwa mwanzo wa CCM kukubali yaishe iishie kulamba matapishi yake na kuendelea kuonekana kama chama cha mafisadi?

Joto la uchaguzi mdogo wa Igunga lilileta nafuu ya muda kwa CCM hata watuhumiwa. Lakini sasa uchaguzi umebakia kuwa historia. Je, CCM itakuja na kisingizio kipi kuacha kuwachukulia hatua watuhumiwa? Je, CCM na mwenyekiti wake wanaogopa nini? Je, wanaogopa yale aliyosema mwenyekiti wa kamati teule ya Bunge iliyomng’oa Lowassa, Dk. Harrison Mwakyembe kuwa kama wasingeficha baadhi ya mambo serikali yote ya Kikwete ingetimuliwa? Je, umma wa Watanzania utegemee usanii mwingine au ukweli kuwekwa wazi kiasi cha yale yaliyofichwa kufichuliwa na wahusika kuwajibika zaidi?

Huo ni upande mmoja wa habari. Je, kina Mwakyembe na spika aliyesimamia uundwaji wa kamati teule ya Bunge, Samuel Sitta wataendelea kuficha ukweli ili waendelee kufaidi ulaji wa uwaziri waliopewa kama fadhila kwa kuikoa serikali? Je, Watanzania ambao, kimsingi, ndio waathirika wakuu wa kashfa hii kutokana na kuwekwa kwenye kiza miaka nenda rudi huku pesa yao ikiendelea kuchotwa kuwalipa wezi wachache wataendelea kuwa mbuzi wa shughuli? Hakika maswali ni mengi kuliko majibu.

Nadhani huu ni wakati muafaka kuwakumbusha CCM na mafisadi kuwajibika maana hawakulazimishwa kufikia uamuzi wa kuvuana magamba. Kuna haja ya wananchi kushinikiza haki itendeke tena haraka sana iwezekanavyo kabla taifa halijaangamizwa na mdudu huyu mchafu wa tamaa, uongo na woga.

Je, watuhumiwa wataiheshimu CCM na kujivua gamba au kuidharau na kuendelea kupeta? Je, CCM itaendelea kuwagwaya na kuendelea kuonekana kama kikaragosi kinachoweza kutishwa na mafisadi wachache? Je, upinzani ulioibua kashfa hii nao utaendelea kuwa kitanda kimoja na CCM ili kuwaokoa mafisadi wake?

Kinachozidi kuiweka CCM pabaya ni ile hali ya mahakama hivi karibuni kuridhia kampuni yenye utata ya Dowans ambayo ilirithi mkataba tata wa Richmond ilipwe tuzo . Wengi wanashangaa uhalali wa Dowans kulipwa mabilioni ya Watanzania. Pia inashangaza ni kwanini serikali iko tayari kulipa kampuni ambayo ni zao la biashara haramu!

Wanasiasa wana kitu kinaitwa presumption- sina Kiswahili chake ambapo husema kuwa kitu chochote hata ni kizuri namna gani kilichopatikana kutokana na njia au kwa kitu haramu nacho ni haramu. Inashangaza kwanini wanasheria wa serikali hawakutumia presumption hii.

Je, hawakujua au walijua lakini kwa vile walikuwa na masilahi kwenye wizi huu waliamua kuuchuna hata kutoa msaada wa kuepuka hili? Maana tunaambiwa Mwanasheria mkuu wa serikali hakuhangaika hata kuweka pingamizi kwenye shitaka husika.

Kitu kingine kinachoshangaza ni ile hali ya wahusika wa Richmond ambayo kimsingi ndiyo Dowans yaani Rostam, Chenge na Lowassa wanashughulikiwa kisiasa badala ya kisheria.

Hii inajenga hisia kuwa kuna wakubwa serikalini ambao wamo kwenye racket hii bila shaka. Je, hawa ni nani? Je, tutayajuawaje majina ya watu hawa iwapo kina Mwakyembe hawataki kuwataja kwa faida zao?

Ajabu nao wanataka kutuaminisha kuwa wanapingana na ufisadi wakati wanaukingia kifua hadi kuufichia siri!

Wengi wanadhani kuwa hawa walioko nyuma ya pazia mmojawapo ni Kikwete. Maana aliwahi kuwahakikishia wananchi kuwa angetatua tatizo la umeme na alikuwa akifuatilia mazungumzo baina ya Lowassa na Richmond.

Na si hilo tu. Kama hana anavyonufaika, ni kwanini hataki kuwashughulikia watuhumiwa vilivyo? Je, Kikwete ana ubavu wa kuwashughulikia Lowassa na Rostam wakati ndio waliomweka madarakani?

Nani mara hii kasahau kuwa, licha ya Rostam kuwa Richmond na hatimaye Dowans ndiye Kagoda wa EPA? Je, kwa Kikwete aliyenufaika na pesa ya EPA anaweza kumkamata mwezeshaji wake?

Je, anaweza kumshughulikia Lowassa naye akawa salama? Hapa ndipo kitendawili cha nini kitatokea kuhusiana na kitendawili cha kujivua gamba kitakapoteguliwa.

Watanzania wengi wangetaka kujua hatima ya nchi yao. Wanataka kujua kama itaendelea kuwekwa rehani kwenye mifuko na mikono michafu ya mafisadi au kurejeshwa kwao.

Kama watafikiri sawa sawa, kadhia ya Dowans-Richmond inaweza kuwa kitufe cha kufyatua hasira zao na kurejesha taifa lao kutokana na wale waliowaamini kushindwa kutimiza wajibu wao na badala yake kuwa washirika wa uangamizaji wa taifa.

Tukubaliane. Kuna ombwe kubwa la uongozi. Tumekuwa na ombwe kubwa kiasi cha kukosa hata utawala achia mbali uongozi. Maana viongozi walikufa zamani. CCM imeshinda ubunge Igunga. Je, itashinda gamba itakapokaa Dodoma au Dar es Salaam au kwingeneko? Time will surely tell. Tia akilini.

Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 18, 2011.

No comments: