MWENZENU ndiyo nimerejea kutoka Igunguli kwenye kampeni za kamupani za uchafuzi wa uchaguzi. Nilikuwa chama gani zaidi ya UNM yaani Ugali Nyama na Maharagwe usiniulize tafadhali. Je, chama change kimepata kura ngapi? Please don’t ask. If you do I shall commit suttee.
Ingawa nimechelewa kutoa tathmini yangu ya uchaguzi wa Igunguli, bado sijachelewa sana. Hivyo ifuatayo ni taarifa yangu na tathmini ya uchafuzi sorry uchaguzi mzima.
Kwanza, Chama Cha Mafisadi kilitembeza pesa chafu hakuna mfano. Ukiachia mbali kuhonga pesa, Chama Cha Mafisadi (CCM siyo CCM chama tawala), kilihonga ubwabwa, gongo hata fulana na kofia. Mtonyaji wangu amenitonya kuwa chama cha wasanii kilitumia zaidi ya madafu bilioni thelathini katika uchaguzi mdogo hivi! Ajabu hawa wanaotapanya pesa kama hizi, wanaendesha kaya isiyo na hata pesa ya kulipia pango la wizara zake! Hebu niulize kwa herufi kubwa.
Inakuwaje wizara inashindwa kulipia pango lake wakati kila bajeti inatengewa pesa ya kufanya hivyo? Au ni yale yale ya kuchukua pesa ya pango na kwenda kujenga mahekalu binafsi.
Kuna mnywa kahawa alisema kuwa hizo wizara furushwa hazidaiwi pango tu bali bili za maji, umeme hata simu. Ajabu wizara hizo hazikosi pesa ya posho ya wakubwa zake, pesa ya kukirimu wageni, pesa ya kupitisha bajeti, pesa ya kuandaa tafrija za kujipongeza na upuuzi mwingine.
Pili, CCM ilitumia vyombo vya dola kama ndata na Uhasama wa Taifa kuhujumu vyama vingine. Hebu uliza yule mama aliyekamatwa akipanga kuhujumu uchaguzi kwa kutumia madaraka yake hadi akanyofolewa mtandio na kukabidhiwa kwa polisi amefanywa nini zaidi ya kungojea kuteuliwa kuwa mkuu wa nkoa? Je, hapa vyombo vya dola la kaya havijatumika kuwabeba wachovu na mafisi na mafisadi? Ndiyo. Hebu jiulize. Kwenye uchaguzi Fanya Fyoko Ukome wa nini? Kwenye uchaguzi bastola kiunoni za nini?
Hamkusikia wahuni wasio na heshima waitwao waheshimiwa walifikia hata kufyatua risasi? Mwenzenu nina bahati tena ya mtende. Si yale mapumbavu na malimbukeni ya silaha yalirusha risasi utadhani mawe! Kama siyo kutumia mbinu zangu za kikomandoo nilizojifunzia Kyuba nilipoarikwa na kugharimiwa na rafiki na komandoo mwenzangu Fidel Castro ningekuwa al marhum wallahi! Una habari risasi moja ilipitia sikioni kwangu na kuangukia pembeni yangu? Hivyo ndiyo ilivyokuwa niaminini.
Ukiachia mbali uhuni na ushamba wa watu wazima, kulikuwa na sakata la ngono nje nje. Ngono zilipamba moto hadi kada mmoja wa chama hicho hicho cha mafisiduni akamkada mke wa kada mwenzake wakafumaniwa. Nadhani kisa cha yule Mchembe Mwingilu hamjakisahau. Aibu sina mfano.
Hawa kweli wanaweza kupambana na ukimwi wakati wao ni wa kuogopwa kuliko ukimwi wenyewe? Achene kupenda chini hata kama mna madaraka ya juu. Mgoni na mzinzi aliyefumaniwa hapaswi kuendelea kuwa madarakani.
Maana atayabaka na kuyanajisi madaraka haya kama anavyonajisi na kubaka wake za wenzake wenye nafasi za chini akitumia madaraka ya juu. Kweli cha maskini huliwa na tajiri! Walijisemea wahenga. Mie nasema wazi. Ukimmendea mshirika wangu wa bedroom navaa bomu na kukulipua kama al Kaidi.
Ukiachia mbali ngono, udini nao haukubaki nyuma. Bila shaka mnakumbuka wale viherehere mashehena waliojiita mashehe wakati si mashehe walivyotishia kumtoa mtu roho eti mkuu wa wilaya alivuliwa hijab wasijue mwezao si dini yao bali mtawala.
Mnaweza kudhani ninawasingizia au kuwakandia na nina chuki za kidini. Hasha. Wako wapi baada ya kugundua kuwa kumbe waliyekuwa wakimtetea si mwenzao? Si wameishia mitini kwa aibu. Watu wengine bwana kupenda kujikomba na kununua kesi. Nani aliwaambia kuwa yule mama ni wa dini yenu wakati ameolewa na mla kiti moto? Achene kudandia mambo dandieni magari. Hayo!
Yaone yanavyotoa toa mimacho. Tumeishawastukia nanyi ni mafisadi mnaotumia dini sawa na wale wanaotumia siasa. Komeni na mkomae nyang’au wakubwa.
Pia kulikuwa na kampeni za uongo mtupu. Nilimsikia mpuuzi mmoja akipanda jukwaani na kusema eti ameleta maendeleo wakati ameleta maanguko. Jamaa mwenyewe wamjua? Si Tunituni aliyeiba hadi migodi na kuuza nyumba za walevi halafu anasema eti hayo ni maendeleo.
Mwe! Njomba hii hunipati na chikuchapoti kwa hili njomba. Huwezi kuamini, Igunguli iligeuka uwanja wa uongo na upuuzi. Hata lile gamba lililojivua hivi karibuni eti nalo lilikuwa likiwahimiza wananchi walisikilize wakati ni jizi la kawaida! Kaya hii! Kweli imegeuka danguro la kila changu wa kisiasa kufanyia ufuska wake.
Ukiachana na uongo, kulikuwa na mashindano ya vyama kama vitatu kuonyeshana utajiri. Vyama hivyo sitavitaja leo. Huwezi kuamini kuwa vilikuwa vikishindana kutua kwa helkopta huku wanaohutubiwa wakiwa maskini hata wasio na makubazi miguuni!
Nani angeamini kuwa wakati wapiga domo walibebwa kwa mahelkopta, kura zilisafirishwa kwa punda na mikokoteni! Akili au matope? Cha muhimu nini kati ya walaji wachache na wababaishaji kibao na kura zenyewe? Hata hivyo siwalaumu. Kwao kula ni bora kuliko kura na kura ikiwa bora basi iwezeshe wao kula. Hizo ndizo siasa uchwara alizosema Roast Tamu bin Gamba bin Fisadi bin Kagoda al Ajemia.
Lol! Nilitaka kutenda dhambi isiyo na kitubio wala msamaha! Wiki iliyopita nilighairi kwenda Mwitongo kumkumbuka Mchonga baada ya kuona wezi, majambazi, wanafiki na maadui zake wakijaza kule kumsanifu eti wakimuenzi. Tangu lini mbwa akamkumbuka samba? Tangu lini juha akamkumbuka mwenye busara zaidi ya kumkumbuka juha mwenzake?
Akifanya hivyo jua anasanifu kama jamaa zangu waliojazana Mwitongo kumsanifu Mchonga. Hata wale walioghushi shahada eti nao walikuwapo! Kweli simba akifa mzoga wake waweza kuliwa na hata panya.
Nitaendelea na tathmini ya uchafuzi mwaka 2015 baada ya kuwachunguza hawa wanaojipitisha pitisha eti tuwachague wakati hawana maana wala udhu.
Naona kali la Mwiguli linaelekea mtaani kwangu. Acha niwahi nikamfumanie na yule mke wa kada mwenzake. Au naye ana powers of attorney kuwanonihino wake za wenzake?
Imetoka hiyo! Ikirudi? Mtajaza wenyewe.
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 18, 2011
No comments:
Post a Comment