Monday, 17 October 2011

Kumbe wanyama ni bora kuliko watanzania!


Tarehe 5 Oktoba vyombo vya habari vilimkariri waziri wa Waziri wa Maendeleo Mifugo na Uvuvi Matayo David akisema kuwa serikai itawachukulia hatua watakaosafirisha wanyama kikatili. Waziri alibainisha kuwa watakaovunja sheria hii ya ustawi wa wanyama watafungwa mwezi mmoja au kutozwa faini kati ya shilingi 20,000 na 100,000. Hiki si kiasi kidogo kwa mtanzania anayeishi kwa kubangaiza kama vile kuchinja kuku na kusafirisha wanyama wake kwenda sokoni.

Inashangaza kugundua kuwa waziri hajui kuwa baada ya kuua Mamlaka ya Reli, watanzania hawana namna ya kusafirisha mifugo yao zaidi ya kuwaswaga na kuwatembeza makumi ya kilometa. Kama wanafunzi wa vijijini wanajiswaga kwenda kurundikana madarasani kama vifaranga huku wakikalia mawe, itashindikanaje wanyama kuswagwa?

Inasikitisha na kufedhehesha sana. Je wanaosafirisha wanadamu kikatili kama wale waliopoteza maisha kwenye meli ya Islander mbona hawakupata kinga hii? Je ni wangapi wanasafirishwa kikatili kwenye dala dala, mlori, na mabasi ya vijini na serikali inaona na kukaa kimya? Kulikoni kujali wanyama na kupuuzia wanadamu?

Je ni watoto wangapi hawana mahali pa kuchezea kutokana na sehemu za wazi kuvamiwa na wezi wachache wenye pesa na ushawishi na serikali ikikaa kimya kwa miongo mingi? Je hawa hawafanyiwi ukatili? Je ni sehemu ngapi za beaches pwani zimevamiwa na vibaka wajiitao wawekezaji na kuzizungushia seng’enge wakiwaacha watanzania wakitamani kwenda kuogelea? Rejea mauji ya Kigamboni ya kijana wa kitanzania yaliyofanywa na mwekezaji uchwara wa kihindi hivi karibuni. Je ni kwanini serikali inaona mateso ya wanyama na kutoona ya watanzania? Je ni watanzania wangapi wanababanishwa kwenye magereza na kutunzwa kikatili wakati serikali ikiangalia?

Japo wanyama wanahitaji kuonewa huruma iwapo wananchi wa kawaida hawaonewi huruma? Nani hajui kuwa watanzania kwa sasa wanaishi kizani kama wadudu huku serikali hiyo hiyo inayohusika na kiza hiki ikiendelea kujifanya kama aihusiki na jinai hii! Kama serikali aihusiki inakuwaje inawavumilia watendaji wabovu kama mawaziri husika wa wizara ya Nishati na Madini au wale wa Wanyama na Utalii?

Ni jambo na kusikitisha na kushangaza kwa serikali inayoruhusu kutoroshwa kwa wanyama wa mamilioni kujifanya inajali wanyama wa kufugwa. Ingawa lengo letu hapa si kutetea ukatili wa wanyama, ila ukiangalia kiwango kikubwa cha utesaji wa wanyama kilichofumbiwa na macho wakati wa kuwatorosha, unashangaa hii huruma, kama kweli ipo, inaanzia wapi na itaishia wapi? Je kuna wafadhili waliolalamikia hili au wanaotaka kutoa pesa kwa serikali hivyo inajenga mazingira ya kujipatia pesa kwa kujifanya inawajali wanyama? Huwezi kuwajali wanyama kabla ya kuwajali watu. Hivi wagonjwa wanolazwa watatu kitanda kimoja au wanafunzi wanaokalia mawe au kwenye sakafu hawafanyiwi ukatili hasa ikizingatiwa kuwa nchi yetu imejaliwa utajiri wa kumwaga ingawa tunautapanya kutokana na upogo na uroho wa watu wachache?

Safu hii huwa haina muda wa kumtetea mtu au kikundi cha watu zaidi ya kumwanga ukweli kama ulivyo hata kama unauma ili wahusika waelewe na kuchukua hatua. Hivyo, tuseme wazi. Badala ya serikali kuja na mipango ya alinacha ya kuwajali wanyama ianze kuwajali wanadamu ambao wamepewa umilki juu ya wanyama.

Waziri Matayo aabiwe bila woga kuwa kipaumbele chake hakina maana iwapo waziri huyo huyo anashindwa hata kuwashauri mawaziri wenzake wanaohusika na utalii kuacha ukatili wa wanyama na wanadamu. Maana unapowatorosha wanyama bila kupitia mikondo ya kisheria, licha ya kuwahujumu watanzania, unawaongezea umaskini ambao mwisho wake ni ukatili kutokana kushinda wakihangaishwa na maisha wasipopaswa kufanya hivyo.

Serikali yetu ni ya ajabu wakati mwingine. Hebu tutoke nje ya mada kidogo. Nani amesahau ilivyoweza kuandaa uchaguzi mdogo wa Igunga kwa kuweza kusafirisha wapiga kampeni kwa helkopta huku kura zikisafirishwa kwa punda na baiskeli. Hii kweli ni akili? Nani hajui kuwa kuna vyama vimetumia mabilioni ya shilingi yakatwayo kwenye kodi za wananchi maskini kwenda kuwapigia kelele na wengine kuzini na wake zao? Nani hajui kuwa pesa nyingi imetumika kuwarubuni wananchi ili mtu wa chama apite na chama kiendelee kuzoa ruzuku huku wananchi wakiendelea kusota? Je hawa na wanyama ni wapi wanapaswa kuonewa huruma kwanza?

Hivi nani hajui kuwa wananchi wa Igunga wametapeliwa mchana kweupe? Kwanini wasitapeliwe iwapo tunaambiwa waliojiandikisha kupita kura walikuwa zaidi ya 150,000 lakini walipiga kura ni theluthi moja, kwanini? Je waligundua baadaye kuwa ulikuwa ni upotezaji wa muda kwenda kupiga kura wakati maisha yao hayabadiliki kama ya wanyama? Imebidi tuunganishe kisa hiki na hiki cha wanyama kuonyesha jinsi vipaumbele vya serikali yetu vilivyo vya hovyo.

Leo waziri anapata jeuri ya kutangaza hadharani kuwa atakayewatesa wanyama atatoza faini au kufungwa huku waziri huyo huyo akishuhudia wamachinga wakiteswa na wezi wa baadhi ya halmashauri za miji. Waziri huyo anajua fika kuwa wakati wamachinga wapiga kura wakinyanyaswa, kuna wamachinga toka ima India au China wamejaa kwenye miji yetu wakilindwa na serikali hiyo hiyo inayovunja sheria kuwaruhusu wafanya umachinga wakati sheria hairuhusu. Je haya hayafanyiki? Kama ni kutimiza wajibu na kutekeleza sheria basi serikali ifanye hivyo bila kubagua wala kuendekeza pale kwenye maslahi yake tu. Hii nchi ni ya wananchi wote hata kama hawana sauti wala mamlaka zenye uzalendo za kuwatetea. Ni aibu kufikiri kulinda haki za wanyama kabla ya kuanza kulinda za wanadamu.

Chanzo: Dira Oktoba 17, 2011

No comments: