The Chant of Savant

Thursday 13 October 2011

KUMBUKUMBU MAALUM YA MWALIMU NYERERE


Mwalimu Nyerere sikia

Mpendwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere baba wa taifa letu,

Naadika ujumbe huu kwako maalum nikiamini kuwa utausoma na kuwasomea mashujaa wenzako kama vile Edward Sokoine, Horace Kolimba, Jenerali Imran Kombe na wahanga wengine waliouawa na watu wachafu wenye chuki na yale yote uliyopigania, kusimamia na kutekeleza.

Mwalimu,
Leo ni siku maalumu kwa wapenda haki nchini na duniani. Kwani ndiyo tunaadhimisha miaka 12 ya kifo chako. Ingawa kimwili hatuko nawe, kiroho tuko nawe. Ingawa miaka 12 inaweza kuonekana mingi. Sisi wapenzi wako tunaona ni kama jana ukiachia mbali mateso kutufanya tuone kama ni karne moja imepita baada ya kurudishwa nyuma kwa mamilioni ya miaka. Najua mwalimu kuna mengi yametokea ambayo huyajui. Yapo ya kuudhi na kufurahisha.

Cha mno ni kwamba kile Chama chako ulichokiasisi na kukifanya kiwe kipenzi cha watanzania ni kama kiko ICU kikipumlia mashine tayari kwa kukata roho wakati wowote. Hakipendwi tena wala kuheshimika. Kila mtu anajisemea na kujifanyia atakavyo kana kwamba hakuna mwenye nyumba. Wale mafisi wenye uchu wa pesa uliokuwa ukipigana nao vita sasa wameshika kani kama alivyowahi kuseme Profesa Issa Shivji. Wezi siku hizi wanaitwa wafanyabiashara maarufu huku mafisadi wakiitwa magamba ya nyoka. Ni juzi juzi kimetoka kwenye uchaguzi na ushindi wa aibu. Hakiitwi cha mapinduzi bali majina mengi ya ajabu ajabu. Mara wakiite chama cha magamba, maangamizi, mafisadi, wauzauza na mengine mengi.

Mwalimu, katika hili la magamba, hata yule jamaa uliyemtolea uvivu kuwa alikuwa amejilimbikizia mali nyingi za wizi yumo. Kwa sasa yumo msambweni kuvuliwa kama gamba ingawa anasitasita. Hayuko peke yake. Wapo wengine kama vile Andrew Chenge na Rostam Aziz ambaye amejivua gamba siku za hivi karibuni ingawa kwenye ulaji hajavuliwa. Umma unatamani ungekuwepo uwatimue kama mbwa au kuwapa vipande vyao kama ulivyowahi kumpa jamaa mmoja uliyemuita mhuni. Maana hali ilivyo ni kwamba kuna watu wanasitasita sijui kwa kuwaogopa wasitaje uchafu wao. Sijui ni kwanini, ambao wanamwambia leo toka na kesho wananywea kama hamna namna nyuma ya pazia?

Mwalimu, unakumbuka? Siku hizi uadilifu na maadili ulivyokuwa ukipigania na kusisitiza hakuna. Kuna ubadhilifu badala ya uadilifu na madili badala ya maadili. Mambo yamezidi kuchacha. Nakumbuka mpendwa mkeo mama Maria hakuwa na shea kwenye uongozi wako. Siku hizi ni tofauti. Kijana wako Yoweri Museveni siyo yule mwanampinduzi wa zamani. Ni king’ang’anizi na dhalimu hakuna. Una habari yeye na rais wa Malawi Bingu wa Mutharika wameishawateua wake zao kuwa mawaziri? Najua hutaamini lakini hivyo ndivyo hali ilivyo.

Mwalimu,
Nakumbuka mkeo hakuwa na ASIZE. Usiniulize Asize na ugonjwa au mnyama gani. Ni vifaa fulani watumiavyo wake za wakubwa kukusanyia pesa na kuchuma utajiri kupitia migogoni mwa madaraka ya waume zao. Una habari mwalimu? Siku hizi yale madini uliyokuwa umekatalia kuchimbwa yamegeuka balaa badala ya Baraka. Watu walioko kando kando yake wamegeuka watumwa na wageni katika nchi yao. Wanazuiliwa kupita karibu na machimbo ili wasiibe madini na wakipita wanapiga risasi. Mazingira ndiyo usiseme. Mito imechafuliwa na mashimo makubwa yamechimbwa kiasi cha huko tuendako kuwa jangwa kama hali haitabadilika. Nani aibadilishe?

Mwalimu,
Kile chama alichoanzisha Gavana wako wa benki kuu Mzee Edwin Mtei kiitwacho CHADEMA kama ulivyokitabiri kinaanza kuonyesha makali kiasi cha kukubalika nchini hakuna mfano. Kimeishafichua ufisadi ambao ulifikia mahali pa kutishia kuiangusha serikali hadi waziri mkuu Edward Lowassa akatimuliwa. Najua mwalimu unamkumbuka mtu huyu ambaye ulimsemea mbaya alipokuja Msasani kutaka Baraka zako ili agombee urais. Ulisema wazi kuwa wengine wananuka na wamejilimbikizia mali za wizi. Rafiki yako Lowassa alitimuliwa na kashfa iliyoiacha nchi kizani huku ikipoteza mabilioni ya shilingi. Mpaka ninavyoandika, kampuni hii iliyojivua gamba na kuvaa jingine kwa kujiita Dowans inakaribia kufilisi nchi yako. Maana mahakama juzi iliipa tuzo la kusababisha kiza la shilingi 111,000,000,000.

Kitu kingine mwalimu, mambo yamebadilika sana. Serikali imefilisika huku watu binafsi wakitajirika. Unaweza kuamini kuwa kuna wizara zimeishafungashiwa virago na kutupiwa vitu nje kwa kushindwa kulipa pango la nyumba zile ulizotaifa? Hizi ni zile zilizonusurika kuuzwa na kijana wako Ben ambaye baada ya wewe kufa aligeuka na kuwa kituko cha mwaka. Huwezi kuamini kuwa alipokuwa akiondoka madarakani alifikia hatua hata ya kujiuzia mgodi huku akigeuza ikulu yako pango la wezi na wanyang’anyi. Siku hizi yupo yupo tu na haonekani kutokana na watu kutokuwa na hamu naye.

Mwalimu,
Itakuwa ni utovu wa nidhamu kumaliza waraka huu bila kukupa habari mbaya za kifo cha swahiba yako Simba wa vita. Alikuwa miaka miwili iliyopita akiwa amesononeka kutokana na kuona machukizo yakifanyika mbele za macho yake. Halafu mwalimu, unamkumbuka yule tapeli mmoja wa Magomeni karibu na nyumba yako ya zamani aliyejiita mtabiri? Jamaa aliharibikiwa akaanza kutabiri maafa hatimaye yakamkumba yeye. Ajabu alipokuwa akitabiri upuuzi wake hakuna aliyekuwa tayari kumkabili na kumnyamazisha. Kitu kingine mwalimu, siku hizi biashara ya uga imekuwa kero kwa taifa. Huwezi kuamini kuwa kuna hata viongozi wa kidini na wa kiserikali wanafanya biashara hiyo. Haya si maneno yangu. Ni maneno ya rais Jakaya Kikwete. Nadhani mwalimu unamkumbuka. Ni yule kijana uliyemwambia mwaka 1995 kuwa asubiri akomae aongeze nchi. Kwa sasa ndiye rais.

Mwalimu nadhani unamkumbuka kijana wako Samuel Sitta. Miaka michache alichaguliwa kuwa spika wa bunge na kufanya mapinduzi yaliyosababisha Lowassa auteme uwaziri mkuu baada ya kuteuliwa huku kukiwa na shinikizo la kutaka rais asimteua kwa vile ulivyomuacha unajua na wananchi wanakumbuka. Hakudumu. Uliyosema hayakukawia. Yalijitokeza na jamaa akajikuta anatupwa nje kwa aibu huku mkewe akiangusha chozi kama kichanga. Hayo tuyaache mwalimu.

Mwalimu kuna mengi ya kukwambia ila nafasi haitoshi. Nimalizie kwa kukutaarifu kuwa siku hizi uongozi haupatikani kwa ambaye hana pesa wala jina kubwa au kuwa mtoto wa wakubwa. Hiyo ndiyo hali tuliyo nayo watu wako tunaoendelea kukumbuka na kuteseka hasa kwenye kiza na ufisadi.

Naomba nimalizie hapa kwa kukutakia mapumziko mema ya milele.

Chanzo:Dira Oktoba 13, 2011.

2 comments:

Profee said...

Nimezikubali hizo contents kaka,kama vipi pitia www.TanzaniaKwetu.com ili usajili blog yako kule,pamoja sana kaka!

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Sijui mnavyosajili blog hivyo nipe nuggets