Wednesday, 26 October 2011

Badala ya kujivua gamba Ewassa amejivua nguo


INGAWA amejitahidi kula kobisi, kwa wale wenye kufuatilia mambo watakubaliana nami kuwa Eddie Ewassa aliyependa kujionyesha kama kidume kumbe ni mwoga.

Jamaa si alitupata wanywa kahawa lilipopigwa talalila kuwa angefanya kweli na kutoa somo kwa dunia tusijue atageuka mwoga!

Tukiwa hatuna hili wala lile si wambea wakatangaza kuwa Ewassa angeitisha kigwena na kumwaga mtama kwa kuku ili watafune! Usiambiwe! Kila mnywa kahawa na mlevi alijiweka tayari kupokea ufunuo huu wa kumwaga mtama.

Mpayukaji kama ada nilinunua kabrasha kubwa tayari kuchoronga yote ambayo yangenenwa na kigogo huyu.

Wengi tulijiandaa hata kumuuliza maswali mazito juu ya mambo mazito na tuhuma nzito. Wapo waliojiandaa kuzomea zomea huku wengine wakijiandaa kwenda kwake kujipendekeza ili awape mshiko kama ilivyotokea kwa wasomi uchwara hivi karibuni. Jamani kujigonga kwa fisadi ni uchangudoa wa kimaadili hata kama wahusika wanaona ni dili.

Hauchi hauchi kuchile. Kule Richmondoli nyasi zilitandazwa tayari farasi kufungiana nyama na nyangwa. Saa ilipowadia tukamuona jamaa akiingia ukumbini na waramba viatu wake kina EF. Kibondemaji na Kayaanda waliokuwa wakihanikiza kwenye runinga kutukana watu kwa vile eti wanamsakama mungu wao.

Huku viroho vikitweta na kijasho chembamba kikituchuruzika tayari kusikia yasiyosikika jamaa si alianza sanaa .

Hatukuamini masikio yetu kutokana na yale aliyoanza kusema. Ilibidi tuvumilie maana mvumilivu hula mbivu ingawa wakati mwingine aweza kuambulia mbovu kama sisi.

Wajua nini? Badala ya kumwaga mipwenti si alianza kumsifia mshikaji wake wa barabarani wa Chama Cha Mafisadi (CCM), Sio CCM unayoijua, hii ninyine kabisa. Wengi hatukuamini macho na masikio yetu.

Tulizidi kuvumilia tukifiri kuwa yale yalikuwa maroroso na makando kando ya kutuandaa tayari kupokea injili. Hola! Jamaa alizidi kujiweka karibu na mshikaji wake hadi muda ukazidi kuyoyoma huku mie nikitamani niamke nimwulize swali baya.

Jamaa aliendelea kujivua gamba kiana katika kila mstari aliosoma toka kwenye hotuba yake uchwara. Mara aseme, “ sie ni damudamu na hatukukutana baharini wala relini. “Mara wanatuzushia kuwa sisi si wamoja na ulaji wetu si mmoja. Mara namheshimu na kumhusudu Njaa Kaya. Mara hivi mara vile.

Nilitamani nimwambie akajiunge na akina Isha Mashauzi na Hadiji Kopo akaimbe mipasho badala ya kujiita mwanasisasa. Maana maongezi yake haikuwa siasa bali mipasho tena mipasho kwa Nepi Nnaunge.

Wengi walianza kujiuliza nani kamroga huyu. Utadhani alikuwa ameambiana na habithi Kashafi wa Libia aliyekuwa akijidanganya na kuudanganya ulimwengu kuwa walibia walikuwa wakimpenda hadi kumfia asijue wakimpata wanampiga hadi kumdedisha kama ilivyotokea.

Hakuna aliponiacha hoi pale alipojua ukweli mchungu pale walipomtia mbaroni na kuanza kuzoza akiuliza eti alikuwa amewakosea nini NTC asijue walibia walijua kila janja na ukatili wake. In the end walimdedisha kwa kichapo cha mwizi.

Tuendelee na huyu, kusema ukweli hajarogwa. Kama niliyosikia ni kweli basi nasikia anasumbuliwa na Richmonduli.

Wapo wanaosema eti alilaaniwa na mzee Mchonga pale alipomtolea uvivu. Iwe kweli au la mie simo. Tuendelee na stori zake. Kadili alivyozidi kuchafua hewa kwa mipasho uchwara tulizidi kukodoa mimacho huku mshawasha na hamu vikizidi kuongezeka jamaa asiongee hata pwenti moja!

Wenye akili tukajua tumeingizwa mkenge kuletwa kusikiliza rongorongo za mfa maji. Kwa ufupi ni kwamba jamaa tuliyetegemea ima avue gamba au kumkaba mtu shati si aliishia kujivua mwenyewe na kubaki kama alivyozaliwa kiakili!

Tafsiri ya haraka iliyonijia ni kwamba jamaa alikuwa anaandaa mazingira ya kujivua gamba kwa kujionyesha ana heshimu genge lao.

Najua. Siku ya kufanya kweli atasema, “kwa kuheshimu genge na mwenyekiti wake, ingawa sikutenda kosa lolote, nimeamua kujivua gamba ili kuleta mshikamano wa genge.” Wengi wataguna. Jamaa hatajali miguno. Badala yake atabwabwaja sifa za genge lililomlea na kumpa ulaji hadi akawa mkwasi.

Kama haitoshi, wenzake watatuma salamu za pongezi kwa kuonyesha ukomavu wa kisiasa na uzalendo. Ebo, wengi wataguna. Uzalendo gani wa kuleta Richmonduli?

Hata hivyo, radio mbao zimenitonya kuwa alikuwa ana usongo wa kumwaga mtama lakini akiwa amebakiza dakika tano na ushei simu ilipigwa toka Vigogoni kumuonya kuwa akimwaga mtama atashughulikiwa kwa kupelekwa mbele ya pilato.

Nasikia simu ilitoboa wazi kuwa Ewassa anapaswa kujua wazi kuwa ana kigwena ingawa wameamua kumnyamazia. Jamaa kusikia hivi, nasikia alianza kunonihino kwa presha.

Naona gari lile kama la fisadi linakuja, acha niwahi nikalimwagie maji machafu.

See you guys!
Chanzo: Tanzania Daima Oktoba 26, 2011.

No comments: