Friday, 21 October 2011

Watawala wetu na ufisadi wa kielimu


Zamani shahada ya heshima haikutolewa hovyo hovyo. Siku hizi, hata hivyo, rais wa nchi anaweza kupewa shahada kama njugu kiasi cha maana ya kusoma na shahada husika kupokea. Ajabu ya maajabu rais anayepewa shahada za heshima hupenda kuitwa daktari utadhani kasomea! Hii matokeo yake ni kuzuka kwa madaktari wa kughushi wengi sawa na waganga wa kienyeji. Tumefikia mahali kuwa na mawaziri walioghushi shahada za udaktari huku rais akiwafumbia macho. Je atawezaje kuwashughulikia iwapo gonjwa lao la kupenda sifa hata wasipostahili ni moja?

Vyuo vyetu vikuu vimeanza kugeuka vyoo vikuu. Maana vinatoa shahada bila kufuata hata vigezo wala utaratibu. Inakuwaje mtu mmoja hata kama ni rais kupewa shahada za juu za heshima karibu kila mwaka na kusiwepo kuvunjwa taratibu? Je ni kwanini vyuo vyetu viko tayari kupinda kanuni na kujishushia heshima kwa kutoa shahada kama njugu.

Hapa Kanada mkuu wa nchi ni Malkia Elizaberth anayewakilishwa na Governor General of Canada. Sikumbuki kusikia au kuona malkia au mwakilishi wake hata waziri mkuu wakigawiwa shahada. Je kwanini watawala wetu wanapenda shahada za dezo?

Watafiti tafitini mjue chanzo cha ugonjwa huu. Je yaweza kutokana na wakuu wengi wa vyuo kuwa marafiki na wateule wa rais au rais anatumia watu wake kulazimisha apewe shahada kama njugu? Hakika huu nao ni ufisadi wa kielimu.

No comments: