MPENDWA Anna Makinda Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Samahani sitakuita Anne kama unavyopenda kuitwa nikizingatia kuwa wale waliozaliwa wakati wakao walikuwa wakipewa majina bila kutumia manjonjo ya kiingereza.
Ndiyo maana watu wa umri wako ni akina Katarina siyo katheleen au Josephina siyo Josphine nakadhalika.
Kwa mara ya kwanza nakuandika barua hii ingawa si mara ya kwanza kukuandika tena kwa kukuchambua siyo kukupongeza.
Nimewahi kuandika mara nyingi juu yako. Mfano, kukaripia pale ulipomnyamazisha mbunge wa zamani wa Arusha, Godbless Lema alipodai kuwa waziri mkuu ni muongo. Ulijua hoja yake tena bila staha.
Katika hili niliandika pia kukulaumu kwa kuburuza Bunge na kuwafanya wawakilishi wa wananchi kama watoto wa shule. Hilo lilipita ingawa nilidhani ungenijibu kama siyo kutoa angalau maelezo yanayoingia kichwani. Lakini hukufanya hivyo.
Pia nimewahi kuandika kukutaka ukanushe kuwa wewe si chaguo la mafisadi hasa baada ya kutokea uvumi kuwa wakati akienguliwa mzee wa viwango Spika aliyekutangulia Samuel Sitta, ulipitishwa na mafisadi ili kuepuka kurudiwa kwa kile kilichomng’oa waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa. Bahati mbaya hukujibu wala kukanusha.
Niliwahi kukuandika nikikushutumu kutumiwa na muhimili mmoja wa dola yaani utawala kinyume cha maagizo na kanuni za mgawanyo wa madaraka (separation of power) na utawala bora (good governance). Kadhalika, hukukanusha wala kujitetea.
Niseme ukweli nilitokea kutokupenda achia mbali kukuheshimu. Pamoja na mapungufu yako yote niliyowahi kuelezea kuanzia kutokuwa na elimu ya sheria wala uwezo wa kuliongoza Bunge, juzi ulinifurahisha kiasi cha kuandika waraka huu wa kukupongeza.
Nakupongeza kwa mambo makuu mawili kumruhusu Naibu wako Job Ndugai kuwatolea uvivu wabunge akisema kuwa baadhi yao wanaingia bungeni wakiwa wanatoka kuvuta sigara mbali mbali (ambazo zilitafsiriwa kama bangi au sigara kubwa na kunusa vitu vingine ambavyo wengi tulitafsiri kama unga au madawa ya kulevya. Ulitumia njia nzuri kwa vile Ndugai ni mwenzao anawajua nani anavuta au kunusa nini ukiachia kumchukua au kuchukuliwa na nani.
Uzuri wa sakati hili kuonyesha kuwa ni kweli hakuna mbunge hata mmoja aliyejitokeza kukanusha hata kulaani. Nakupongeza kwa hili na Ndugai pia ingawa sikubaliani naye kuhusiana na kauli yake kuwa hajui idadi ya watoto alio nao.
Hili lilimwonesha kama mtu asiye na maadili kwenye ndoa na familia yake maana yeye kwa dini yake haruhusiwi kuwa na wake wengi. Alisema hayo alipokuwa akihojiwa na kituo cha Televisheni kimoja hivi karibuni. Hili tuliache si hoja ya leo.
Pili, ulikaririwa ukiwapa nasaha wabunge wa viti maalumu kuacha kubweteka na kuuchapa usingizi wa pono na kuridhika na viti hivyo ambavyo ulisema vinawadhalilisha. Wengi wanaona ushauri huu kuwa wa kinafiki kwa vile nawe ulipata usipka kwa njia hiyo hiyo ingawa ulipigiwa kura.
Hili nilishaliandikia sana. Ni ukweli usiopingika kuwa umma unawaona wabunge wa vitu maalumu kama wanyonyaji na mizigo kwa mlipa kodi. Imefikia mahali wanaitwa misukule! Unawaona hivyo kutokana na ukweli kuwa hakuna wanayemwakilisha bali jinsia zao. Maana kama ni kusema eti wanawakilisha wanawake, ni uongo.
Maana wanawake wanaume watoto na watanzania wote wanawakilishwa na wabunge wa kuchaguliwa majimboni. Ingekuwa wabunge husika wanawakilisha wanaume tungesema wanawake wanahitaji wawakilishi.
Dhana hii imefanya baadhi ya watu kuviita viti maalumu astagffirulah, viti vya chupi. Kuna udhalilikaji kama huu? Wengi wanahoji wanamwakilisha nani bungeni iwapo wanawake sawa na wanaume wanawakilishwa na wale waliowachagua?
Pia ukiangalia mizengwe inayotumika hata rushwa kuwapata wabunge hawa unaishiwa imani na ushawishi nao. Nani anapinga kuwa kupitisha hadi kuchaguliwa hugubikwa na vitendo vya rushwa kama ilivyowahi kudaiwa huko Mbeya miaka mitatu iliyopita kuwa wanawake wanatakiwa rushwa ya ngono ili kupitishwa? Nani alikanusha tuhuma hizi?
Hata ukiangalia chimbuko la viti hivi unagundua kuwa ni udhalilishaji mtupu. Chini ya mfumo kandamizi wa chama kimoja, baada ya kugundua wingi wa wanawake kama wapiga kura, chama kiliwatengea wanawake na vijana nafasi za kuwadhibiti na kuwafuatilia huku wakichongeana na kuchukiana ili wasitishie maslahi ya wanaume.
Hata ukiangalia waliokuwa wakichaguliwa katika nafasi hizi ima walikuwa wake wa wakubwa, nyumba zao ndogo (hasa pale wanawake wasioolewa walipopitishwa kirahisi na vyombo vya juu vya chama) au waliojipendekeza kwa chama.
Kimsingi, wanawake na vijana walipewa viti vya upendeleo ili wavigombee na kusahau kugombea nafasi nyingine zilizokuwa zimemilikiwa na wanaume. Hii ilikuwa ni sawa na kuwapa mbwa mfupa halafu ukaiba kwenye lindo lao. Bahati nzuri Makinda umewahi kuingia kwenye mikiki ya kugombea ubunge jimboni na ukashinda. Hivyo, unaongea kutokana na uzoefu usioweza kutiliwa shaka.
Kwa ufupi viti maalum ni udhalilishaji na utekemezi visivyo kifani. Kwa maana nyingine wanaovipenda na kuvitegemea licha ya kujidhalilisha, wanaonesha kuwa ni watu tegemezi wasio na ubavu wa kwenda majukwaani kupambana na wanasiasa wenzao.
Kuhusu la wabunge kuvuta na kunusa vitu vinavyodhaniwa kuwa mihadarati, hili nalo si jambo jepesi. Kuna haja ya kuunda utaratibu wa kuwachunguza wabunge walevi wa aina yoyote ili waumbuliwe na wale waliowachagua wawajibishe kwenye chaguzi zijazo. Huenda hii ndiyo sababu kubwa ya kufanya baadhi ya wabunge kulala lala hovyo bungeni.
Kwa ufupi, nakupongeza Makinda hata kama sikubaliani nawe kwa mambo mengi. Kwa ujumbe huu mfupi, naomba niishie hapa nikikushauri ubadilike na kuwa spika wa viwango.
Kila la heri na pongezi kwa mara ya pili. Wako akukosoaye ili ujirekebishe na kuepuka aibu.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 15, 2012.
No comments:
Post a Comment