The Chant of Savant

Wednesday 22 August 2012

Kumbe na waheshimiwa wanakula kaya!


Walianza na kashfa ya kulala mjengoni huku wakilipwa posho ya kuuchapa, wakaona haitoshi.Wakaja na madai ya kuongezewa posho ya makalio, wakaona hii haichangamshi. Maana walevi licha kushangaa kuwa makalio nayo yanalipwa posho waliona kama wizi na ujambazi wa kutumia madaraka badala ya bunduki.Walikuja na kashfa ya kula rushuwa wakaona hii cha mtoto.Sasa wamekuja na kubwa ya kuvuta sigara kubwa na kunusa bwimbwi. Haya si maneno yangu. Ni maneno ya naibu wa Microphone Johab Ngudai.
Mama Microphone bint Speaker Annae Shemamba Makida Makida ambaye inaelekea anatoka ukoo wa mgosi Machungi Shekiango naye amekuja na mpya yake. Aliwapasha wale wabunge wa underwear au misukule akiwataka watoke usingizini na kuingia kwenye kimbembe cha kugombea kura za kula badala ya kutegemea nonihino zao ingawa naye aliupata uspiika kwa njia hiyo hiyo ya nepi. Leo hili siyo hoja, another day.
Turejee kwa wala majani. Kama wao wanavuta mibangi na kubwia bwimbwi kwanini wasiuze hiyo midudu? Kumbe ndiyo maana wameshindwa kuondoa biashara ya mibwimbwi kwa vile wanauza na kubwia? Ila sisi walevi tukujivutia vijibangi kidogo ndata hao na kiherehere chao. Badala ya kuwasumbua wala bwimbwi wanaojipa raha kama w alivyoshauri mkuu wa kaya, kawakamateni hao wanaokula vvyote, bwibwi, majani na kodi zenu. Wala unga hawamwibii mtu. Siyo kama hawa wanaosema nipe kura yako nikuibie kula yako. Kama nyinyi kweli walume si mkavamia mjengo na kuwatoa nje mkiwa mmewafunga pingu na uhishimiwa wao? Juzi mlimuogopa yule mla rushwa Ommy Badwell. Nyinyi na Takokuru hamna maana kabisa. Nawaona kama vibaka mliojivalia magamba. Lakini siyo kosa lenu bali kaya yenu. Maana kwa masikio yangu juzi nilimsikia mkuu mwenyewe mzee wa sanaa Njaa sorry simalizii, akimtetea mzee wa Vijisenti Endelea Chenga kuwa wainglishi waliomchunguza na kukuta kuwa alikwapua eti walikosea tena kuchapisha. Huyu jamaa naye kweli mpuuzi. Yaani jitu zima na kubwa lenye cheo kikubwa linadanganya kitoto! Mwe! Tumekwisha kama wakuu wetu ndiyo hawa!
Kaya yetu haishi vituko. Juzi nilitaka kujinyotoa roho kama siyo bi mkubwa kunibembeleza kuwa nikifanya hivyo atabaki mpweke. Kwa hiyo wapenzi wa mipasho na kijiwe mshukuruni huyu bi mkubwa maana ningejinyotoa roho msingepata mtetezi wala mpashaji wa hawa wala majani. Basi mpigieni makofi tafadhali huku mkijipanga kuwapiga makofi wala majani na wabwia unga wanaokula kodi zenu. Wajua kwanini nilitaka kujinyotoa roho? Si pale yule jambazi Koshita Muhalu aliyeiba njuluku kule Urumi akiwa sijui balozi sijui mwakilishi alipoachiwa na pilato. Jitu linaiba mifweza tena kwa mabilioni, linafunguliwa kesi uchwara halafu wanasharia wa lisirikali wanafanya mchezo mchafu linashinda na kulipwa pesa ya wale wale lililowaibia. Tunakwenda wapi? Mapilato wetu nao wamegeuka kama vyangu. Leo wanatishwa na lisirikali wanatoa hukumu za ajabu ajabu. Hamkuona walivyowahujumu matabibu na wapiga chaki?
Anyway, leo hayo siyaongelei. Nitaongelea hili la wahishimiwa wa mjengoni kuvuta mibangi na kubwia miunga. Hivi mlitegemea nini kutoka kwa watu waliopata uhishimiwa kwa njia ya rushwa, kuchakachua au chupi? Hivi kama tunafanya uchunguzi wa walioiba kura za kula au kuhonga na kuchakachua si mjengo utabaki na miviti tu? Hawa wavuta wabangi wanaowakilisha matumbo yao wanapaswa ima wakimatwa wanavuta mibangi wafikishwe kwa pilato ingawa mapilato wamegeuka kuwa voda fasta au watunge sheria ya kuruhusu watu kujivutia mibangi na kubwia miunga ili bei zake zishuke nasi tufaidi. Kumbe ndiyo maana wawekezaji sorry wachukuaji wanaiba kwenye kaya utadhani shamba la bibi tena bibi mwenye chizi na kipofu! Sasa kama wahishimiwa wanaingia mjengoni wakiwa wamevuta mibangi mnadhani watashindwa kuwa na mawazo ya kibangibangi? Tena nakumbuka mmoja niliyekuwa nikimjua anavuta bangi akiwa mjengoni ingawa alisharudisha namba mwendazake. Wajua nani huyu? Mtoto wa njini msiseme dito.
Kwa utaalamu wangu wa madawa niliosomea kule Ujerumani nikapata shahada ya PhD in Medicine isiyo ya kughushi kama za akina Buttoks Masaburi, Makorongo Muhanga, Meli Nyago, Doedodos Kamaliza na wavuta bangi wengine. Nakuta kuwa ndiyo maana wahishimiwa wanapenda kulala mjengoni. Hii ni kutokana na kile tunachokiita kitaalamu effects of consuming and abusing and overusing and nonihono drugs and bwibwiz. Nadhani jamaa zangu akina Stivi wahasira na Joni Kombahaha mnanipata. Maana nyinyi kwa kuchapa usingizi mjengoni utadhani baby aliyezaliwa jana au nyoka aina ya kifutu! Hata mgoshi Machungi aliwahi kuniambia kuwa yule mzee wa Kisambaa nadhani mwamjua aitwaye Jose Makambale alikuwa anakula ndumu ndiyo maana alikuwa akipayuka hovyo hovyo. Inawezekana hata huyu jamaa Njaa Kaya mwenyewe anaweza kuwa anakula majani maana ile anguka anguka sieewi eewi. Anyaway nitamuuliza mgosi Machungi wa Kiango aniambie tena. Sasa jamani kama watunga sharia tena wanaoitwa wahishimiwa wanakula mijani na kubwia mibwimbwi hao watoto wetu mashuleni si wataogea? Au ni kwa vile wengine wanaokula mibangi na kubwia mibwimbwi wakizaa watoto na watoto wanakuwa wameishaathirika na mibwimbwi yao? Ndiyo maana mnawaona mitaani wanatembea matako nje na kujichorachora kila upuuzi huku wakiimba nyimbo za vurugu na kelele au al maarufu rafu.
Mie kuna kipindi nashindwa kuwatofautisha kati ya walaji na wapingaji. Maana nao ukisikia mikakati yao utajua kuna ukombozi. Badala ya kuleta mageuzi wanaleta mashauzi. Maana tangu waanze kupiga mikelele yao mara tutaandamana mara tutateka kaya mara tutapinga lile kumbe nao wanavuta mibangi! Mbona wahishimiwa wa upingaji hawakulaumu wala kukana kama nao hawali hiyo midude? Mimi nilishangaa kusikia eti Chakudema inadhaminiwa na gabacholi wa chama magamba. Hivi huu siyo uamuzi wa kibangibangi? Mtu unapinga chama chake halafu eti anajifanya anaku-love. Kama anawa-love si ajiunge na nyinyi? Au ni kwa vile anajua kuwa wote ni walaji tena wa majani na bwimbwi? Tusipoangalia mtatuingiza mkenge na kuiteketeza kaya yetu. Jamani tisiogopane. Lazima tiambiane ukwei, wapingaji nanyi mnaboa ingawa mchango wenu ni mkubwa lakini siyo kama inavyotakiwa. Tusilamu wapingaji peke yao. Hata walevi mnaboa kwa ujuha wenu wa kuwa watazamaji wakati kaya yenu nanyi mkiliwa tena mc hana kutwa.
Juzi nilisikia eti al Shabib wameishaanza kuwekeza mipesa ya uharamia kwenye kaya yenu ili baadaye wagombee urahisi. Aka! Mie simo! Acha nikambomu huyu mhishimiwa kipisi cha bangi kabla hajaingia kwenye mshangingi wake. Na ndata yule naona anatunyemelea kumbaff. Ngoja nione kama atatukamata wote ili kiumane kudaaadeki.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 22, 2012.

No comments: