The Chant of Savant

Thursday 30 August 2012

Matonya: Kioo cha jamii iliyoharibikiwa


INGAWA marehemu mzee Paulo Mawezi almaarufu Matonya anaingia kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kwa kile Waingereza waitacho ‘the whole wrong reason’, ameacha somo kubwa kwa wenye kufikiri.
Taarifa zilizotufikia ni kwamba mzee huyu maarufu kama alama ya umaskini na ufisi wa taifa letu amefariki dunia. Mzee huyu mwenyeji wa Dodoma alikuwa kivutio kwa wengi jijini Dar es Salaam ambako yalikuwa makao makuu ya shughuli zake za kuomba.
Kipindi fulani alimtoa jasho Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam wa wakati ule, Yusuf Makamba alipomwamuru ahame na kuachana na shughuli za kuomba kwa sababu alikuwa akilidhalilisha taifa. Matonya hakukubali ‘kufa kibudu’. Alipambana na Makamba hadi kumtishia kuwa angemng’oa kwenye nafasi yake. Kwa wenye kuuona ukweli, Matonya alikuwa bora kuliko Makamba. Kwani imeandikwa kuwa ajikwezaye atashushwa na asiyejikweza kupandishwa.
Sababu kubwa aliyotoa Matonya ni kwamba, akina Makamba walikuwa walafi wanaokula kwa mikono na miguu bila kunawa huku wengi wanaowanyonya wakiangamia. Matonya aliwaona akina Makamba kama ombaomba waliojisahau hadi kujipa haki ya kuwafukuza wenzao. Matonya aliomba na kuwafikishia mke na watoto wake wakati wenye madaraka huomba na kuficha Uswisi.
Anayetilia hili shaka ajiulize walioficha pesa tena kwa mabilioni ya Kitanzania ni nani kama si wale ombaomba wenye masuti? Ni ombaomba walafi na wenye roho mbaya kuliko Matonya ingawa ombaomba ni ombaomba hata kama amevaa manyang’unyang’u au suti.
Hivyo, kuomba kwa Matonya ilikuwa ni haki yake. Na kweli, kuomba ni bora kuliko kuiba au kujihusisha na ufisadi, mihadarati na jinai nyingine ambazo zimelifikisha taifa letu hapa lilipo. Kwetu sisi Matonya alikuwa matunda ya siasa za kifisi na ubabaishaji. Pia alama na kumbukumbu kwa wenye akili kuwa mambo hayakuwa sawa. Ni bahati mbaya kuwa watawala wetu hawakujifunza suto lililotokana na shughuli za Matonya.
Badala yake walitaka kutumia maguvu kumficha ili asiwaudhi wao na wageni wao, hasa wafadhili. Hakika huu mchezo umekuwa ukiendelea hata nje ya nchi ambapo wazungu huja Tanzania na kupiga picha za watu maskini na kuzipeleka kwao kutengeneza mabilioni kwa kisingizio cha kuhamasisha watu wao matajiri kuwachangia waswahili wenye dhiki. World Vision linaongoza kwa jinai hii. Inashangaza ni kwanini mamlaka zetu haziwazuii hawa wafanyabiashara ya nafsi za watu kupiga hizo picha.
Tukirejea kwa Matonya, alikuwa shujaa aliyewabana watawala wetu. Hata walipowaficha maskini wengi vijijini, yeye alikharifu hujuma hii na kujitokeza na kuomba, hasa jijini Dar es Salaam ambako ni moyo wa nchi.
Matonya atakumbukwa Dar es Salaam, Dodoma na Morogoro (alikoweka makao yake ya muda baada ya kutimuliwa kwa muda mfupi na Makamba kabla hajamdharau na kumshinda na kurejea Dar).
Kifo cha Matonya ni pigo kwa taifa, hasa maskini aliowawakilisha kwenye uso wa nchi kwa kung’ang’ania kuomba badala ya kuiba. Inashangaza watawala wanaosifika kwa kuombaomba kumfukuza ombaomba mwenzao. Je, ni kwa sababu hakuwa ombaomba mwenye suti au anayetumia kalamu?
Ingawa kwa jicho la kawaida Matonya alionekana kuwa mtu wa kawaida, hakuwa mtu wa kawaida. Matonya alikuwa supastaa wa kweli tofauti na hawa masupastaa uchwara wa maigizo na wa siasa wanaochafua maadili na kuwa chanzo cha maangamizi ya umma.
Matonya alikuwa kioo cha jamii iliyoharibikiwa. Jamii ya ufisi, unafiki na kujisahau. Hakuficha udhaifu wake wala mahitajio yake. Alipeperusha bendera ya watu maskini. Matonya alikuwa bora kuliko majizi na majambazi ambayo yameuza rasilimali zetu hadi kufikia kuuza hata bendera yetu.
Alifanya kazi hata kama ilidharaulika tofauti na majambazi na matapeli wanaopewa kazi ya heshima wakaidhalilisha kwa ufisi upogo na uroho wao. Matonya hakuwahi kuibia benki kama wale majambazi wa EPA.
Matonya alihubiri dini ya kweli ya umaskini utokanao na unafiki na ufisi tofauti na wahubiri wengi wa dini ambao ni matapeli. Kama kuna pepo basi asipoingia Matonya hawa majambazi wenye suti wataishia kwenye moto wa aina yake.
Ingawa Matonya alikuwa ombaomba asiyevaa suti kama wale wanaovaa suti, anapaswa kuenziwa kwa kuwa darasa na kioo cha jamii kwa wenye akili na uzalendo. Matonya alikuwa ombaomba wa kutengenezwa na ombaomba wenye masuti. Maskini hakuomba dola wala yen.
Yeye aliomba ili kuishi na siyo kuomba kwa tamaa na roho mbaya kama wanaoomba mabilioni wakayaficha ugenini au kuyatumia kutafuta ukubwa. Kwa Matonya maisha yalikuwa rahisi na ya wazi tofauti na ombaomba wenye mamlaka, ambao hufanya maisha yao kuwa magumu na kujiona miungu.
Matonya hakuomba rushwa iwe ya dola, shilingi, ngono, au ardhi. Matonya hakuomba rushwa ya kusomeshewa watoto wala kutoa upendeleo katika kazi au mtihani. Matonya hakuruhusu mkewe au mtoto wake kutumia nafasi yake. Hatujui kama watoto wake walikuwa ombaomba au vinginevyo tofauti na wenye madaraka ambao hugeuza mali ya familia, ukoo na marafiki hata waramba viatu wao.
Matonya hakuwahi kutoa ajira kwa upendeleo, udugu, rushwa, udini wala jinai yoyote itendwayo na waitendao chini ya kivuli cha madaraka. Matonya hakuhusika na wizi kule TRA, Tanesco, BoT, Maliasili, Uhamiaji, Bandari na kwingineko kunakosifika kwa wizi. Hakuhubiri kutenda miujiza ya kitapeli wala kuwaibia wanyonge, hakuhubiri maji na kunywa mvinyo.
Kama Matonya angegombea urais ningempa kura yangu. Kwani Matonya hakuwa binadamu tu bali mwakilishi wa kweli wa wanyonge. Matonya hakuwakilisha tumbo lake wala kupewa posho za makalio, usingizi na umbea. Ingawa Matonya alionekana kuomba na kula dezo, ukweli ni kwamba alitoa jasho kupewa alichopata. Nenda kapumzike mzee Matonya ulikuwa changamoto kwa wenye akili na udhu.
Chanzo: Tanzania Daima Agosti 29, 2012.

1 comment:

Anonymous said...

NO COMMENTS